Categories
Michezo

Uganda Hippos waing’ata Burkina Faso na kutinga nusu fainali AFCON U 20

Uganda Hippos waliandikisha historia Alhamisi usiku walipoibwaga Burkina Faso penati 5-4 na kufuzu kwa nusu fainali ya kombe la bara Afrika kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 mjini Nouakchott Mauritania.

Burkina Faso maarufu kama Young Stallions walianza vyema mechi kwa mashambulizi mengi lakini kipa wa Uganda Komakach alikuwa mwiba na kupangua matobwe yote.
Ugand pia walishuhudia mikwaju yao kupitia kwa Steven Sserwadda ,Ivan Bogere na Isma Mugulusi ikipanguliwa.

Mechi ilimalizikia kwa sare tasa baada ya dakika 120 na kuamuliwa kupitia matuta ya penati Uganda wakiunganisha zote 5 huku kipa wa Hippos Komakach akipangua

penati ya kwanza iliyochongwa na Naser Djiga Yacouba .

Uganda wanaoshiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza watacheza nusu fainali na mshindi kati ya Tunisia na Moroko watakaomenyana kwenye robo fainali ya Ijumaa.

Ghana wakimenyana na Cameroon

Ghana waliibandua Cameroon pia kupitia penati 5-3 kufuatia sare tasa dakika 120 katika kwota fainali ya kwanza.

Ghana ukipenda Black Satelites watamenyana na mshindi wa robo fainali ya Ijumaa baina ya Afrika ya kati na Gambia katika hatua ya nusu fainali.

Categories
Kimataifa

Uganda yakana madai kwamba viongozi wakuu serikalini wamechanjwa kisiri dhidi ya COVID-19

Waziri wa Afya nchini Uganda Jane Aceng amekanusha taarifa kwamba viongozi wa juu wa serikali wamepata chanjo dhidi ya COVID-19 hata kabla ya taifa hilo kupokea rasmi chanjo hizo.

Kwenye ujumbe wa Twitter, Aceng amesema rais na wandani wake wa karibu hawajapokea chanjo hizo jinsi ilivyodaiwa.

Uganda inatarajiwa kupokea dozi laki moja za chanjo kutoka kampuni ya India, AstraZeneca na nyingine 300,000 kutoka kampuni ya Sinopharm ya Uchina.

Hata hivyo, haijathibitishwa ikiwa chanjo hizo zimewasili katika taifa hilo ambalo kufikia sasa limethibitisha visa 40,221 vya COVID-19.

Kumekuwa na mgogoro katika usambazaji wa chanjo hizo duniani, huku Rais wa Rwanda Paul Kagame akikerwa na unafiki na hujuma kwenye usambazaji wa chanjo hizo hasa kwa mataifa yenye kipato cha chini.

Rais Kagame alisema hayo kwenye ujumbe wake baada ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tedros Adhanom Ghebreyesus kusema kuwa makubaliano kati ya nchi tajiri na watengenezaji wa chanjo hizo yametatiza ununuzi na usambazaji wa chanjo hizo kupitia mpango wa Covax.

Mpango wa Covax unanuia kuhakikisha usawa katika usambazaji wa chanjo dhidi ya COVID-19 miongoni mwa mataifa yote duniani.

Mnamo mwezi Disemba, vuguvugu la People’s Vaccine Alliance lilionya kwamba asilimia 70 ya mataifa ya kipato cha chini yataweza kutoa chanjo kwa asilimia kumi pekee ya raia wake.

Lilitoa wito kwa kampuni zinazotengeneza chanjo hizo kutoa habari kuhusu teknolojia inayotumika ili kurahisisha utengenezaji na kuwawezesha watu wengi zaidi kupata chanjo hizo.

Categories
Michezo

Mechi za Uganda za kufuzu kwa mashindano ya FIBA Afrobasket zaahirishwa kutokana na Covid 19

Shirikisho la mpira wa kikapu ulimwenguni FIBA limelazimika kuahirisha mechi za Uganda za kufuzu kwa mashindano ya kombe la Afrika FIBA Afrobasket mjini Monastir Tunisia  baada ya wachezaji watano wa Uganda kupatikana na virusi vya Covid 19 .

Yamkini wachezaji hao hawakupatikana na virusi hivyo baada ya vipimo vya kwanza kabla ya safari ,lakini wakapatikana na virusi  kufuatia vipimo walivyofanyiwa walipowasili mjini Monastir  Tunisia.

Kufuatia hatua hiyo mechi za Uganda dhidi ya Misri iliyokuwa ichezwe  Februari 18,ile ya Uganda dhidi Moroko Februari 20 na Uganda dhidi ya Cape Verde Februari 21 zimeahirishwa na zitapangwa upya.

Michuano ya makundi  kufuzu kwa mashindano ya FIBA Afrobasket yanaandaliwa katika miji ya Monastir Tunisia na Younde Camroon  huku mataifa 16 bora yakijikatia tiketi kwa mashindano hayo yatakayoandaliwa mwezi Agosti nchini  Rwanda.

Categories
Kimataifa

Maafisa wa usalama nchini Uganda washtumiwa kwa kuwajeruhi wanahabari waliokuwa wakiripoti kumhusu Bobi Wine

Muungano wa Wahariri nchini Uganda umeshtumu vikali vikosi vya usalama nchini humo (UPDF) baada ya kuwajeruhi wanahabari kadhaa waliokuwa wakiripoti habari kumhusu mwanasiasa Robert Kyagulanyi.

Wanahabari hao walikuwa wameandamana na mwanasiasa huyo almaarufu Bobi Wine akiwasilisha malalamshi kwa afisi za Umoja wa Mataifa kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu nchini humo.

Mashahidi wanasema kuwa wanajeshi waliwasili kwa malori nje ya afisi za kutetea haki za binadamu za Umoja wa Mataifa (UNHRC) katika mji mkuu wa taifa hilo Kampala na kuanza kuwapiga wanahabari.

Kulingana na taarifa ya muungano wa wahariri nchini humo, angalau wanahabari 10 wa mashirika tofauti ya habari walijeruhiwa kabla kupelekwa hospitalini kwa matibabu.

Mwanahabari mmoja aliweka katika mtandao wa Twitter, picha za yaliyokuwa yakijiri katika eneo hilo huku akionyesha mmoja wa wanahabari akitokwa na damu kichwani.

Kituo kimoja cha kibinafsi cha runinga kilionyesha picha za wanahabari wakitoroka ili kuepuka kucharazwa.

Akijibu shutuma hizo, Msemaji wa vikosi hivyo vya usalama Brigadia Generali Flavia Byekwaso amesema kundi lililoandamana na Bobi Wine walijeruhi afisa mmoja wa usalama ndiposa ikabidi wafurushwe kwa nguvu.

Kuna wasi wasi nchini Uganda kuhusu hatima ya wafuasi wa upinzani ambao wamesemekana kutoweka.Waliokamatwa wamesemekana kuteswa.

Rais Yoweri Museveni hivi maajuzi alisema kuwa watu 300 wamezuiliwa kwa kuzua vurugu na kuhusika na visa vingine vya uhalifu.

Categories
Burudani

Cindy Sanyu azungumzia tuzo za MAMA

Mwanamuziki wa Uganda wa mtindo wa dancehall Cindy Sanyu amesema kwamba hasumbuliwi na hatua ya waandalizi kukosa kumteua kuwania tuzo za MAMA mwaka 2021.

Cindy ni mmoja wa wasanii wa muziki walioinuka sana hivi karibuni hasa kuanzia mwisho wa mwaka 2019 na wengi walitarajia kwamba atakuwa mmoja wa wawaniaji wa tuzo hizo ambazo zitaandaliwa nchini Uganda.

Mwanamuziki huyo sasa anasema kwamba hatua ya yeye kukosa kuteuliwa kuwania tuzo za MAMA haibadilishi chochote katika kazi yake kama mwanamuziki kwani tayari ashakuwa msanii mkubwa na ameafikia mengi.

“Sikukasirika nilipokosa kuteuliwa kwa tuzo hizi kwani mimi ni msanii mkubwa sana ambaye hahitaji tuzo la MAMA kunisongesha mbele. Tayari nimeshinda tuzo la AFRIMMA kwa hivyo sihitaji uteuzi wao.” alisema Cindy wakati alihojiwa na kituo kimoja cha runinga nchini Uganda.

Cindy ni mmoja wa wale ambao waliomba kwamba tuzo za MAMA ziahirishwe kwani watu wa nchi hiyo walikuwa na maambo mengine mengi ya maana ya kushughulikia na mengi yalitokana na janga la Corona.

Alionekana pia kutokubaliana na hatua ya kuchaguliwa kwa mwanamuziki wa Marekani DJ Khaled kuongoza au kuwa mtangazaji mkuu wa hafla ya tuzo za MAMA.

Watu wengi nchini Uganda walionelea kwamba haingekuwa vyema kuandaa hafla ya kutuza wshindi wa MAMA wakati ambapo wengi hawawezi kujimudu baada ya kupoteza ajira na vitega uchumi kutokana na Janga la Corona.

Wanaharakati pia hawakufurahishwa na hafla hiyo ambayo ingeandaliwa wakati ambapo wanamuziki wengi wamefungiwa na hawawezi kuandaa tamasha nchini Uganda.

Tuzo za MAMA zingeandaliwa mwezi huu wa pili mwaka 2021 nchini Uganda lakini zikaahirishwa kwa muda usiojulikana kutokana na malalamishi ya wengi nchini humo.

Mwanadada Cindy ndiye naibu rais wa chama cha wanamuziki wa Uganda almaarufu “Uganda Musicians Association” na amesema kwamba hatawania urais wa chama hicho baada ya Ykee Benda kujiuzulu.

Categories
Michezo

Uganda yaipakata Msumbiji AFCON U 20

Timu ya Uganda maarufu kama Hippos imeanza vyema mechi za kundi A katika mashindano ya kuwania kombe la AFCON kwa chipukizi walio chini ya umri wa miaka 20 baada ya kuwacharaza Msumbiji mabao 2-0 katika mechi iliyochezwa Jumatatu alasiri nchini Mauritania .

Mshambulizi wa klabu ya Police Derrick Kakooza alipachika bao la kwanza dakika ya 57 kupitia penati kabla ya kiungo wa KCCA Steven Serrwada dakika 4 kabla ya kipenga cha mwisho huku ushindi huo ukiwaweka katika nafais nzuri ya kutinga robo fainali wakiongoza kundi hilo kwa alama 3 sawa na Cameroon kuelekea kwa mechi kati ya timu hizo mbili Jumatano hiii.

Mashindano hayo yanashirikisha mataifa 12 huku fainali yake ikipigwa tarehe 6 mwezi ujao.

 

Categories
Kimataifa

Mahakama ya Uganda yaagiza Bobi Wine aachiliwe huru

Mahakama moja nchini Uganda imetoa agizo kwa maafisa wa usalama kuondoka nyumbani kwa mwanasiasa wa upinzani Bobi Wine.

Hii ni baada ya mahakama hiyo kuitaja hatua ya kumuweka Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine, kwenye kifungo cha nyumbani kuwa isiyo halali.

Mwanasiasa huyo hajaweza kutoka nyumbani kwake tangu aliporudi kutoka kituo alikopigia kura katika uchaguzi mkuu nchini humo siku 11 zilizopita.

Agizo la kuachiliwa huru kwa Bobi mapema Jumatatu limetolewa kufuatia uamuzi wa kesi iliyowasilishwa na mawakili wake ya kupinga hatua ya maafisa wa usalama wa serikali kuendelea kuzingira makazi yake.

Hatua hiyo ilishutumiwa vikali na baadhi ya viongozi na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu ulimwenguni lakini maafisa hao wakadai kwamba Bobi alikuwa akipewa ulinzi kwa sababu alikuwa mgombea urais.

Tume ya uchaguzi nchini humo ilimtangaza Bobi kuwa aliibuka nafasi ya pili kwenye kinyang’anyiro cha urais, baada ya kushindwa na Rais Yoweri Museveni.

Hata hivyo, Bobi alipinga vikali matokeo hayo, akidai kwamba anao ushahidi wa kutosha wa kudhihirishwa kuwa kulikuwa na udanganyifu mkubwa katika shughuli ya kuhesabu na kujumlisha kura hizo.

Categories
Michezo

Waakilishi wa East Africa waning’inia kubanduliwa CHAN

Waakilishi wa Afrika mashariki Uganda,Rwanda na Tanzania wanakaribia kuyaaga mashindano ya kuwania kombe la CHAN nchini Cameroon.

Uganda Cranes wanaoshiriki kwa mara ya 5 kati ya makala ya 6 ya CHAN wanakariabia kuyaaga mashindano katika hatua ya makundi kwa mara ya 5 mtawalia baada ya kuambulia kichapo cha 1-2 kutoka kwa limbukeni Togo Ijumaa usiku katika uwanja wa Reunification mjini Doula Cameroon.

Baada ya kipindi cha kwanza kumalizika kwa sare tasa katika mchuano huo wa kundi C, kipindi cha pili kilikuwa na msisimko wa aina yake huku beki wa Uganda Paul Mbowa  akijaribu kuondosha mpira kwenye eneo la hatari aliupiga kwa kichwa na kutumbukia katika lango lake lakini dakika chache Waganda wakasawazisha kupitia kwa Saidi Kyeyune aliyepiga tobwe la mbali na kutua kimiani.

Dakika 6 baadae Yendoutie Nane aliifungia Togo maarufu kama Sparrow Hawks bao la ushindi baada ya kupata mwanya kwnye safu ya Ulinzi na kusajili ushindi wa kwanza .

Katika pambano la awali Amavubi ya Rwanda na mabingwa watetezi Moroko waliambulia sare tasa  ,huku Moroko wakihitaji angaa pointi katika mechi ya mwisho Jumanne ijayo dhidi ya Uganda,ili kufuzu kwa robo fainali wakati Rwanda wakihitaji ushindi dhidi ya Togo ili kufuzu kwa awamu ya nane bora kwa mara ya pili.

msimamo wa kundi C

1.Moroko—-alama 4

2.Togo——-alama 3

3.Rwanda—-alama 2

4.Uganda —-alama 1

Waakilishi wa mwisho wa East Africa Taifa Stars kutoka Tanzania watamenyana na Brave Warriors kutoka Namibia katika kundi D mchuano ambaye atakayepoteza atakuwa timu ya pili kuyaaga mashindano baada ya Zimbabwe hususan kufuatia timu zote kupoteza mechi za ufunguzi.

Tanzani ilicharazwa magoli 2-0 na Zambia huku Namibia wakinyukwa 3-0 na Guinea.

Pambano la ufunguzi la kundi D Jumamosi litakuwa baina ya Guinea na Zambia kuanzia saa moja usiku huku atakayeshinda  akifuzu kwa robo fainali baada ya timu zote kushinda mechi za ufunguzi.

Mechi za kuhitimisha hatua ya makundi zitaanza Jumapili usiku na kukamilika Jumatano ijayo kabla ya kupisha robo fainali Jumamosi na Jumapili ijayo.

 

Categories
Kimataifa

Marekani yataka kuchunguzwa kwa ghasia za uchaguzi nchini Uganda

Muungano wa Ulaya na Marekani zimetoa wito wa uchunguzi kufanywa kuhusiana na ghasia za uchaguzi zilizotokea nchini Uganda huku kiongozi wa upinzani nchini humo Bobi Wine akiendelea kuzuiliwa nyumbani.

Rais Yoweri Museveni alitangazwa mshindi kwa hatamu ya sita huku mtandao wa internet ukifungwa na madai ya unyanyasaji wa watu yakitolewa.

Viongozi wa upinzani na wafuasi wa upinzani nchini humo wamelalamika kutokana na visa vya kuhangaishwa na maafisa wa usalama kabla na baada ya uchaguzi huo.

Msemaji wa serikali ya Uganda Jumanne alimtuhumu balozi wa Marekani nchini  Uganda Natalie Brown kwa kukiuka maadili ya kibalozi kwa kujaribu kumtembelea kiongozi wa upinzani  Bobi Wine, ambaye anazuiliwa nyumbani kwake.

Wine, mwenye umri wa miaka 38, aliibuka wa pili kwenye uchaguzi huo wa urais ambao ulimdumisha mamlakani Yoweri Museveni kwa hatamu ya sita na amesema ametenganishwa na mawakili wake na chama huku akinuia kupinga matokeo ya uchaguzi huo mahakamani.

Msemaji wa serikali ya nchi hiyo Ofwono Opondo alisema jaribio hilo  la Brown ni ishara kuwa hana nia njema.

Categories
Burudani

Jose Chameleon akosa umeya wa Kampala

Uchaguzi wa Umeya nchini Uganda uliandaliwa jana tarehe 20 mwezi Januari mwaka huu wa 2021 na wala sio tarehe 14 wiki jana kama ilivyodhaniwa na wengi.

Mwanamuziki Jose Chameleone au ukipenda Joseph Mayanja alikuwa mmoja wa wawaniaji 11 wa kiti cha meya wa jiji kuu Kampala.

Hata hivyo taarifa za sasa kutoka Kampala zinaonyesha kwamba Lord Mayor Erias Lukwago wa chama cha FD ambaye kitaaluma ni wakili na amewahi kuhudumu kama mbunge amehifadhi kiti chake.

Chameleone ameshindwa kwenye kinyang’anyiro hicho kinyume na ripoti za awali kwenye mitandao ya kijamii hata kabla ya uchaguzi wa umeya nchini Uganda kwamba alikuwa ameshinda.

Kwenye shughuli hiyo ya jana iliyoshuhudia idadi ndogo ya wapiga kura, Jose Chameleone alipiga kura katika kituo cha Kiduuka huko Mitungo akiwa ameandamana na kaka zake Pius Mayanja kwa jina lingine pallaso na Douglas Mayanja kwa jina lingine Weasel.

Kaka hao wawili pia ni wanamuziki.

Chameleone aliingia kwenye kinyang’anyiro hicho kama mwaniaji huru baada ya kushindwa kupata tileti ya chama cha mwanamuziki mwenza Bobi Wine cha NUP ambayo ilitwaliwa na Latif Sebaggala.

Inasemekana kwamba Jose alikosa tikiti ya NUP kwa kukosa vyeti vinavyohitajika vya masomo na kukosa kitambulisho cha kitaifa.

Hata hivyo aliahidi kuendelea kumuunga mkono Bobi Wine ambaye alikuwa akiwania Urais wakati huo lakini kulingana na matokeo, alishindwa na Rais Yoweri Museveni.