Categories
Kimataifa

Angela Merkel ashinikiza kufungwa kwa shughuli nchini Ujerumani kudhibiti Covid-19

Kansella Angela Merkel wa Ujerumani ameonya kuhusu kipindi kigumu na kirefu cha majira ya baridi,huku akitetea  kurejelewa tena kwa sheria za kufunga shughuli nchini humo kuzuia kusambaa kwa ugonjwa wa Covid-19.

Merkel alionywa  na wabunge wa mrengo wa kulia alipotangaza kurejelewa kwa sheria hizo katika bunge.

Maafisa wa afya wamesema kuwa takriban watu 89 walifariki  nchini humo siku ya alhamisi kutokana na ugonjwa huo,huku wengine 16,774 wakiambukizwa virusi vya ugonjwa huo.

Hata hivyo sheria hizo si kali kuliko zile zilizotangazwa na taifa la Ufaransa ambalo lilifunga baa,migahawa na majumba ya mazoezi ya misuli na ya wasanii.

Ongezeko la maambukizi ya ugonjwa huo barani ulaya limesababisha mataifa husika kutangaza sheria kali zaidi.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alitangaza sheria mpya za kukabiliana na janga hilo baada ya vifo kutokana na ugonjwa huo kuongezeka kwa kiwango kikubwa tangu mwezi Aprili.

Siku ya Alhamisi  taifa hilo lilirekodi visa 47,637 vipya vya ugonjwa huo,ikilinganishwa na visa 36,437 vya siku iliotangulia na vifo vya watu  235 siku ya jumatano.

 

 

Categories
Kimataifa

Bara la Ulaya laongeza juhudi za kukabiliana na maambukizi ya COVID-19

Jamhuri ya Czech inaweka kizuizi cha kadiri cha wiki tatu, huku ikifunga shule, baa na vilabu wakati Ulaya ikijitahidi kudhibiti kuongezeka kwa visa vya maradhi ya COVID-19.

Shule, baa na vilabu vitasalia kufungwa hadi tarehe tatu mwezi ujao huku migahawa ikiruhusiwa tu kuwasilisha chakula kwa wateja au kukiuza kwa kuwapakia, hadi saa mbili usiku kila siku.

Mabweni ya vyuo vikuu pia yanafungwa kwa muda, na masomo yataendeshwa wanafunzi wakiwa nyumbani kupitia mtandao.

Shule za chekechea zitasalia kufungwa na mikakati maalum kuwekewa watoto wa wafanyakazi wa kutoa huduma muhimu.

Kumerekodiwa vifo 1,051 vya kutokana na maradhi ya COVID-19 katika Jamhuri ya  Czech tangu tarehe mosi mwezi Machi, wakati taifa hilo lilipothibitisha kisa cha kwanza cha maradhi hayo.

Uholanzi pia iliamuru kufungwa kwa migahawa na unywaji wa pombe kwenye maeneo ya umma umepigwa marufuku na sharti barakoa zivaliwe katika maeneo hayo.

Naye Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema kwenye hotuba ya televisheni kuwa atatangaza vizuizi zaidi.

Chancella wa Ujerumani Angela Merkel amesikitishwa na  hali inayozidi kuzorota Barani Ulaya.

Categories
Kimataifa

Pompeo: Afisa wa ngazi ya juu Urusi aliamuru Navalny apewe sumu

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Mike Pompeo amesema kuwa inawezekana kitendo cha kumpa sumu kiongozi wa upinzani nchini Urusi, Alexei Navalny kiliamuliwa na afisa wa ngazi ya juu wa serikali ya Urusi.

Pompeo amejizuia kutoa maelezo zaidi kuhusu hoja hiyo, akiongeza tu kuwa watu wote duniani wanatambua kilichotokea.

Akizungumza katika mahojiano na chombo kimoja cha habari cha Marekani, waziri Pompeo amesema kuwa serikali ya Marekani itatafakari cha kufanya kujibu kisa hicho cha kumpa sumu Navalny, kwa lengo la kuhakikisha kuwa vitendo kama hivyo havitokei tena. Wakati huo huo, Ujerumani imekabidhi ushahidi wake kwa shirika la kimataifa la kudhibiti matumizi ya silaha za kemikali-OPCW, kuthibitisha kuwa Navalny alipewa sumu aina ya Novichok.

Naye Waziri Mkuu wa Italia, Giussepe Conte amenukuliwa akisema amearifiwa na rais wa Urusi Vladimir Putin, kuwa ameunda tume ya kuchunguza kisa cha Navalny kupewa sumu.

Source: DW