Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga amesema kuwa ripoti ya BBI inalenga kuwaweka wanaume na wanawake walio kwenye ulingo wa siasa katika kiwango sawa.
Raila alisema kuwa kupitia kwa ripoti hiyo, taifa hili litaweza kuafikia sheria ya thuluthi mbili katika maswala ya jinsia.
Raila ambaye alikuwa akiwahutubia viongozi wa wanawake wa mashinani katika kaunti ya Nairobi, alitoa wito kwao kupigia debe ripoti hiyo kwa vile watanufaika pakubwa iwapo itaungwa mkono na kuidhinishwa na wakenya.
Kwa mara nyingine alishtumu kampeini tata zinazolenga kuhujumu mchakato huo huku akitoa wito kwa viongozi wa kike kuiunga mkono.
Alikashifu matamshi yanayohusishwa na upande unaomuunga mkono naibu wa Rais William Ruto ambao unadai kuwa mchakato wa BBI si swala muhimu kwa sasa.
Kwa mujibu wa Raila, naibu wa rais na washirika wake hawaambii wakenya ukweli.
Alisisitiza kuwa ripoti ya BBI ndio zawadi bora ambayo yeye na rais Uhuru Kenyatta wanaweza kukabidhi kwa kizazi kijacho.