Categories
Michezo

Viboko wa Uganda kukabiliana na Ngorongoro Heroes ya Tanzania fainali ya CECAFA

Fainali ya kuwania  kombe la Cecafa kwa vijana  chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 itapigwa Jumatano  alasiri baina ya mabingwa watetezi Tanzania dhidi ya Uganda katika uwanja wa Black Rhino Academy eneo la Karatu mjini Arusha Tanzania.

Wenyeji Tanzania maarufu kama Ngorongoro Heroes  walianza safari ya michuano  hiyo katika kundi A  kwa kuipakata  Djibouti magoli 6-1 ,kabla ya kuimenya Somalia mabao 8-1 katika pambano la mwisho na hatimaye  kuibandua Sudan Kusini bao 1-0 kwenye nusu fainali.

Upande mwingine  Viboko wa Uganda au Hippos walianza kundi B kwa kutoka sare tasa dhidi ya Sudan Kusini kabla ya kuigaragaza  Burundi mabao 6-1 katika mechi ya mwisho na kuitema kenya mabao 3-1 kwenye nusu fainali.

Uganda na Tanzania tayari zimejikatia tiketi kupiga fainali za 15 za kuwania kombe la Afcon mwaka ujao nchini Mauritania kwa kufika fainali.

Tanzania wakipiga fainali ya mwaka jana dhidi ya Kenya

Fainali ya Jumatano  itashuhudia Tanzania wakilenga kuhifadhi ubingwa wa mwaka uliopita wakati Waganda pia wakipania kulipiza kisasi kwa kukosa kunyakua kombe hilo wakiwa nyumbani mwaka uliopita.

Kenya na Sudan Kusini zitamenyana kuanzia saa sita adhuhuri katika mechi ya kuwania nafasi ya tatu na nne katika uwanja wa Black Rhino Academy eneo la Karatu mjini Arusha.

 

 

Categories
Michezo

Uganda Hippos wabanwa mbavu na Sudan Kusini CECAFA

Uganda walilazimishwa kwenda sare tasa dhidi ya Sudan Kusini katika mechi ya ufunguzi ya kundi B kuwania kombe la Cecafa kwa vijana walio chini ya umri wa  miaka 20 iliyochezwa Jumatatu jioni katika uwanja wa Black Rhino Academy Complex.

Ilikuwa mara ya  tatau mtawalia kwa timu ya Uganda kutatizwa na  Sudan Kusini,baada ya Uganda Cranes kuhitaji bao la dakika ya mwisho kabla ya kuishinda Sudan Kusini katika pambano  kufuzu kwa kombe la Afcon jijini Kampala kabla ya kucharazwa na Sudan Kusini bao 1-0 kwenye mechi ya marudio iliyochezwa katika uwanja wa taifa wa Nyayo.

Uganda maarufu kama Hippos  watarejea uwanjani Jumatano kwa mechi ya pili dhidi ya Burundi mechi ambayo lazima washinde ili kufuzu kwa nusu fainali.

Mashindano ya Cecafa yataingia siku ya tatu Jumanne kwa mchuano mmoja wa kundi  A kati ya Djibouti na Somalia katika uwanja wa Black Rhino Academy Complex kuanzia saa kumi alasiri.

Mechi za makundi zitafikia tamati Ijumaa kabla ya nusu fainali kung’oa nanga Novemba 30 ikifuatwa na fainali ya Disemba 2.

Timu bora kutoka kila kundi na timu bora ya pili kutoka makundi yote matatu zitafuzu kwa nusu fainali ilihali timu mbili bora zikifuzu kuwakilisha ukanda wa Cecafa katika mashindano ya kombe la mataifa ya afrika Afcon mwaka ujao nchini Mauritania.