Categories
Burudani

Tory Lanez ataka aruhusiwe kuzungumzia kesi yake na Megan Thee Stallion

Mwanamuziki wa nchi ya Canada Tory Lanez ameomba mahakama impatie ruhusa ya kuzungumzia matukio yaliyosababisha kesi ambayo inaendelea kortini dhidi yake.

Lanez haelewi jinsi Megan ana uhuru wa kuzungumzia kesi hiyo hata kwenye mitandao ya kijamii huku yeye akibanwa na agizo la mahakama linalomzuia kusema chochote kuhusu kesi hiyo.

Agizo hilo pia linamzuia kuwasiliana na Megan na kumkaribia.

Mwezi Julai mwaka 2020, Megan alipachika picha kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha kisigino cha mguu wake kikiwa kimeshonwa na kuelezea kwamba anafurahia kuwa hai baada ya kupigwa risasi.

Anaendelea kuelezea kwamba nia ya aliyemshambulia ilikuwa kumdhuru na kwamba hakutiwa mbaroni Jumapili asubuhi tarehe 12 mwezi Julai mwaka 2020 bali maafisa wa polisi walimpeleka hospitalini ambako alifanyiwa upasuaji kuondoa risasi na kumshona.

Tory Lanez ambaye anasemekana kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na Megan The Stallion wakati huo alikamatwa siku hiyo hiyo yapata saa kumi asubuhi kwa kosa la kuwa na silaha ambayo alikuwa ameficha kwenye gari na baadaye kuachiliwa huru baada ya kulipa dhamana ya dola elfu 35.

Wawili hao walikuwa wamehudhuria sherehe nyumbani kwa kylie Jenner ambako mvutano kati ya Megan na Tory ulitokea wakiwa ndani ya gari jumapili asubuhi.

Polisi ambao walikuwa wakishika doria walifika mahali hapo mara moja na wakampeleka Megan hospitalini na kumkamata Tory.

Afisi ya wakili katika wilaya ya Los Angeles ndiyo iliweka kesi hiyo mahakamani na alipofikishwa mahakamani mwezi Novemba mwaka 2020, Tory Lanez alikana mashtaka dhidi yake.

Megan amekuwa akizungumzia kesi hiyo kwenye mitandao ya kijamii na ndio maana sasa, Tory naye ameomba mahakama imkubalie naye aseme ukweli wake kuhusu kesi hiyo.

Tory Lanez ambaye jina lake halisi ni Daystar Peterson alizindua albamu yake ya tano kwa jina “Daystar” ambayo ametumia kuzungumzia matukio kati yake na Megan yaliyosababisha kesi ambayo inaendelea mahakamani.

Categories
Burudani

Shakilla asema ana ujauzito wa Eric Omondi!!

Baada ya kushindwa kwenye shindano la “Wife Material” ambalo lilikuwa la kumtafutia mke mchekeshaji Eric Omondi, Shakilla msichana wa vituko vingi amejitokeza na kudai kwamba ana ujauzito wa Eric na mwanawe mtarajiwa hawezi kulelewa mitaani bila baba.

Shakilla ambaye ni maarufu kwenye mtandao wa Instagram anasema mimba hiyo ni ya wiki mbili tu. Swali ni, anajuaje ni mtoto wa kike anatarajia? (Hii ni baada yake kurejelea mwanawe kama “Princess”.)

Kwenye Instagram, Shakilla alipachika video akimpongeza Carol wa Band Beca kwa kuchaguliwa na wakenya kuwa mke wa Eric Omondi lakini akaendelea kwa kusema kwamba Eric na yeye wanajua kwamba walifungamana milele na hakuna awezaye kuvunja uhusiano huo.

Hapo ndipo alimwaga mtama kwamba ana ujauzito.

Shakilla amekuwa akijitafutia umaarufu kwa njia zote kwenye mitandao ya kijamii jambo ambalo limesababisha afanye vituko. Wakati mmoja alivua nguo na kucheza akiwa mubashara kwenye Instagram na mwanamuziki Tory Lanez wa Canada.

Wakati mwingine alitiwa mbaroni kwa kuingia kwenye makazi ya mwanamuziki Willy Paul bila mwaliko na Willy akamshtaki kwa polisi.

Baadaye alidai kwamba anamiliki jumba la kifahari na kwamba anaishi maisha mazuri lakini picha zikasambazwa mitandaoni zikimwonyesha akipika ndani ya nyumba ya chumba kimoja almaarufu “bedsitter”.

Huku haya yakijiri, mmoja wa wasichana ambao walikuwa kwenye shindano la Wife Material kwa jina “Shilah” kutoka Kitale alijitokeza na kusema kwamba mchekeshaji Eric Omondi hakujamiiana nao na kwamba aliwaheshimu sana.

Lakini video ambazo Eric mwenyewe alizichapisha kwenye Instagram mara kwa mara, zilimwonyesha akibusu wasichana tofauti waliokuwa wakimshindania.

Eric omondi hajajibu madai hayo ya Shakilla.