Categories
Burudani

Coy Mzungu azawadiwa gari

Mchekeshaji wa nchi ya Tanzania Coy Mzungu alizawadiwa gari na usimamizi wa Wasafi Media kampuni inayomilikiwa na Diamond Platnumz na ambayo inadhamini tamasha la Cheka Tu ambalo alianzisha Coy.

Diamond Platnumz mwenyewe ndiye aliwasilisha gari hilo kwa Coy Mzungu jambo ambalo hakutarajia wakati wa awamu ya Mzizima ya tamasha hilo la Cheka Tu.

Coy alikuwa jukwaani na mchekeshaji wa Kenya Eunice Mamito na Diamond akajiunga nao na kutangaza kwamba alikuwa amepitia tu kushukuru wote waliohudhuria tamasha hilo na kumpokeza gari Coy Mzungu.

Kwa mara ya kwanza, ukumbi wa mikutano wa jumba la kibiashara la Mlimani City Jijini Dar es Salaam ulijaa tangu kuanzishwa kwa tamasha hilo la vichekesho.

Baada ya kutangaza zawadi hiyo, Diamond alimwelekeza Coy na wengine nje ambapo gari lenyewe lilikuwa limeegeshwa. Kwa furaha nyingi alipokea zawadi yake Coy Mzungu na hata kusimama juu ya gari lenyewe huku akishukuru usimamizi wa Wasafi.

Wakati wa kuondoka nchini Tanzania Eunice Mamito alimtania Diamond Platnumz akisema kwamba anastahili kukumbuka kina dada anapogawa magari.

Mamito ni mmoja wa wachekeshaji wa Kenya ambao wamepata nafasi ya kutumbuiza kwenye tamasha hilo la vichekesho nchini Tanzania. Wengine ni pamoja na Sammie Kioko, Eric Omondi na Mc Jessy.

Categories
Burudani

Msanii Q Chief atoa ilani kwa Wasafi Media

Msanii wa Bongo Fleva Q Chief ameupa usimamizi wa Wasafi Media na Kampuni ya Tigo muda hadi mwisho wa siku hii leo ili apate maelezo kamili kuhusu sababu ya kuweka jina lake na picha yake kwenye bango la tamasha lao bila idhini yake.

Kupitia Instagram, Q Chief alisema kwamba hakuna yeyote aliwasiliana naye rasmi kutoka kwa kampuni hizo ili kumshirikisha kwenye tamasha hilo la Jumamosi tarehe 30 mwezi Januari mwaka 2021 almaarufu kama “Wasafi Tumewasha na Tigo”.

Anaendelea kuelezea kwamba mashabiki wake wengi wamekuwa wakimpigia simu kujua ni kwa nini hakuonekana kwenye tamasha hilo ilhali walikuwa wakimtarajia jambo ambalo anasema linaathiri kazi yake ya muziki.

Q Chief anasema amekuwa akijaribu kuwasiliana na usimamizi wa Wasafi Media bila mafanikio huku akiambiwa kwamba wahusika bado wana uchovu wa tamasha la jumamosi.

Hata hivyo wengi wa mashabiki wake kwenye Instagram, wanaonelea kwamba hakustahili kuweka ilani hiyo kwenye mitandao ya kijamii na kwa kufanya vile wanahisi anajitafutia umaarufu.

Hakuna jibu lolote limetolewa na Wasafi Media inayomilikiwa na Diamond Platnumz wala kampuni ya mawasiliano ya rununu ya Tigo kuhusu lalama za Q Chief.

Categories
Burudani

Rayvanny azindua albamu yake mpya

Leo tarehe mosi mwezi Februari mwaka 2021, Raymond Shaban Mwakyusa mwanamuziki wa Tanzania maarufu kama Rayvanny amezindua albamu yake kwa jina “Sound From Africa”.

Mwimbaji huyo anayefanya kazi ya muziki chini ya kampuni ya WCB, ameweka albamu hiyo kwenye majukwaa mbali mbali ya mitandaoni.

Rayvanny ameshirikisha wanamuziki wengine wengi kwenye albamu hiyo yenye nyimbo 23 ambazo ni, Sound from Africa, Tetema, Senorita, Kelebe, chuchumaa remix, tingisha, Number One, Juju, Koroga, Rotate, Bebe, Baby, Bailando, Twerk, Zuena, Lala, Mama, Kiuno, Marry me, Zamani, Waongo, Juu na Woza.

Wanamuziki walioshirikishwa humo ni kama vile Diamond Platnumz, Jah Prayzah, GIMS, Innos B, Frenna, Aminux, Nasty C na Saida Kroli kati ya wengine wengi.

Habari kuhusu kuzinduliwa kwa albamu hii, zimewadia muda mfupi baada ya taarifa kuhusu ajali aliyopata Rayvanny akiwa jukwaani kutumbuiza ambayo ilitamatisha ghafla tamasha la “Wasafi Tumewasha na Tigo”.

Kulingana na video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, Rayvanny anaonekana kama ambaye aliteleza na kutanguliza kicha anapoanguka.

Vanny Boy aliweza kuinuka baada ya kuanguka na alisaidiwa kuondoka jukwaani na mtumbuizaji mwenza. Mkubwa wa Wasafi Media Diamond Platinumz alisitisha sherehe ya baadaye iliyokuwa imepangwa huku akihimiza mashabiki kutumia muda huo kushukuru Mungu na kumwombea Rayvanny.

Categories
Burudani

Ninamheshimu Nandy – Diamond Platnumz

Jana wakati akihojiwa kwenye Wasafi Fm, Diamond aliulizwa kuhusu ulivyo uhusiano kati yake na msanii wa kike nchini Tanzania nandy.

Simba au ukipenda Chibu Dangote (anavyojiita Diamond) ,alisema kwamba anamheshimu mwanadada huyo na ndio hivyo. Alielezea jinsi walikutana Dubai mwaka 2018 wakapigwa picha pamoja na hata akampa Nandy mkufu wenye nembo ya “WCB” akavaa na kupigwa picha nao.

WCB ni kampuni ya kusimamia wanamuziki ambayo inamilikiwa na Diamond Platnumz. Ilitokea kwamba wawili hao, Nandy na Diamond hawafuatani kwenye mitandao ya kijamii lakini Chibu alisema hakuna tatizo lolote kati yao.

Diamond alimsifia Nandy kama mwanamuziki wa kike wa Tanzania ambaye anapeperusha bendera ya Tanzania huko nje.

Alisema pia kwamba huenda mahusiano ya kimapenzi ya Nandy na mshindani wake kwenye biashara ndiyo yaliweka umbali kati yao.

Nandy alisemekana kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na marehemu Ruge Mutabaha mmoja wa wamiliki wa Clouds Media, kamouni ya uanahabari ambayo ni mpinzani mkuu wa Wasafi Media nchini Tanzania.

Nandy kwa sasa anaendelea na kazi ya kuunda video ya wimbo wake kwa jina “Leo” na msanii wa Congo Koffi Olomide baada ya Koffi kufanya kazi na Diamond Platnumz mwaka jana.

Wakati akihojiwa mwaka jana akiwa na Diamond Platnumz, Koffi alisema kazi na Diamond ilikuwa imembana sana hata hangeweza kumpa nafasi Nandy wakati huo ili wakamilishe kazi yao.

Categories
Burudani

Gigy Money amlaumu Beyonce

Baada ya mwanamuziki wa Tanzania kwa jina Gigy Money kupata adhabu kali kutoka kwa Baraza la Sanaa nchini Tanzania – BASATA mwanadada huyo sasa anajuta akimlaumu mwanamuziki wa Marekani Beyonce.

Kwenye akaunti yake ya Instagram akiweka video fupi ya Beyonce na mume wake Jay Z wakitumbuiza jukwaani huku Beyonce akiwa amevalia vazi sawa na lililomtia mashakani.

Ishara kwamba huwa anajifunza kwa Beyonce. Kwenye video hiyo Gigy ameandika, “Role Model umeniponza @Beyonce”. Gigy amefuta kila kitu kwenye hiyo akaunti yake ya Instagram isipokuwa video hiyo ya Beyonce na Jay Z.

Gigy amesimamishwa asijihusishe na tamasha zozote kwa muda wa miezi zita na amepigwa faini ya shilingi milioni moja za Tanzania ambazo ni sawa na elfu 47, 184 za Kenya.

Kilichomletea matatizo Gigy Money ni vazi lake akitumbuiza kwenye tamasha la mwaka mpya la Wasafi Media ambalo lilikuwa linapeperushwa moja kwa moja kenye runinga ya Wasafi.

Gigy aliingia jukwaani akiwa amevalia dera na baadaye akalivua na kubakia na vazi ambalo linanata mwili wote na kuonyesha maungo yake.

Kitendo hiki kilisababishia kituo cha Runinga cha Wasafi matatizo kwani pia kimesimamishwa kisirushe matangazo kwa miezi sita na mamlaka ya mawasiliano nchini Tanzania.

Wasafi Media kampuni kuu ya kituo cha redio cha Wasafi fm, kituo cha runinga cha Wasafi Tv na kampuni ya muziki ya Wasafi Classic Baby – WCB inamilikiwa na Diamond Platnumz.

Categories
Burudani

Niko sawa! Zuchu awambia mashabiki

Malkia wa kampuni ya wanamuziki nchini Tanzania Wasafi Classic Baby WCB Zuchu amewaarifu mashabiki wake kwamba yuko salama salmini. Hii ni baada ya msanii huyo kuanguka akiendelea kutumbuiza huko Dodoma jana usiku.

Alikuwa kwenye tamasha la Wasafi Media na alianguka alipojaribu kukwea ngazi moja ambayo ilikuwa nguzo ya jukwaa la muda ambalo walikuwa wakitumia.

Hata hivyo aliinuka kwa haraka na kupanda kwenye chuma hizo na kuendelea kucheza huku akishangiliwa na mashabiki.

Lakini wafuasi wake wamekuwa wakimkejeli kwenye mitandao ya kijamii huku wengine wakihofu kuhusu usalama wake baada ya ajali hiyo.

Kwa sababu hiyo, Zuchu akapachika picha kwenye akaunti yake ya Instagram akiwa amevalia mavazi alokuwa amevaa wakati akitumbuiza na kushikilia bunda la pesa kana kwamba ni rununu na kuandika maneno haya; “Hello Ambulensi, niko salama msijali.”

Mtumiaji mmoja wa Instagram kwa jina ‘Carrymasttory’ aliweka picha ya Zuchu na kuandika, “Nipo hospitali ya mkoa wa Dodoma hapa hadi muda huu hajaletwa akiwa anaumwa hata maumivu tuu, kumbe kamekomaa eeehhh?”

Carrymasttory huwa anachambua watu maarufu nchini Tanzania pamoja na matukio mbali mbali nchini humo.

Zuchu ambaye hajamaliza hata mwaka mmoja katika kundi la WCB amepata umaarufu mkubwa ndani na nje ya Tanzania na kufikia sasa ameteuliwa kuwania na kushinda tuzo kadhaa ndani na nje ya Tanzania.

Categories
Burudani

Harmonize amtambua Diamond Platnumz

Mwanamuziki wa Tanzania kwa jina Harmonize amechagua kumtambua mwanamuziki mwenza Diamond Platnumz katika kheri njema za mwaka mpya.

Wanamuziki hao wawili wa Tanzania wanasemekana kutokuwa na uhusiano mzuri hasa baada ya Harmonize kugura kampuni ya muziki kwa jina Wasafi Classic Baby – WCB inayomilikiwa na Diamond.

Mmiliki huyo wa Konde Music amewashangaza wengi baada ya kuamua kumtambua rafiki yake wa zamani ambaye pia alikuwa mkubwa wake.

Aliweka picha ya Diamond Platnumz kwenye akaunti yake ya Instagram na kuandika, “Nazungumza kutoka moyoni naakupenda kakangu. Ni mwaka mpya 2021. Asante kwa kubadilisha maisha yangu. wewe pekee uliona dhahabu kwenye mchanga na giza jingi sana!!! Leo hii Afrika nzima na hasa Afrika Mashariki wanajivunia uwepo wangu. Upendo huu ni wa milele ndugu yangu. Kila nilichokifanya nilikuwa na nia ya kukufurahisha usinielewe vibaya. Keti peke yako bila yeyote pembeni usome ujumbe huu utaelewa ninachomaanisha. Wewe ni shujaa. wakati mwema. Mimi Konde Boy na wanamuziki wote wa Konde Gang tunakupenda. Mwaka mpya mwema Chibu Dangote Diamond Platnumz kaka mkubwa.”

Haya yanajiri baada ya Harmonize kujaribu kuonyesha kwamba kuna uhasimu kati yake na Diamond kupitia wimbo alioutoa mwisho wa mwaka jana kwa jina “Ushamba”.

Alionekana kumkejeli Diamond kwenye wimbo huo na alipohojiwa, Diamond alisema ushindani ni muhimu katika sekta ya muziki nchini Tanzania ili isonge mbele.

Harmonize ameandika maneno hayo usiku wa kuamkia leo na anaonekana kana kwamba bado yuko nchini Ghana ambako alikuwa amekwenda kwa likizo.

Diamond Platnumz hajajibu hatua hii ya mkono wa maridhiano kutoka kwa Harmonize, anaonekana kuzamia kazi ambapo jana yeye na kikosi kizima cha Wasafi media walikuwa katika eneo la Dodoma kwa ajili ya ile ziara yao kwa jina “Tumewasha na Tigo”.

Categories
Burudani

Shishi Baby aomba ukuu wa Wilaya

Mwanamuziki na mjasiriamali wa nchi ya Tanzania Zena Yusuf Mohamed maarufu kama Shilole au ukipenda Shishi Baby ametoa ombi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli.

Wakenya wanamfahamu dada huyo kutokana na video iliyosambazwa awali kwenye mitandao ya kijamii ambapo alishindwa kutamka neno, “Subscribe”.

Mwanadada huyo ambaye anamiliki mkahawa kwa jina Shishi Food anasema anatamani sana kuwa mbunge lakini kwa sasa anaomba Rais ampe ukuu wa wilaya.

Amewahi kuwa mwenyeji wa watu mashuhuri kwenye mkahawa huo wake, wa hivi punde zaidi akiwa mwanamuziki tajika wa Congo, Koffi Olomide.

Shishi anakubali kwamba hana kisomo, aliachia darasa la saba, lakini ana kipaji cha uongozi na ikiwa Rais ataona vyema ampatie kazi hiyo ya kusimamia wilaya.

Mwanamuziki huyo alitaja Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Bi. Jokate Urban Mwegelo wa miaka 33 ambaye awali alikuwa mtangazaji na mfanyibiashara akisema ikiwa atapatiwa kazi ataifanya kama anavyoifanya Jokate kwa kujitolea.

Siku za hivi karibuni Shilole amekuwa akijitahidi sana kujitafutia yeye na binti zake pale ambapo amekuwa akitangazia kampuni kadhaa biashara zao na inaaminika kampuni hizo zinamlipa vizuri.

Amekuwa pia akihusishwa kwenye tamasha linaloendeshwa na wasafi media ya Diamond Platnumz almaarufu “Tumewasha na Tigo”.

Alijihusisha pia kikamilifu na kampeni za chama cha CCM kabla ya uchaguzi mkuu na sasa inasubiriwa kuona ikiwa Rais Magufuli ataridhia ombi lake.

Categories
Burudani

Muigizaji Sammy Kioko nchini Tanzania

Ijumaa tarehe 27 mwezi Novemba mwaka 2020 kuliandaliwa tamasha la vichekesho kwa jina “Cheka Tu” huko jijini Daresalaam nchini Tanzania na mchekeshaji wa Kenya Sam Kioko alikuwa mmoja wa waliotumbuiza siku hiyo.

Onyesho hilo lilikuwa limedhaminiwa na Wasafi Media inayomilikiwa na Diamond Platnumz na Kioko alipata nafasi ya kukutana na Diamond kabla ya onyesho.

Waliohudhuria ni pamoja na dadake Diamond ambaye pia ni mwanamuziki kwa jina Queen Darleen na Babu Tale, meneja wa muda mrefu wa mwanamuziki Diamond Platnumz ambaye sasa ni mbunge wa eneo la Morogoro Kusini.

Mume wake Queen Darleen Isihaka Mtoro anayemiliki kampuni ya kuandaa tamasha kwa jina “Is- Bar entertainment”alimsifia sana mchekeshaji wa Kenya Sammy Kioko akisema aliwavunja mbavu watanzania.

Sio mara ya kwanza kwa Sammy kuichekesha Tanzania, aliwahi kufanya hivyo tena yapata mwaka mmoja uliopita kwa mwaliko wa mwanahabari wa michezo nchini Tanzania Bi. Meena Ally.

Sammy Kioko alijulikana kama mchekeshaji nchini Kenya baada ya kuibuka mshindi kwenye shindano la uchekeshaji kwa jina “Ultimate Comic” awamu ya kwanza mwaka 2018. Alijishindia gari, mkataba wa kuonekana kwenye runinga na shilingi milioni moja.

Tangu wakati huo amekuwa akiinuka katika fani hiyo na sasa amekwenda kwenye rubaa za kimataifa. Wasichojua wengi ni kwamba Sammy Kioko ni mwalimu. Taaluma yake ya msingi ni ualimu lakini anapenda sana uchekeshaji.

Categories
Burudani

Tangazo la Diamond Platnumz mkurugenzi mkuu wa Wasafi Media

Inatokea kwamba tangazo ambalo lilikuwa linasubiriwa kwa hamu na ghamu kutoka kwa Diamond Platnumz sio kuhusu kuzinduliwa kwa collabo yake na Koffi Olomide.

Tangazo lenyewe ni kuhusiana na ushirikiano wa kibiashara kati ya Wasafi Media, kampuni ya mawasiliano ya rununu nchini Tanzania Tigo na kampuni ya vinywaji ya Pepsi.

Kampuni hizo tatu zitakuwa na ziara katika sehemu mbali mbali nchini Tanzania kwa lengo la kuongeza mauzo.

Akizungumza kwenye makao makuu ya Wasafi Media huko Mbezi, mkurugenzi mkuu wa Wasafi Media Abdul Nasib au Diamond Platnumz alisema kwamba kampuni hiyo ya utangazaji inashirikiana na Tigo na Pepsi kutembelea wateja wake katika mikoa ambapo vituo vya Wasafi vimewashwa na ambapo vitawashwa.

“Linaitwa Wasafi tumewasha na Tigo na unajiburidisha na Pepsi mpaka basi!” maneno yake Diamond hayo.

Kulingana naye hawajapata nafasi ya kushukuru wasikilizaji na watazamaji wao kwa kupendelea Wasafi Media na hii ni nafasi nzuri na njia bora ya kumaliza mwaka.

Msafara wenyewe utaanza tarehe 28 mwezi huu wa Novemba mwaka 2020 katika eneo la Kahama na utahusisha wasanii wa kampuni ya Wasafi na wengine wa nje na orodha kamili itatolewa baadaye.

Wasimamizi wa mauzo kutoka kampuni za Tigo na Pepsi pia walizungumza kwenye kikao hicho na wanahabari ambapo waliahidi wateja wao mengi mazuri kwenye msafara huo.