Categories
Kimataifa

Maafisa wa usalama nchini Uganda washtumiwa kwa kuwajeruhi wanahabari waliokuwa wakiripoti kumhusu Bobi Wine

Muungano wa Wahariri nchini Uganda umeshtumu vikali vikosi vya usalama nchini humo (UPDF) baada ya kuwajeruhi wanahabari kadhaa waliokuwa wakiripoti habari kumhusu mwanasiasa Robert Kyagulanyi.

Wanahabari hao walikuwa wameandamana na mwanasiasa huyo almaarufu Bobi Wine akiwasilisha malalamshi kwa afisi za Umoja wa Mataifa kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu nchini humo.

Mashahidi wanasema kuwa wanajeshi waliwasili kwa malori nje ya afisi za kutetea haki za binadamu za Umoja wa Mataifa (UNHRC) katika mji mkuu wa taifa hilo Kampala na kuanza kuwapiga wanahabari.

Kulingana na taarifa ya muungano wa wahariri nchini humo, angalau wanahabari 10 wa mashirika tofauti ya habari walijeruhiwa kabla kupelekwa hospitalini kwa matibabu.

Mwanahabari mmoja aliweka katika mtandao wa Twitter, picha za yaliyokuwa yakijiri katika eneo hilo huku akionyesha mmoja wa wanahabari akitokwa na damu kichwani.

Kituo kimoja cha kibinafsi cha runinga kilionyesha picha za wanahabari wakitoroka ili kuepuka kucharazwa.

Akijibu shutuma hizo, Msemaji wa vikosi hivyo vya usalama Brigadia Generali Flavia Byekwaso amesema kundi lililoandamana na Bobi Wine walijeruhi afisa mmoja wa usalama ndiposa ikabidi wafurushwe kwa nguvu.

Kuna wasi wasi nchini Uganda kuhusu hatima ya wafuasi wa upinzani ambao wamesemekana kutoweka.Waliokamatwa wamesemekana kuteswa.

Rais Yoweri Museveni hivi maajuzi alisema kuwa watu 300 wamezuiliwa kwa kuzua vurugu na kuhusika na visa vingine vya uhalifu.

Categories
Habari

Wanakandarasi watakiwa kukamilisha mabwawa kabla ya mwezi Septemba

Waziri wa ugatuzi  Eugene Wamalwa amewaagiza wanakandarasi wote wanaojenga mabwawa katika kaunti za Turkana, Marsabit na Pokot magharibi kuhakikisha kuwa mabwawa hayo yanakamilishwa kabla ya mwezi Septemba mwaka huu.

Akiongea alipozindua kisima kinachotumia kawi ya jua katika eneo la Lokiriamet katika kaunti ndogo ya  Loima katika kaunti ya Turkana,  Wamalwa aliwaambia maafisa wa serikali ya kitaifa na serikali za kaunti husika kuwaharakisha wanakandarasi hao na kuhakikisha kuwa miradi hiyo inakamilika kufikia mwezi September.

Alisema kuwa Rais  Kenyatta na mwenzake wa  Uganda walitia saini mkataba wa makubaliano mwaka wa 2019 ambao utashuhudia Kenya ikijenga mabwawa makuu kama yale yaliyoko katika eneo la Kobebe nchini  Uganda ili kuzuia mizozo ya kung’anga’nia maji.

Alisema kuwa ishara za ukame zimeripotiwa huku akiongeza kuwa mabwawa hayo yatawakinga wakazi kutokana na ukame.

Kisima hicho kilichimbwa na shirika la JICA ambalo liliweka pampu ya kawaida ambayo baadaye iliboreshwa na kufanywa kutumia kawi ya jua na kampuni ya uhandisi ya  Trevcon.

Categories
Kimataifa

Mahakama ya Uganda yaagiza Bobi Wine aachiliwe huru

Mahakama moja nchini Uganda imetoa agizo kwa maafisa wa usalama kuondoka nyumbani kwa mwanasiasa wa upinzani Bobi Wine.

Hii ni baada ya mahakama hiyo kuitaja hatua ya kumuweka Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine, kwenye kifungo cha nyumbani kuwa isiyo halali.

Mwanasiasa huyo hajaweza kutoka nyumbani kwake tangu aliporudi kutoka kituo alikopigia kura katika uchaguzi mkuu nchini humo siku 11 zilizopita.

Agizo la kuachiliwa huru kwa Bobi mapema Jumatatu limetolewa kufuatia uamuzi wa kesi iliyowasilishwa na mawakili wake ya kupinga hatua ya maafisa wa usalama wa serikali kuendelea kuzingira makazi yake.

Hatua hiyo ilishutumiwa vikali na baadhi ya viongozi na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu ulimwenguni lakini maafisa hao wakadai kwamba Bobi alikuwa akipewa ulinzi kwa sababu alikuwa mgombea urais.

Tume ya uchaguzi nchini humo ilimtangaza Bobi kuwa aliibuka nafasi ya pili kwenye kinyang’anyiro cha urais, baada ya kushindwa na Rais Yoweri Museveni.

Hata hivyo, Bobi alipinga vikali matokeo hayo, akidai kwamba anao ushahidi wa kutosha wa kudhihirishwa kuwa kulikuwa na udanganyifu mkubwa katika shughuli ya kuhesabu na kujumlisha kura hizo.

Categories
Kimataifa

Marekani yataka kuchunguzwa kwa ghasia za uchaguzi nchini Uganda

Muungano wa Ulaya na Marekani zimetoa wito wa uchunguzi kufanywa kuhusiana na ghasia za uchaguzi zilizotokea nchini Uganda huku kiongozi wa upinzani nchini humo Bobi Wine akiendelea kuzuiliwa nyumbani.

Rais Yoweri Museveni alitangazwa mshindi kwa hatamu ya sita huku mtandao wa internet ukifungwa na madai ya unyanyasaji wa watu yakitolewa.

Viongozi wa upinzani na wafuasi wa upinzani nchini humo wamelalamika kutokana na visa vya kuhangaishwa na maafisa wa usalama kabla na baada ya uchaguzi huo.

Msemaji wa serikali ya Uganda Jumanne alimtuhumu balozi wa Marekani nchini  Uganda Natalie Brown kwa kukiuka maadili ya kibalozi kwa kujaribu kumtembelea kiongozi wa upinzani  Bobi Wine, ambaye anazuiliwa nyumbani kwake.

Wine, mwenye umri wa miaka 38, aliibuka wa pili kwenye uchaguzi huo wa urais ambao ulimdumisha mamlakani Yoweri Museveni kwa hatamu ya sita na amesema ametenganishwa na mawakili wake na chama huku akinuia kupinga matokeo ya uchaguzi huo mahakamani.

Msemaji wa serikali ya nchi hiyo Ofwono Opondo alisema jaribio hilo  la Brown ni ishara kuwa hana nia njema.

Categories
Kimataifa

Mtandao warejeshwa Uganda baada ya kufungwa wakati wa uchaguzi mkuu

Huduma ya mtandao imerejeshwa nchini Uganda baada ya kuzimwa kwa siku tano wakati wa uchaguzi mkuu.

kufuatia agizo la serikali, huduma hiyo ilifungwa Jumatano usiku, saa chache kabla ya kufunguliwa kwa vituo vya kupigia kura kwenye uchaguzi mkuu wa siku ya Alhamisi iliyopita.

Hata hivyo, mitandao ya kijamii bado imesalia kufungwa.

Wakati uo huo, msemaji wa chama cha upinzani cha National Unity Platform (NUP), Joel Ssenyonyi, amesema afisi ambapo mawakala wake walikuwa wakiandaa stakabadhi za kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi huo zimevamiwa na wanajeshi.

Ssenyonyi amesema mawakala hao walikuwa wakikusanya fomu za matokeo ya uchaguzi zilizo na ushahidi wa udanganyifu.

Hii ni baada ya makaazi  ya kiongozi wa chama hicho Bobi Wine kuzingirwa na wanajeshi wa serikali.

Bobi alikataa matokeo ya uchaguzi wa urais kama yalivyotangazwa na tume ya uchaguzi nchini humo.

Kulingana na matokeo hayo, Rais Yoweri Museveni ndiye aliyeshinda kinyang’anyiro hicho dhidi ya Bobi Wine aliyeibuka wa pili.

Bobi alishtumu vikali jinsi uchaguzi huo ulivyofanywa, huku akidai kwamba ana ushahidi wa kutosha kuhusu visa vya udanganyifu.

Categories
Kimataifa

Bobi Wine sasa adai maisha yake yamo hatarini

Mgombeaji urais wa mrengo wa upinzani nchini Uganda, Bobi Wine, amesema anahofia maisha yake.

Hii ni baada ya mgombea huyo kukataa matokeo ya uchaguzi mkuu nchini humo ambapo Rais Yoweri Museveni alihifadhi kiti chake.

Mwanasiasa huyo amesema kuwa alikataa matokeo ya uchaguzi huo, kwani hakutendewa haki, akihoji kwamba ulikumbwa na udanganyifu mwingi.

Bobi Wine, ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi, amesema anahofia maisha yake na yale ya mkewe.

Anasema hajaruhusiwa kuondoka  nyumbani kwake kwani nyumba hiyo imezingirwa na maafisa wa usalama.

Licha ya Bobi kudai kuwa kulikuwa na visa vingi vya udanganyifu kwenye uchaguzi huo, Rais Museveni ameutaja kuwa wa huru na haki.

Kampeni za kabla ya uchaguzi huo zilighubikwa na ghasia huku watu kadhaa wakiuawa.

Serikali ilifunga huduma za mitandao kote nchini humo siku ya kuamkia kupiga kura.

Categories
Habari

Rais Kenyatta ampongeza Museveni kwa kuhifadhi kiti cha urais nchini Uganda

Rais Uhuru Kenyatta amempongeza Yoweri Museveni kwa kuchaguliwa tena kuwa Rais wa Uganda.

Siku ya Jumamosi, Tume ya Uchaguzi nchini humo ilimtangaza Museveni kuwa mshindi wa uchaguzi huo mkuu kwa kujizolea zaidi ya asilimia 58 ya jumla ya kura za urai.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, Museveni alimshinda mpinzani wake mkuu, Bobi Wine, aliyepata asilimia 34 ya kura hizo zilizopigwa mnamo siku ya Alhamisi.

Kupitia ukurasa wa Facebook wa Ikulu ya Kenya, Rais Kenyatta amesema kuchaguliwa tena kwa Museveni ni ushuhuda tosha wa imani waliyonayo wananchi wa Uganda kwa uongozi wake.

Kwenye ujumbe wake wa heri, Rais Kenyatta pia ameahidi kuendelea kushirikiana na Museveni ili kuimarisha zaidi uhusiano kati ya Kenya na Uganda kwa ajili ya manufaa ya wananchi wa mataifa hayo mawili.

Kiongozi wa taifa pia ameusifu uongozi wa Museveni kwa kuimarisha nchi hiyo na vile vile kuandikisha maendeleo bora ya kiuchumi nchni humo.

Museveni, mwenye umri wa miaka 76, amekuwa uongozini tangu mwaka wa 1986 na ushindi wake sasa unamaanisha kwamba ataiongoza Uganda kwa muda usiopungua miaka 40 kama rais.

Hata hivyo, upande wa upinzani tayari umepinga matokeo hayo, huku Bobi Wine akiahidi kutoa ushahidi wa kuonyesha kwamba kulikuwa na udanganyifu mwingi kwenye shughuli ya kuhesabu na kujumlisha kura hizo.

Categories
Kimataifa

Yoweri Museveni atangazwa mshindi katika uchaguzi mkuu wa Urais

Rais wa Uganda aliyetawala wa muda mrefu Yoweri Museveni, amechaguliwa tena kwa muhula wa sita.

Hayo ni kulingana na tangazo lililotolewa na tume ya uchaguzi nchini humo, huku kukiwa na madai ya udanganyifu wa kura kutoka kwa mpinzani wake mkuu Bobi Wine.

Museveni alipata karibu asilimia 59 ya kura, huku Bobi Wine akifuata kwa asilimia 35.

Awali, Wine ambaye ni mwana-Muziki wa zamani, aliahidi kutoa ushahidi wa kuonyesha kwamba kulikuwa na udanganyifu.

Hata hivyo, tume ya uchaguzi imekanusha kwamba kulikuwa na udanganyifu wowote kwenye uchaguzi huo wa siku ya Alhamisi.

Waangalizi wa uchaguzi huo wamekashfu hatua ya serikali kufunga huduma za internet, wakisema hatua hiyo ilihujumu imani.

Wine ameahidi kutoa ushahidi wa kuonyesha kulikuwa na udanganyifu mara tu huduma za internet zikirejeshwa.

Watu kadhaa waliuawa wakati wa ghasia zilizoghubika kampeini za uchaguzi huo.

Wanasiasa wa upinzani pia wameshtumu serikali kwa kuwahangaisha.

Museveni mwenye umri wa miaka -76 ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1986 – amesema anawakilisha udhabiti nchini humo.

Categories
Kimataifa

Museveni aongoza katika matokea ya awali ya kura za Urais

Rais Yoweri Museveni wa Uganda amechukua uongozi wa mapema kwenye matokeo ya mwanzo ya uchaguzi wa urais yaliotangazwa na tume ya uchaguzi nchini humo Ijumaa asubuhi.

Museveni amezoa kura-1,852,263 hiyo ikiwa ni asilimia-63.09 naye mpinzani wake mkuu, Robert Kyagulanyi al-maarufu Bobi Wine ana kura-821,875 hiyo ikiwa ni asilimia 28.36 ya kura zilizohesabiwa kutoka vituo-8,310 vya kupigia kura.

Kuna jumla ya vituo-34,684 vya kupigia kura nchini Uganda.

Wakati huo huo, tume ya uchaguzi nchini humo imetoa hakikisho kuwa matokeo ya uchaguzi yanawasilishwa moja kwa moja hadi kituo kikuu cha kujumulishia matokeo hayo licha ya kufungwa kwa huduma za internet kote nchini humo.

Mkuu wa tume hiyo, Simon Byabakama amesema wanatumia mbinu mbadala kuwasilisha matokeo hayo lakini hakufafanua.

Chini ya sheria za Uganda, tume ya uchaguzi inapasa kuthibitisha matokeo yaliowasilishwa kutoka wilaya zote na kuyatangaza rasmi saa 48 baada ya uchaguzi kukamilika.

Washindi wa viti vya ubunge watatangazwa katika vituo vya kujumulishia matokeo wilayani ilihali mshindi wa kiti cha urais atatangazwa katika kituo cha kitaifa cha kujumulishia matokeo mjini Kampala.

Categories
Kimataifa

Zoezi la kuhesabu kura laendelea nchini Uganda

Shughuli ya kuhesabu kura inaendelea katika baadhi ya vituo vya kupigia kura katika mji mkuu wa Uganda wa Kampala.

Maafisa wa usalama waliongezeka saa ya mwisho kabla ya vituo vya upigaji kura kufungwa saa kumi alasiri.

Malori yaliowabeba wanajeshi yaliendeshwa jijini, ilhali polisi na vitengo vya ulinzi pia walionekana wakishika doria. Katika baadhi ya sehemu, shughuli ya upigaji kura inaendelea.

Kanuni za uchaguzi zinaratibu kuwa watu walioko kwenye milolongo wanaweza kupiga kura baada ya muda rasmi ya kufungwa vituo vya kupigia kura.

Kiongozi wa taifa hilo la Afrika ya Mashariki Yoweri Kaguta Museveni, ameliongoza kwa muda wa miaka 35 sasa huku akijizatiti kuchaguliwa kwa muhula mwingine.

Licha ya kuwa kuna wagombea wengine 10 katika kinyang’anyiro hicho cha urais nchini Uganda, Museveni aliye na miaka 76 anakabiliwa na ukinzani mkali kutoka kwa Bobi Wine mwenye umri wa miaka 38 ambaye ni mwanamuziki aliyegeuka kuwa mwanasiasa.

Awali shughuli ya kupiga kura katika ngome ya upinzani ya Masaka nchini Uganda ilichelewa kwa muda licha ya raia kujitokeza kwa wingi mapema asubuhi.

Kuchelewa kwa shughuli hiyo kutokana na agizo la kusitisha huduma za mitandao hapo jana.

Aidha kuna visa kadhaa vya kufeli kwa mitambo ya kutambua wapiga kura kielektroniki.

Mitambo hiyo hutegemea huduma za Internet ambazo zimekatizwa nchini humo huku milolongo ya wapiga kura ikiendelea kurefuka kwenye vituo vya kupigia kura.

Raia wa Uganda waliofanikiwa kupata huduma za Internet walipachika jumbe kwenye mitandao ya kijamii kuelekezea shida zinazowasibu kuwasiliana kwa njia ya rununu.