Categories
Habari

Kenya yajiunga na ulimwengu kuadhimisha siku ya ugonjwa wa kisukari duniani

Kenya Jumamosi inajiunga na mataifa mengine ulimwenguni  kuadhimisha siku Kuu ya maradhi  ya  Kisukari Duniani.

Siku hii inaadhimishwa huku wito ukitolewa wa kuongezwa kwa idadi ya wauguzi wa kukabiliana na ugonjwa wa kisukari.

Vile vile ipo haja kwa wauguzi kupewa  mafunzo zaidi ya kusaidia watu wanaoishi na ugonjwa wa kisukari kuelewa na kudhibiti  hali zao.

Zaidi ya watu milioni 460 kwa sasa wanakadiriwa kuishi na ugonjwa wa kisukari ulimwenguni, idadi inayotarajiwa kuongezeka hadi milioni 578 kufikia 2030.

Mwaka jana pekee, hali hiyo ilichangia  vifo vya watu  milioni 4.2.

Athari za ugonjwa wa kisukari zinaangaziwa zaidi  mwaka huu huku zaidi ya  nusu ya watu wanaopatikana  kuwa na maradhi ya  COVID-19 katika maeneo mengine   kuwa  wale wanaoishi   na hali hiyo.

Na huku maradhi hayo ya kisukari   yakizidi  kuongezeka ulimwenguni, wauguzi zaidi waliopewa mafunzo ya  kudhibiti maradhi hayo  wanahitajika kusaidia watu walioathiriwa kuepuka    makali ya maradhi   hayo.

Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limeonya  kuhusu  upungufu wa wauguzi milioni 5.9 na kuashiria kuwa  wauguzi wanaohitimu watahitaji kuongezeka kwa  asili-mia nane kwa mwaka  ili kumaliza upungufu huo ifikapo mwaka 2030.

Categories
Kimataifa

Ufaransa yaapa kuimarisha juhudi za kupambana na Corona hadi mwaka ujao

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema taifa hilo litaendelea kupambana na janga la korona hadi katikati ya mwaka ujao.

Tangazo hilo limetolewa huku visa vya maambukizi nchini humo vikipita watu milioni moja.

Siku ya Ijumaa Ufaransa ilirekodi zaidi ya visa 40,000 vipya vya maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 na jumla ya vifo 298.

Mataifa mengine ambayo yamerekodi ongezeko la visa vipya vya ugonjwa huo ni Urusi, Poland, Italia na Uswizi.

Shirika la Afya duniani WHO limesema huu ni wakati muhimu kwa mataifa ya Ulaya kuimarisha mbinu za kuzuia msambao wa ugonjwa huo na kuhakikisha kuwa mitandao ya huduma za afya inakabiliana vilivyo na janga hilo.

Idadi ya wastani ya kila siku ya maambukizi ya ugonjwa huo imeongezeka mara dufu katika muda wa siku kumi zilizopita.

Bara la Ulaya sasa limerekodi visa  milioni 7.8 vya ugonjwa huo na karibu  vifo vya watu 247,000.

Kimataifa, jumla ya visa milioni 42 vya mambukizi ya ugonjwa huo vimerekodiwa na vifo milioni 1.1.

Akiongea katika hospitali moja jijini Paris, Rais Macron amesema kwamba kwa mujibu wa ripoti ya wataalamu wa magonjwa nchini humo, ugonjwa huo huenda ukasalia nchini humo hadi katikati ya mwaka ujao.

Ufaransa imeongeza tena muda wa makataa ya kutotoka nje usiku kwa majuma sita.