Naibu Rais Dkt. William Ruto amesema atapiga jeki biashara ya kilimo ya mama Margaret Njambi mwenye umri wa miaka 64.
Njambi almaarufu “Cucu wa Gikandu” alijulikana baada ya video yake kutamba mitandaoni akipinga ripoti ya BBI mapema mwezi huu.
Ufahamu wake wa lugha ya Kingereza uliwafurahisha wakenya alipokuwa akimhimiza mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro amkutanishe na naibu Rais William Ruto.
Ombi lake lilitimia baada ya kukutana ana kwa ana na naibu wa rais mtaani Karen siku ya Jumatano.
“Nilizungumza na Margaret Njambi ambaye ni mkulima baada ya video yake kutamba katika mitandao ya kijamii wakati wa mkutano kuhusu maendeleo katika eneo bunge la Kiharu ambapo alielezea angependa kukutana na naibu Rais,” alisema Ruto.
Baadae Naibu Rais aliomboleza na familia ya marehemu mbunge John Oroo Oyioka nyumbani kwake Kitengela kaunti ya Kajiado.
Naibu Rais pia aliomboleza na familia ya marehemu mbunge wa Juja Francis Munyua Waititu nyumbani kwake Juja kaunti ya Kiambu.
“Tunaomba Mwenyezi Mungu apatie familia hizo nguvu na pia azifariji wakati huu ngumu wa majonzi,” alisema naibu rais.