Wazazi wenye watoto walemavu katika Kaunti ya Wajir na maeneo ya karibu wamehimizwa kuwapa watoto wote fursa sawa licha ya hali zao.
Haya yanajiri wakati baadhi ya wazazi wa watoto walio na ugonjwa wa kupooza kwa ubongo kuwaficha wakisema hali hiyo ni laana, hali ambayo inaweza kusababisha vifo vya watoto kama hao.
Kituo cha kuwatunza watoto hao cha Misheni ya Kanisa Katoliki ya Wajir ambacho hupokea na kushughulikia matibabu ya watoto hao kimesifiwa kwa juhudi zake za kushughulikia watoto wenye tatizo hilo ambalo husababishwa na jeraha kwa ubongo au matatizo ya ujauzito.
Akiongea na wanahabari wa kituo cha Televisheni Cha KBC Channel 1, Mtawa Jenipher Mosima ambaye anasimamia kituo hicho alisema watoto wenye ulemavu sio laana na wana haki ya kupata mahitaji yote ya kimsingi kama watoto wengine.
Mosima alisema kutokana na janga la COVID-19, watoto hao wamo kwenye hatari ya kuambukizwa ikiwa wazazi wao hawazingatii kanuni za kiafya.
Aliwahimiza wazazi kutunza watoto wa aina hiyo vizuri na kutokata tamaa kuwatunza.