Categories
Burudani

Rayvanny kuzindua albamu

Msanii wa Bongo Fleva Raymond Shaban Mwakyusa almaarufu Rayvanny ama ukipenda vanny Boy ametangaza kwamba ataachilia albamu yake ya kwanza hivi karibuni.

Vanny ambaye anafanya kazi ya muziki chini ya kampuni ya Diamond Platnumz Wasafi Classic Baby – WCB alianza muziki mwaka 2011 akiwa shule ya upili lakini hajawahi kuzindua albamu.

Alijiunga na WCB rasmi mwaka 2015 na mwaka 2016 akaachilia kibao “Kwetu” ambacho kilivuma sana Afrika mashariki.

Mwezi wa pili mwaka 2020 Rayvanny alizindua EP yake kwa jina “Flowers” ambayo ilifanya vyema kwenye mitandao ya kijamii.

EP au ukipenda ‘Extended Play’ ni mkusanyiko wa nyimbo ambazo hazitoshi kuitwa albamu. Mwanamuziki huyo ameteuliwa kuwania na kushinda tuzo kadhaa.

Ni kati ya wanamuziki wanaofanya vizuri katika WCB na mkubwa wake Diamond aliwahi kufichua kwamba alikuwa akijenga studio zake za muziki isijulikane kama atagura WCB alivyofanya Harmonize.

Diamond alisifia sana studio hizo akisema kwamba zikikamilika zitakuwa bora zaidi Afrika mashariki.

Rayvanny amejulikanisha ujio wa albamu hiyo kwa jina “Sound From Africa” kupitia picha na video ambazo amekuwa akiweka kwenye mtandao wa Instagram lakini hajatangaza tarehe rasmi ya kuiachilia.

Categories
Burudani

Rayvanny Kuondoka Wasafi?

Fikra kuhusu uwezekano wa mwanamuziki kwa jina la usanii “Rayvanny” au ukipenda “Vanny Boy” kuondoka kwenye kampuni ya Wasafi inayomilikiwa na Diamond Platinumz, zinatokana na usemi wa Diamond mwenyewe.

Wakati wa mahojiano yake kwenye kipindi cha ‘The Switch’, kwenye Wasafi FM siku ya jumanne, Diamond alifichua kwamba hivi karibuni Rayvanny anazindua kampuni yake ya kusimamia wanamuziki.

Diamond alisema ameona Studio ambazo Rayvanny anaandaa na kulingana naye zikizinduliwa zitakuwa bora kuliko zote nchini Tanzania.

Alipoulizwa kuhusu uhuru wa wanamuziki walio chini ya Wasafi kuondoka na kujiendeleza, Dianond alisema wana uhuru wa kufanya vile.

Mwimbaji huyo wa kutokea eneo la Tandale alisema kila mara huwa anawahimiza wanamuziki walio chini yake waishi vizuri na watu na watafute kujiendeleza kifedha.

“Iwe mfano ni mimi, nimefika hapa nilipo halafu wakati mmoja unikute kule Tandale nakuomba shilingi mia jamani! ikiwa ni mimi sitakupa!” Alisema mwanamuziki huyo.

Maneno yake yanaonekana kuwa kinaya kwani hadi sasa, kampuni ya Wasafi haijamwachilia kikamilifu mwanamuziki Harmonize ambaye aligura na kuanzisha kampuni yake kwa jina “Konde Music”.

Harmonize alifichua kwamba mkataba wake na WCB unamhitaji alipe milioni mia tano pesa za Tanzania kabla apate hakimiliki za nyimbo zake na kuandikisha hakimiliki yake mwenyewe.

Kulingana naye amelazimika kuuza mali nyingi kulipa deni hilo lakini bado hajalimaliza.

Inasubiriwa kuona ikiwa Rayvanny atagura Wasafi au atasalia tu akiendeleza biashara yake kando au atagura na ikiwa atagura safari yake itakuwa rahisi au ngumu kama ya Harmonize?