Categories
Burudani

Eric Omondi apimana nguvu na Diamond Platnumz

Mchekeshaji huyo wa nchi ya Kenya anamtania mwanamuziki wa Tanzania Diamond Platnumz kwa kile ambacho anakitaja kuwa kushambulia Afrika mashariki kwa kupata wapenzi na watoto.

Eric anasema alimwonya Diamond kwamba atalipiza kisasi lakini hakuamini na kwamba anajua sasa ameshachoka kukimbizana na wapenzi analea watoto.

Diamond Platnumz ana watoto na wapenzi wake wa zamani kwenye nchi zote za Afrika mashariki ambazo ni Kenya, Uganda na Tanzania.

Nchini Kenya ana mtoto na msanii Tanasha Donna ambaye anaitwa Naseeb Junior kama yeye na siku yao ya kuzaliwa ni moja, ukienda Uganda ana Zari Hassan ambaye ana watoto wake wawili, Princess Tiffah na Prince Nillan na kwao Tanzania anayejulikana ni Hamissa Mobeto ambaye ana mtoto kwa jina Dillan.

Eric alitoa video inayomwonyesha akiwa na mwanamuziki na muigizaji wa Tanzania Gigy Money ambaye ni rafiki wa karibu wa Diamond Platnumz anapoanza kulipiza hatua ya Diamond ya kunyakua warembo Afrika Mashariki.

Wimbo ambao ametumia kwenye video hiyo ni “Kwaheri” ambao umeimbwa na Jua Cali na Sanaipei Tande ishara kwamba Gigy amehama Tanzania na kumwacha Diamond na kuja Kenya kwa Eric Omondi japo yote hayo ni uigizaji tu.

Kulingana na maneno, picha na video kutoka kwa Eric Omondi kwenye mitandao ya kijamii, Gigy Money na Betty Kyallo huenda wakawa wahusika kwenye awamu ya pili ya kipindi chake “Wife Material”.

Categories
Burudani

Shosholites, Eric Omondi

Baada ya kumalizana na kipindi cha awali ambacho kilichanganya wengi kwa jina “Wife Material” muigizaji Eric Omondi amezamia kingine kwa jina “Shosholites”.

Kwenye wife material alihusisha mabinti wengi wakidhani kwamba kweli alikuwa akitafuta mke kikweli. Alichagua binti mmoja mwimbaji katika Band Beca mpaka wakafunga arusi ambayo wengine walidhania ni ya ukweli ila yote yalikuwa maigizo tu.

Kwa muda sasa, Eric omondi amekuwa akiachilia picha na video zinazoonyesha kina mama wazee ambao wanajaribu mitindo ya kisasa ambayo inachukuliwa na wengi kuwa ya wanawake wa umri mdogo kama vile kujipodoa.

Kwenye maelezo ya hizo picha na video Eric alionekana kuhimiza wafuasi wake kumtumia video za nyanya zao wakifanya mambo yasiyo ya kawaida kwa umri wao na huenda wakajishindia hela.

Mshindi atapatiwa laki moja, atakayeibuka wa pili atajinyakulia shilingi elfu hamsini, wa tatu elfu thelathini na nambari nne atapatiwa majani chai ya mwezi mzima na kampuni ya Old Farm.

Kampuni hiyo ya Old Farm Tea ndiyo inadhamini kipindi hicho cha Eric Omondi kwa jina Shosholites ambacho kinazinduliwa leo kwenye akaunti ya Eric Omondi ya Youtube.

Kulingana naye, hili litakuwa shindano la kipekee la talanta.

Eric Omondi na wachekeshaji wengine wanaonekana kugeukia mitandao ya kijamii ili kuendeleza fani yao kutokana na masharti mengi ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya korona.

Masharti hayo yamepiga marufuku mikutano mikubwa na ile ya usiku maanake kuna kafyuu ya saa nne usiku hadi saa kumi alfajiri.

Lakini maajuzi yeye na Mc Jessy wametumbuiza nchini Tanzania ambapo hakuna masharti makali baada ya serikali nchini humo kutangaza mwaka jana kwamba ugonjwa wa Covid 19 ulikuwa umeisha.

Categories
Burudani

Ezekiel Mutua ataka Eric Omondi akamatwe

Mkurugenzi mkuu wa bodi ya kuorodhesha filamu nchini Kenya Daktari Ezekiel Mutua sasa anataka mchekeshaji Eric Omondi akamatwe.

Kulingana naye, Eric amekuwa akiendesha danguro kwenye kipindi chake cha mitandaoni kwa jina “Wife Material” huku akikisingizia kuwa mpango wa ushauri kwa wasichana hao.

Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Mutua anamkosesha Eric kwa kuonekana wazi akibusu wasichana tofauti kati ya waliokuwa kwenye shindano hilo, ilhali kuna ugonjwa wa Covid 19.

Analaumu mmoja wa walioalikwa kufundisha wasichana hao kwa kuwafunza jinsi ya kujamiiana na Eric Omondi akitaja kitendo hicho kuwa cha kishetani.

Kulingana naye, studio ambazo Eric Omondi alizindua katika eneo la Lavington hazisaidii vijana jinsi alikuwa amepanga lakini zinatumika kudhulumu wasichana. Anahimiza makachero wa DCI kuzuru eneo hilo na kumkamata mmiliki .

Ezekiel pia analaumu makundi ya kutetea haki za wanawake akisema yako kimya wanawake wenzao wakidhulumiwa. Bwana Ezekiel Omondi huwa anaendesha kampeni ya kuhakikisha kwamba video chafu au ambazo zinavuruga maadili na hata muziki havionyeshwi hadharani.

Ezekiel na Eric wamewahi kujipata wakizozana tena pale ambapo Ezekiel alimkosoa Eric kwa kupiga picha akiwa nusu uchi.

Wakati huo Eric alikuwa anajitayarisha kufungua studio zake ambazo anasema zitahudumia vijana bure bila malipo kwa nia ya kuendeleza sanaa na talanta.
Baadaye Eric alimfokea Mutua akimwambia aache kutaja jina lake.

Categories
Burudani

Shakilla asema ana ujauzito wa Eric Omondi!!

Baada ya kushindwa kwenye shindano la “Wife Material” ambalo lilikuwa la kumtafutia mke mchekeshaji Eric Omondi, Shakilla msichana wa vituko vingi amejitokeza na kudai kwamba ana ujauzito wa Eric na mwanawe mtarajiwa hawezi kulelewa mitaani bila baba.

Shakilla ambaye ni maarufu kwenye mtandao wa Instagram anasema mimba hiyo ni ya wiki mbili tu. Swali ni, anajuaje ni mtoto wa kike anatarajia? (Hii ni baada yake kurejelea mwanawe kama “Princess”.)

Kwenye Instagram, Shakilla alipachika video akimpongeza Carol wa Band Beca kwa kuchaguliwa na wakenya kuwa mke wa Eric Omondi lakini akaendelea kwa kusema kwamba Eric na yeye wanajua kwamba walifungamana milele na hakuna awezaye kuvunja uhusiano huo.

Hapo ndipo alimwaga mtama kwamba ana ujauzito.

Shakilla amekuwa akijitafutia umaarufu kwa njia zote kwenye mitandao ya kijamii jambo ambalo limesababisha afanye vituko. Wakati mmoja alivua nguo na kucheza akiwa mubashara kwenye Instagram na mwanamuziki Tory Lanez wa Canada.

Wakati mwingine alitiwa mbaroni kwa kuingia kwenye makazi ya mwanamuziki Willy Paul bila mwaliko na Willy akamshtaki kwa polisi.

Baadaye alidai kwamba anamiliki jumba la kifahari na kwamba anaishi maisha mazuri lakini picha zikasambazwa mitandaoni zikimwonyesha akipika ndani ya nyumba ya chumba kimoja almaarufu “bedsitter”.

Huku haya yakijiri, mmoja wa wasichana ambao walikuwa kwenye shindano la Wife Material kwa jina “Shilah” kutoka Kitale alijitokeza na kusema kwamba mchekeshaji Eric Omondi hakujamiiana nao na kwamba aliwaheshimu sana.

Lakini video ambazo Eric mwenyewe alizichapisha kwenye Instagram mara kwa mara, zilimwonyesha akibusu wasichana tofauti waliokuwa wakimshindania.

Eric omondi hajajibu madai hayo ya Shakilla.

Categories
Burudani

Eric Omondi achagua wa kuoa

Baada ya shindano la siku kadhaa la wasichana 9 kwa nia ya kujichagulia mke, hatimaye Eric Omondi amepata mmoja.

Kwenye akaunti yake ya Instagram rais huyo wa wachekeshaji barani Africa aliweka picha ya binti anayefahamika kama Carol na kumpongeza kwa kuibuka mshindi wa shindano hilo alilolipa jina la “Wife Material”.

Anamsifia sana mwanadada huyo ambaye ni mwanamuziki katika kundi la Band Beca akisema yuko tayari kuishi naye milele na kupata watoto.

Omondi anashukuru wote ambao waliingia kwenye shindano hilo na wakenya kwa jumla kwa kumsaidia kuchagua mke na anatumai wakenya watahudhuria arusi yao.

Tarehe 23 mwezi Novemba, Eric alitangaza kupitia Instagram kwamba anatafuta mke na akahimiza kila anayetaka kujaza nafasi hiyo atume ombi kupitia video fupi. Kina dada wengi walituma maombi lakini kati yao alichagua tisa ambao walishindania nafasi ya “First lady of comedy in Africa”.

Wasichana hao walipatiwa majaribio kadhaa kama vile kumwandalia Eric chakula, kukaa kwenye mazingira tofauti kama vile mashambani, mitaa ya mabanda na hata ufukweni kati ya majaribio mengine.

Eric na wasichana hao tisa

Wengi walionekana kushabikia hatua yake ya kutafuta mke huku wengine wakimkashifu kwa kuchezea mabinti za watu.

Mwanamuziki wa nyimbo za injili Ringtone Apoko alijitokeza na zawadi ya laki moja kwa yeyote atakayekubali kuacha shindano hilo la wife material akilitaja kuwa usherati.

Duru zinaarifu kwamba mmoja wa wasichana hao kwa jina Mwikali anasemekana kukubali kung’atuka na kwamba alipokea zawadi ya laki moja kutoka kwa Ringtone.

Wakenya walihitajika kupigia kura washindani hao tisa na mshindi ndiye angekuwa mke mtarajiwa wa Eric na ametangaza alasiri ya leo kwamba Carol wa Band Beca ndiye mshindi.

Inasubiriwa kuona ikiwa kweli ndoa itafungwa au ni maigizo tu!

Categories
Burudani

Eric Omondi ahuisha tishio la kutohamisha studio zake

Mchekeshaji Eric Omondi ambaye anajiita Rais wa wachekeshaji barani Afrika ametimiza tishio lake la kutohama eneo ambalo amefungua studio zake huko Lavington.

Hii ni baada ya shirika linalosimamia eneo la jiji la Nairobi NMS kuweka ilani kwenye lango la studio hizo tarehe 30 mwezi Novemba na kuwataka wenyeji kuhama kisa na sababu biashara hiyo imewekwa katika eneo la makazi.

Siku hiyo Eric alikashifu hatua hiyo akiisema kuwa kikwazo kwa vijana ambao wanajaribu kujitafutia riziki. Na jumamosi tarehe 5 mwezi Disemba mwaka huu wa 2020, Eric Omondi alichapisha video ikionyesha watu wakipaka rangi lango la studio zake kufuta ilani ya NMS.

Mchekeshaji huyo aliongeza kusema kwamba wameweka camera za CCTV katika sehemu tofauti za studio hizo ambazo pia ni afisi yake akisema wako tayari kukamata wezi maanake ni wezi tu ambao hutekeleza kazi zao usiku.

Kufikia sasa Eric anasisitiza kwamba hajapokea mawasiliano rasmi kutoka kwa shirika la kusimamia eneo la jiji la Nairobi kuhusu ilani ya kuhama.

Msemaji wa shirika hilo la NMS Bi. Rose Gakuo alijibu madai hayo akisema jambo hilo linashighulikiwa na NMS itatoa taarifa karibuni.

Mchekeshaji huyo ambaye ameanzisha shindano la kina dada kwa jina “wife Material” huku akitafuta mke, anasema studio hizo ni za kuendeleza kazi yake, kazi ya wasanii waliobobea na wale ambao wanaanza sanaa.

Alizipa studio hizo majina ya waigizaji maarufu Mzee Ojwang’ na Mama Kayai.