Categories
Kimataifa

Maafisa wa usalama nchini Uganda washtumiwa kwa kuwajeruhi wanahabari waliokuwa wakiripoti kumhusu Bobi Wine

Muungano wa Wahariri nchini Uganda umeshtumu vikali vikosi vya usalama nchini humo (UPDF) baada ya kuwajeruhi wanahabari kadhaa waliokuwa wakiripoti habari kumhusu mwanasiasa Robert Kyagulanyi.

Wanahabari hao walikuwa wameandamana na mwanasiasa huyo almaarufu Bobi Wine akiwasilisha malalamshi kwa afisi za Umoja wa Mataifa kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu nchini humo.

Mashahidi wanasema kuwa wanajeshi waliwasili kwa malori nje ya afisi za kutetea haki za binadamu za Umoja wa Mataifa (UNHRC) katika mji mkuu wa taifa hilo Kampala na kuanza kuwapiga wanahabari.

Kulingana na taarifa ya muungano wa wahariri nchini humo, angalau wanahabari 10 wa mashirika tofauti ya habari walijeruhiwa kabla kupelekwa hospitalini kwa matibabu.

Mwanahabari mmoja aliweka katika mtandao wa Twitter, picha za yaliyokuwa yakijiri katika eneo hilo huku akionyesha mmoja wa wanahabari akitokwa na damu kichwani.

Kituo kimoja cha kibinafsi cha runinga kilionyesha picha za wanahabari wakitoroka ili kuepuka kucharazwa.

Akijibu shutuma hizo, Msemaji wa vikosi hivyo vya usalama Brigadia Generali Flavia Byekwaso amesema kundi lililoandamana na Bobi Wine walijeruhi afisa mmoja wa usalama ndiposa ikabidi wafurushwe kwa nguvu.

Kuna wasi wasi nchini Uganda kuhusu hatima ya wafuasi wa upinzani ambao wamesemekana kutoweka.Waliokamatwa wamesemekana kuteswa.

Rais Yoweri Museveni hivi maajuzi alisema kuwa watu 300 wamezuiliwa kwa kuzua vurugu na kuhusika na visa vingine vya uhalifu.