Adhabu iliyotolewa kwa kituo cha runinga cha Wasafi nchini Tanzania imerekebishwa. Mamlaka ya mawasiliano nchini Tanzania TCRA ilitangaza hayo leo kupitia kwa mkurugenzi mkuu Bwana James Kilaba.
TCRA inasema ilipokea rufaa kutoka kwa usimamizi wa Wasafi Tv inayomilikiwa na msanii Diamond Platnumz kuhusu adhabu hiyo na baada ya kutathmini wameamua kwamba marufuku hiyo ambayo ingekamilika mwezi Juni mwaka huu wa 2021 ikamilike tarehe 28 mwezi Februari mwaka huu wa 2021.
Tangazo la kufungwa kwa kituo hicho lilitolewa na TCRA tarehe tano mwezi Januari mwaka huu na tarehe 21 mwezi huo, usimamizi wa Wasafi Tv ukaandikia TCRA kuomba adhabu yao irekebishwe. Tarehe 28 mwezi Januari, wasimamizi hao wa runinga ya Wasafi walirejea tena TCRA ambapo walipata kusikilizwa.
Bwana Kilaba anasema kwamba Wasafi Tv ilikiri kukiuka kanuni fulani za maadili.
Sababu kuu ya Wasafi Tv kupoteza leseni ya kupeperusha matangazo ni hatua yao ya kupeperusha moja kwa moja tumbuizo la mwanamuziki Gigy Money ambaye anasemekana kuvaa mavazi ambayo yalionyesha umbo lake visivyo.
Msanii huyo Gigy money pia aliadhibiwa na BASATA au ukipenda “Baraza la Sanaa la Taifa” ambapo alifungiwa asiwahi kufanya kazi yoyote ya sanaa kwa muda wa miezi sita.
Gigy siku hiyo kwenye tamasha la Wasafi Media, aliingia jukwaani akiwa amevaa dera kisha baadaye akalivua na kubakia na vazi la kushikilia mwili ambalo rangi yake ilikaribia kufanana na rangi ya ngozi yake ungedhania yuko uchi.
Usimamizi wa Wasafi haujasema lolote kuhusu kupunguziwa adhabu.