Categories
Michezo

Miamba na limbukeni watinga makundi ya ligi ya mabingwa Afrika CAF

Miamba kadhaa wa soka barani Afrika walifuzu kwa hatua ya makundi kuwania taji ya ligi ya mabingwa Afrika kufuatia mechi za marudio ya michujo ya pili iliyosakatwa Jumanne .

Teungueth

Mabingwa mara 9 wa kombe hilo na mabingwa watetezi Al Ahly kutoka Misri walitinga hatua ya makundi kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-0 baada ya kuwacharaza SONIDEP ya Niger magoli 4-0 katika mkumbo wa pili uliosakatwa mjini Cairo Misri Jumanne usiku.

Al Ahly

Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kusini maarufu kama Masandawana walipata ushindi wa jumla wa mabao 5-1 dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana  baada ya kuwapiga wageni Jwaneng mabao 3-1 Jumanne.

Mamelodi Sundowns

Kaizer Chiefs ukipenda Amakhosi ,wakicheza ugenini Luanda walikosa  heshima na kuwapiga kumbo Premeiro De Agosto bao 1-0  na kufuzu kwa makundi ya kombe hilo kwa mara ya kwanza baada ya miaka 24 ,huku limbukeni Teungueth ambao ni mabingwa wa Senegal wakiwaduwaza miamba Raja Casablanca ya Moroko walipowabandua kupitia penati 3-1 kufuatia sare tasa.

Kaizer Chiefs

Timu nyingine iliyotinga awamu ya makundi kupitia kupewa ushindi wa ubwete kufuatia kujiondoa kwa wapinzani wao ni Zamalek kutoka Misri waliocheza hadi fainali ya mwaka jana,waliopewa ushindi baada ya Gazzelle ya Chad kujiondoa.

Mechi zaidi kupigwa Jumatano ambapo ratiba kamili ya timu 16 kucheza hatua ya makundi itabainika.

 

Categories
Michezo

Ahly waibana Zamalek na kutwaa kombe la 9 ligi ya mabingwa Afrika

Kilabu ya Al Ahly ukipenda Red Devils ilinyakua kombe la ligi ya mabingwa barani Afrika kwa mara ya 9 Ijumaa usiku  katika  uwanja wa Cairo International baada ya kuwalemea Zamalek kwenye fainali iliyokuwa derby ya Cairo.

Mohammed Madgy Afsha aliwafungia Ahly bao la ushindi dakika nne kabla ya mechi kukamilika baada ya pambano hilo kuonekana kama lingeamuliwa katika muda wa ziada.

Kiungo Amr Soleya alifungua ukurasa kwa magoli katika mechi hiyo iliyokuwa ya kusisimua alipounganisha tobwe  la Ali Maloul katika dakika ya 6  na kuwaweka Ahly kifua mbele  na kuwafanya Ahly kutawala mechi kwa muda tokea  mwanzoni mwa mechi.

Hata hivyo kiungo mkongwe Shikabala alitumia tajriba yake na kufyatua kombora kali mithili ya fataki, akiunganisha pasi ya Achraf Bencharki na kumwacha kipa wa Ahly Mohammed El Shanawy akiduwaa asiwe na la kufanya na kipindi cha kwanza kukatika kwa sare ya 1-1.

Licha ya kujaribu kurejesha bao hilo ,muda uliwapa kisogo Zamalek  huku Ahly wakijihami zaidi baada ya kocha Pitso Mosimane kufanya mabadiliko ya kiufundi akiwaondoa washambulizi na viungo na kuwajumuisha mabeki na kushikilia uongozi huo hadi kipenga cha mwisho.

Idadi ndogo ya mashabiki waliohudhuria fainali hiyo walipata burudani ya kipee na kufurika uwanjani kushangilia ushindi wa Ahly ikiwa pia historia kwa maya kwanza ambapo fainali hiyo inashirikisha timu hizo za Misri.

Mosimane pia aliingia kwenye madaftari ya kumbukumbu kwa kuishinda Zamalek kwa  mara ya pili katika fainali ya kombe hilo ,baada ya kuwashinda na kunyakua kombe  hilo kwa mara ya kwanza akiwa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini mwaka 2016.

Ahly ndio timu iliyoshinda kombe hilo mara nyingi ikiwa mara 9 na la kwanza tangu mwaka 2013 , huku vilabu kutokea Misri vikinyakua jumla ya vikombe 15 vya ligi ya mabingwa .

 

 

Categories
Michezo

Ahly na Zamalek kuzindua uhasama wa jadi fainali ya ligi mabingwa Ijumaa

Fainali ya ligi ya mabingwa barani afrika itasakatwa Ijumaa usiku katika uwanja wa Cairo International ,ikiwa derby ya Cairo baina ya mabingwa mara 8 Al Ahly dhidi ya Zamalek kuanzia saa nne usiku.

Timu hizo zitakutana kwa mara ya 9 katika kombe hilo la ligi ya mabingwa, Ahly wakiibuka washindi mara  5 na nyingine 3  kuishia sare, lakini zote  zikiwa aidha mechi za makundi au nusu fainali.

Itakuwa mara ya kwanza kwa timu hizo kukutana katika fainali ya kombe  hilo  zikiwania dola milioni 2 nukta 5 na fursa ya kucheza kombe la dunia baina ya vilabu.

Katika mechi za nyumbani timu hizo zimepambana mara  215 Ahly maarufu kama  Red Devils wakishinda mechi  91 ,huku Zamalek wajulikanao kama White Knights wakisajili ushindi kwenye michuano  50  na kurekodi sare 74 .

Ahly wamenyakua ligi ya mabingwa mara 8  ikiwa timu iliyoshinda taji hiyo mara nyingi zaidi na kushinda mataji 4  ya kombe la shirikisho,4 ya African Cup winners cup   na lile la super cup mara 4  kwa jumla wakiwa na vikombe 19 vya Afrika.

Hata hivyo Red Devils wamekawia tangu mwaka 2014 ikiwa mara ya mwisho kwao kunyakua kombe la shirikisho huku yale ya ligi ya mabingwa yakiwakwepa na ndiyo timu iliyokawia muda mrefu zaidi kabla ya kushinda kombe la ligi ya mabingwa.

Al Ahly wakiwa mazoezini

Upande wa pili wa sarafu Zamalek wamewshinda mataji matano ya ligi ya mabingwa ,4 ya Super Cup na moja ya shirikisho na nyingine moja ya African cup winners cup wakiwa na vikombe 11 vya Afrika.

Zamalek iliibuka ya pili katika kundi A nyuma ya Toupiza Mazembe  kabla ya kuwatema waliokuwa mabingwa matetezi Esperance ya Tunisia jumla ya mabao 3-2 katika robo fainali na kuwabandua Raja Casablanca jumla ya mabao 4-1 kwenye nusu fainali.

Ahly nao waliibuka wapili kundini B nyuma ya Etoile du Sahel kabla ya kuibwaga Mamelodi Sundowns magoli 2-1 katika kwota fainali na hatimaye kuwadhalilisha mabingwa wa Moroko Wydad Casblanca  kwa kuwalabua mabao 5-1 katika nusu fainali.

Kocha wa Afrika Kusini Pitso Mosimane alishika hatamu za kuwanoa  Ahly  mwezi Septemba  mwaka huu akitokea Mamelodi Sundowns ya nyumbani ambao alishinda nao kombe hilo la ligi ya mabingwa mara moja .

Jaime Pacheco wa kutoka Ureno alirejea kuwafunza Zamalek pia mwezi Septemba mwaka huu  akiwa hana kazi tangu aigure timu hiyo mwaka 2014.

Zamalek wakiwa mazoezini

Misri itanyakua kombe hilo la ligi ya mabingwa Ijumaa usiku  kwa mara ya 15  likiwa taifa pekee kunyakua mataji mengi zaidi kwani awali Zamalek wameibuka mabingwa mara 5 nao Ahly wakashinda mara 8 wakati Ismaily ikishinda kombe moja.

Ahly wameshinda kombe la ligi ya mabingwa mwaka 1982 ,1987,2001,2005,2006,2008,2012 na 2013  na kupoteza fainali mara 4 ,ya mwisho ikiwa mwaka 2018.

Zamalek wametawazwa mabingwa miaka ya 1984 ,1986 ,1993,1996 na 2002  na kushindwa katika fainali mara mbili  ya mwisho ikiwa 1996.

Fainali hiyo kati ya Al Ahly  na Zamalek itapeperushwa mbashara kupitia KBC Channel one kuanzia saa nne usiku

 

 

 

Categories
Michezo

Zamalek waipakata Raja Casablanca na kutinga fainali ya ligi ya mabingwa

Zamelek walijikatia tiketi kucheza derby ya fainali kuwania kombe la ligi ya mabingwa barani Afrika kufuatia ushindi mkubwa wamabao 3-1 dhidi ya Raja Casablanca Jumatano usiku katika marudio ya nusu fainali ugani Cairo.

Zamalek ambao wamenyakua kombe hilo mara 5, walikuwa na wakati mgumu huku wageni Raja wakichukua uongozi kunako dakika ya 61 kupitia kwa  Ben Malango,  kabla ya Ferjani Sassi ,kusawazisha naye  Mostafa Mohammed akafunga mabao mawili ya haraka katika dakika za 84 na 87 mtawalia na kuwapa wenyeji fursa ya kuwania kombe la 6.

 

Ni mara ya kwanza kwa Zamalek maarufu kama White Nights  kucheza fainali hiyo tangu wapoteze mwaka 2016 kwa Mamelodi  Sundowns.

Zamalek walifuzu kwa fainali hiyo ya Novemba 27 dhidi ya Al Ahly katika uwanja wa Borg El Arab mjini Alexandria ,baada ya kuwapiku Raja Casablanca kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-1 kufuatia ushindi wa bao 1-0 katika duru ya kwanza ya nusu fainali.

Ahly wametwaa kombe hilo mara 8 na walitinga fainali kufuatia ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Wydad Casablanca ya Moroko  kumaanisha kuwa kombe hilo litanyakuliwa na timu ya Misri.

Mshindi wa fainali ya Novemba 27 atatuzwa kombe dola milioni 2 nukta 5 za Marekani na nafasi ya kucheza fainali ya kombe la dunia baina ya vilabu mwezi ujao nchini Qatar.

Categories
Michezo

Zamalek na Raja kumaliza udhia Jumatano

Washindi  mara tano wa ligi ya mabingwa barani Afrika ,Zamalek watawaalika Raja Casablanca katika duru ya pili ya nusu fainali Jumatano usiku  katika uwanja wa kimtaifa wa Cairo ,huku wenyeji wakiongoza bao 1-0 kutokana na mkumbo wa kwanza.

Achraf Bencharki aliwafungia Zamalek bao pekee na la ushindi Oktoba 18 mjini Casablanca kabla ya marudio kuahirishwa mara mbili kutokana na zaidi ya wachezaji 11 wachezaji wa Casablanca kupatikana na ugonjwa wa Covid 19.

Itakuwa mara ya nne kwa Zamalek kukutana na Raja katika kipute hicho huku Zamalek wakishinda mechi mbili na mchuano mmoja kuishia sare.

Zamalek watahitaji sare tu ili kufuzu kucheza na Al Ahly katika fainali ya Novemba 27 huku Raja wakihitaji ushindi wa mabao 2-0 ili kugeuza  matokeo ya kwanza na kufuzu kwa fainali.

Mshindi wa fainali ya Novemba 27 atatuzwa  dola milioni 2 nukta 5 na nafasi ya kushiriki fainali ya kilabu duniani mwezi ujao nchini Qatar.

 

Categories
Michezo

Fainali ya Ligi ya Mabingwa Caf ni Novemba 27

Fainali ya kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika itaandaliwa  Novemba 27  katika uwanja wa Borg Al Arab Stadium mjini  Alexandria,Misri.

Kwa mjibu wa Kamati andalizi ya  mashindano hayo ya baina ya vilabu  marudio ya nusu fainali ya pili kati ya Zamalek na mabingwa wa Moroko Raja Casablanca itakuwa tarehe 4 Novemba katika uwanja wa kimataifa wa Cairo.

Nusu fainali hiyo ilikuw aipigwe Novemba mosi lakini ikaahirishwa kutokana na wachezaji 11 wa timu ya Casablanca kupatikana na ugonjwa wa Covid 19 na hivyo kuzuiliwa kusafiri hadi Misri na Serikali ya Kifalme ya Moroko.

Zamalek wanaongoza bao 1 kwa bila kutokana na mkumbo wa kwanza huku mshindi akichuana dhidi ya mabingwa mara 8 Al Ahly ambao walitinga fainali kwa ushindi wa jumla ya mabaoa 5-1 katika nusu fainali .

Mechi hizo zimeratibiwa upya kufuatia agizo la chama cha soka nchini Misri ambao ni mwandalizi wa mechi hizo ,kuambatana na masharti ya kimataifa dhidi ya Ugonjwa wa Covid 19.

Mshindi wa kombe hilo atashiriki kombe la dunia baina ya vilabu ,kipute kitakachoandaliwa nchini Qatar kati ya Desemba 11 na 21 mwaka huu kando na zawadi ya  Dola Milioni 2 nukta 5.

 

 

Categories
Michezo

Fainali ya ligi ya mabingwa Afrika yaahirishwa na Caf

Shirikisho la kandanda Afrika Caf limelazimika kuarisha fainali ya ligi ya mabingwa iliyokuwa ichezwe Novemba 6  kwa sababu zisizoweka kuepukika.

Kulingana na taarifa ya Caf kuahirisha  huko kumechangiwa na kucheleweshwa kwa pambano la marudio la nusu fainali baina ya Zamalek ya Misri inayopaswa kuwaalika Raja Casablanca  ya Moroko kufuatia hatua ambapo wachezaji zaidi ya 10 wa Raja walipatikana na virusi vya Korona na kulalimisha serikali ya Moroko kuwazuilia kusafiri.

Nusu fainali hiyo ilikuwa imepangwa kuchezwa Jumapili ya Oktoba 31 lakini kwa sasa itasubiri hadi wachezaji wa Raja wapone kutokana na ugonjwa wa Covid 19.

Caf wamelazimika kusongeza mbele fainali hiyo ili kutoa fursa kwa mechi za kimataifa za kufuzu kwa  kombe la Afcon zitakozochezwa baina ya wiki ya kwanza na wiki ya pili ya mwezi ujao .

Al Ahly wametinga fainali baada ya kuwagaragaza  Wydad Casblanca kutoka Moroko jumla ya mabao 5-1 katika nusu fainali ya kwanza wakati Zamalek wakiongoza bao 1 kwa bila kutokana na duru ya kwanza ya nusu fainali.

Mabingwa wa kombe hilo watatunukiwa dola milioni 2  nukta 5 pamoja nafasi ya kushiriki kombe la dunia baina ya vilabu.

Categories
Michezo

Caf huenda ikalazimika kufutilia mbali nusu fainali kati ya Zamalek na Raja Casablanca

Shirikisho la kandanda barani Afrika Caf , huenda likalazimika kufutilia mbali marudio ya nusu fainali ya ligi ya mabingwa  kati ya Zamalek ya Misri na Raja Casablanca ya Moroko ,baada ya wachezaji   16 wa Raja kupatikana na ugonjwa wa Covid 19.

Zamalek walikuwa wamesajili ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya  Raja Casablanca  katika uwanja wa  Mohamed V ,huku mechi ya marudio iliyokuwa ichezwe Jumamosi iliyopita ikiahirishwa baada ya wachezaji 8 wa kikosi cha Raja kupatikana na Covid 19.

Kufuatia hatu hiyo serikali ya Moroko ilipiga marufuku usafiri wa kuingia na kutoka nchini humo na kulazimu shirikisho la soka kuandika barua kwa Caf  kuomba  pambano hilo liahirishwe.

Caf ilikubali kuahirisha nusu fainali hiyo hadi Novemba Mosi ,lakini kulingana na taarifa za hivi punde Serikali ya Moroko haituruhusu wachezaji hao kusafiri hadi misri kwa mchuano huo wa Jumapili hii kufuatia kuongeza kwa visa vya wachezaji walioambukizwa Covid 19.

Uchunguzi mwingine utafanyiwa wachezaji hao Jumanne hii kabla ya uamuzi wa mwisho kutolewa.

Fainali ya ligi ya mabingwa Afrika Caf imeratibiwa Novemba 6 huku Caf ikisisitiza kuwa haitaahirisha tarehe ya fainali liwe liwalo.

 

 

Categories
Michezo

Caf yalizimika kuaahirisha mechi ya Zamalek na Raja Casablanca

Shirikisho la soka Afrika Caf limelazimika kuahirisha marudio ya nusu fainali kati ya Zamalek ya Misri dhidi ya Raja Casablanca ya Moroko.

Caf imechukua hatua hiyo baada ya wachezaji wote wa Casablanca kuingia Karantini kufuatia kisa ambapo wachezaji wake wanane wa kikosi cha kwanza kupatikana na Covid 19.

Serikali ya Moroko imefutilia mbali kibali cha usafiri nje ya nchi walichokuwa wameipa timu ya Raja huku wachezaji wote wakitengwa wa wiki moja hadi Oktoba 27 wakati vipimo vipya vitafanyiwa wachezaji hao kwa mara ya pili.

Raja walipangiwa kuchuana na Zamalek Oktoba 24 katika mechi ya marudio ya nusu fainali ,pambano ambalo litaratiwa upya na Caf huku  Zamalek wakiongoza  bao 1 kwa bila kutokana na duru ya kwanza.

Hata hivyo Caf imesisitiza kuwa fainali ya ligi ya mabingwa itasalia ilivyopangwa tarehe 6 Novemba.

Marudio ya nusu fainali ya kwanza ni ijumaa ,mabingwa mara 8 Al Ahly wakiwakaribisha Wydad Casablanca ya Moroko ,wenyeji wakiongoza mabao 2-0 kutokana na mkondo wa kwanza wiki iliyopita.

Mshindi wa kombe hilo kutuzwa dola milioni  1 nukta 5 na pia kujikatia tiketi kwa mashindano ya kombe la dunia baina ya vilabu.

 

 

 

 

Categories
Michezo

Raja Casablanca walimwa nyumbani na Zamalek

Miamba wa soka nchini Misri Zamalek walijiweka katika nafasi nzuri ya kutinga fainali ya kipute cha ligi ya mabingwa Africa Caf baada ya kukosa heshima za mgeni na kuwaadhibu Raja Casablanca ya Moroko  bao 1-0  katika duru ya kwanza ya semi fainali Jumapili usiku.

Katika mchuano huo uliopeperushwa mbashara na runinga ya Kbc ulishuhudia wenyeji Casablanca wakitawala mechi kwa kipindi kirefu lakini wakakosa kumakinika mbele ya lango la Zamalek.

Bencharki wa Zamalek akisherehekea bao na wenzake

Achraf Bencharki  ambaye ni raia wa Moroko alirejea nyumbani katika uwanja wa Complex Mohammed V na  kuwafungia Zamalek bao la pekee na la ushindi kunako dakika ya 18  kipindi cha kwanza kwa njia ya kichwa  .

Zamalek walicheza mchezo wa kujihami katika kipindi cha  pili chote na kunusurika kwa ushindi huo maridhawa.

Mkondo wa pili utachezwa katika uwanja wa kimataifa wa Cairo Jumamosi hii .

Timu za Misri zilisajili matokeo mazuri ugenini nchini Moroko  huku pia mabingwa mara 8 Al Ahly pia walikuwa wamewashinda Wydad Casablanca ya Moroko Jumamosi iliyopita mjni Casablanca na watapiga mechi ya marudio Jumapili hii.