Categories
Kimataifa

Maafisa watatu wa polisi Ufaransa wasimamishwa kazi kwa kumdhulumu mtu mweusi

Utawala wa Ufaransa umewasimamisha kazi maafisa watatu wa polisi baada ya kuonekana kwenye video wakimpiga mtu mmoja mweusi kati kati mwa Jiji la Paris.

Kisa hicho cha siku ya Jumamosi kimeibua malalamiko mengi nchini Ufaransa kuhusu mienendo ya maafisa wa usalama.

Hayo yanajiri huku serikali ikijaribu kuanzisha sheria itakayoharamisha kuonyeshwa kwa nyuso za maafisa wa polisi kwenye vyombo vya habari.

Wakosoaji wa sheria hiyo wanasema pasipo picha za aina hiyo, hakuna kisa hata kimoja ambacho kingefahamika wazi kati ya vile vilivyotokea juma lililopita.

Mnamo siku ya Alhamisi, mchezaji soka shupavu Kylian Mbappe, ambaye ni mweusi aliungana na wenzake wa timu ya taifa ya Ufaransa na pia wana riadha katika kulaani kisa hicho cha hivi punde.

Picha za video kuhusu kisa hicho zinaonyesha maafisa watatu wa polisi wakimpiga kwa mateke, makondo na virungu mtu huyo baada ya kuingia kwenye studio yake ya kurekodi nyimbo.

Categories
Kimataifa

Ufaransa kulegeza masharti ya COVID-19 msimu wa Krismasi

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema nchi yake itaanza kulegeza masharti yaliyowekwa katika kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Corona, kwa kuruhusu baadhi ya maduka kuendelea na biashara zao, kuanzia mwishoni mwa juma hili.

Macron ametangaza kuwa watu wataruhusiwa pia kutangamana na familia zao msimu ujao wa sherehe za Krismasi.

Hata hivyo, rais huyo amesema baa na migahawa zitaendelea kufungwa hadi tarehe 20 Januari mwaka ujao.

Ufaransa imeripoti zaidi ya visa milioni 2.2 vya watu walioambukizwa Corona na vifo vya zaidi ya watu elfu 50 tangu kuripotiwa kwa kisa cha kwanza cha ugonjwa wa COVID-19 nchini humo.

Kupitia hotuba ya televisheni, Macron amesema nchi yake imepita kilele cha wimbi la pili la maambukizi ya Corona.

Amesema kwamba masharti mengi yaliyotangazwa kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo yatalegezwa kaunzia tarehe 15 Desemba kwa ajili ya sherehe za Krismasi, ambapo kumbi za sinema zitafunguliwa na masharti yaliyowekewa shughuli za usafiri kuondolewa iwapo kiwango cha maambukizi mapya kitakuwa chini ya visa 5,000 kwa siku.

Mnamo siku ya Jumatatu, Ufaransa ilitangaza visa vya watu 4,452 walioambukizwa ugonjwa wa COVID-19 katika muda wa masaa 24, hiyo ikiwa idadi ya chini zaidi nchini humo tangu tarehe 28 Septemba.

Kiwango cha wastani cha maambukizi ya Corona kwa siku kilikuwa visa 21,918 ambapo kilele chake kilikuwa visa 54,440 mnamo tarehe 7 mwezi huu.

Categories
Kimataifa

Ufaransa yaripoti zaidi ya visa 60,000 vya COVID-19 kwa siku moja

Ufaransa imenakili visa vipya 60,486 vya maambukizi ya Korona katika muda wa siku moja, kiwango ambacho ni cha juu zaidi kunakiliwa kwa siku tangu kutokea kwa chamko la ugonjwa huo.

Idadi hiyo mpya imeongeza kiwango cha watu walioambukizwa ugonjwa huo nchini humo hadi watu million 1.7 kulingana na takwimu kutoka Chuo Kikuu cha Johns Hopkins.

Jumla ya vifo 828 viliripotiwa jana huku ikiwa takriban watu elfu 40 wameaga dunia nchini humo kutokana na ugonjwa huo.

Serikali ya Ufaransa wiki iliyopita iliweka masharti makali ya watu kusalia nyumbani kwa mara ya pili ili kukabiliana na msambao wa Korona.

Masharti hayo makali ya watu kutotoka majumbani mwao yatakuwapo hadi tarehe moja mwezi ujao.

Katika muda huo, watu wanaweza tu kuondoka nyumbani kwenda kazini iwapo hawawezi kufanyia kazi nyumbani au kwenda kununua bidhaa muhimu za matumizi ya nyumbani na kwenda kwa matibabu kwa muda wa saa moja pekee kwa siku.

Maduka yasiyouza bidhaa za lazima, migahawa na baa zimefungwa lakini masomo shuleni yanaendelea.

Amri ya kutotoka nje ingalipo kati ya saa nne usiku na saa 12 alfajiri nchini humo.

Categories
Kimataifa

Ufaransa yaapa kuimarisha juhudi za kupambana na Corona hadi mwaka ujao

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema taifa hilo litaendelea kupambana na janga la korona hadi katikati ya mwaka ujao.

Tangazo hilo limetolewa huku visa vya maambukizi nchini humo vikipita watu milioni moja.

Siku ya Ijumaa Ufaransa ilirekodi zaidi ya visa 40,000 vipya vya maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 na jumla ya vifo 298.

Mataifa mengine ambayo yamerekodi ongezeko la visa vipya vya ugonjwa huo ni Urusi, Poland, Italia na Uswizi.

Shirika la Afya duniani WHO limesema huu ni wakati muhimu kwa mataifa ya Ulaya kuimarisha mbinu za kuzuia msambao wa ugonjwa huo na kuhakikisha kuwa mitandao ya huduma za afya inakabiliana vilivyo na janga hilo.

Idadi ya wastani ya kila siku ya maambukizi ya ugonjwa huo imeongezeka mara dufu katika muda wa siku kumi zilizopita.

Bara la Ulaya sasa limerekodi visa  milioni 7.8 vya ugonjwa huo na karibu  vifo vya watu 247,000.

Kimataifa, jumla ya visa milioni 42 vya mambukizi ya ugonjwa huo vimerekodiwa na vifo milioni 1.1.

Akiongea katika hospitali moja jijini Paris, Rais Macron amesema kwamba kwa mujibu wa ripoti ya wataalamu wa magonjwa nchini humo, ugonjwa huo huenda ukasalia nchini humo hadi katikati ya mwaka ujao.

Ufaransa imeongeza tena muda wa makataa ya kutotoka nje usiku kwa majuma sita.

Categories
Kimataifa

Bara la Ulaya laongeza juhudi za kukabiliana na maambukizi ya COVID-19

Jamhuri ya Czech inaweka kizuizi cha kadiri cha wiki tatu, huku ikifunga shule, baa na vilabu wakati Ulaya ikijitahidi kudhibiti kuongezeka kwa visa vya maradhi ya COVID-19.

Shule, baa na vilabu vitasalia kufungwa hadi tarehe tatu mwezi ujao huku migahawa ikiruhusiwa tu kuwasilisha chakula kwa wateja au kukiuza kwa kuwapakia, hadi saa mbili usiku kila siku.

Mabweni ya vyuo vikuu pia yanafungwa kwa muda, na masomo yataendeshwa wanafunzi wakiwa nyumbani kupitia mtandao.

Shule za chekechea zitasalia kufungwa na mikakati maalum kuwekewa watoto wa wafanyakazi wa kutoa huduma muhimu.

Kumerekodiwa vifo 1,051 vya kutokana na maradhi ya COVID-19 katika Jamhuri ya  Czech tangu tarehe mosi mwezi Machi, wakati taifa hilo lilipothibitisha kisa cha kwanza cha maradhi hayo.

Uholanzi pia iliamuru kufungwa kwa migahawa na unywaji wa pombe kwenye maeneo ya umma umepigwa marufuku na sharti barakoa zivaliwe katika maeneo hayo.

Naye Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema kwenye hotuba ya televisheni kuwa atatangaza vizuizi zaidi.

Chancella wa Ujerumani Angela Merkel amesikitishwa na  hali inayozidi kuzorota Barani Ulaya.