Categories
Burudani

Msanii Q Chief atoa ilani kwa Wasafi Media

Msanii wa Bongo Fleva Q Chief ameupa usimamizi wa Wasafi Media na Kampuni ya Tigo muda hadi mwisho wa siku hii leo ili apate maelezo kamili kuhusu sababu ya kuweka jina lake na picha yake kwenye bango la tamasha lao bila idhini yake.

Kupitia Instagram, Q Chief alisema kwamba hakuna yeyote aliwasiliana naye rasmi kutoka kwa kampuni hizo ili kumshirikisha kwenye tamasha hilo la Jumamosi tarehe 30 mwezi Januari mwaka 2021 almaarufu kama “Wasafi Tumewasha na Tigo”.

Anaendelea kuelezea kwamba mashabiki wake wengi wamekuwa wakimpigia simu kujua ni kwa nini hakuonekana kwenye tamasha hilo ilhali walikuwa wakimtarajia jambo ambalo anasema linaathiri kazi yake ya muziki.

Q Chief anasema amekuwa akijaribu kuwasiliana na usimamizi wa Wasafi Media bila mafanikio huku akiambiwa kwamba wahusika bado wana uchovu wa tamasha la jumamosi.

Hata hivyo wengi wa mashabiki wake kwenye Instagram, wanaonelea kwamba hakustahili kuweka ilani hiyo kwenye mitandao ya kijamii na kwa kufanya vile wanahisi anajitafutia umaarufu.

Hakuna jibu lolote limetolewa na Wasafi Media inayomilikiwa na Diamond Platnumz wala kampuni ya mawasiliano ya rununu ya Tigo kuhusu lalama za Q Chief.

Categories
Burudani

Tangazo la Diamond Platnumz mkurugenzi mkuu wa Wasafi Media

Inatokea kwamba tangazo ambalo lilikuwa linasubiriwa kwa hamu na ghamu kutoka kwa Diamond Platnumz sio kuhusu kuzinduliwa kwa collabo yake na Koffi Olomide.

Tangazo lenyewe ni kuhusiana na ushirikiano wa kibiashara kati ya Wasafi Media, kampuni ya mawasiliano ya rununu nchini Tanzania Tigo na kampuni ya vinywaji ya Pepsi.

Kampuni hizo tatu zitakuwa na ziara katika sehemu mbali mbali nchini Tanzania kwa lengo la kuongeza mauzo.

Akizungumza kwenye makao makuu ya Wasafi Media huko Mbezi, mkurugenzi mkuu wa Wasafi Media Abdul Nasib au Diamond Platnumz alisema kwamba kampuni hiyo ya utangazaji inashirikiana na Tigo na Pepsi kutembelea wateja wake katika mikoa ambapo vituo vya Wasafi vimewashwa na ambapo vitawashwa.

“Linaitwa Wasafi tumewasha na Tigo na unajiburidisha na Pepsi mpaka basi!” maneno yake Diamond hayo.

Kulingana naye hawajapata nafasi ya kushukuru wasikilizaji na watazamaji wao kwa kupendelea Wasafi Media na hii ni nafasi nzuri na njia bora ya kumaliza mwaka.

Msafara wenyewe utaanza tarehe 28 mwezi huu wa Novemba mwaka 2020 katika eneo la Kahama na utahusisha wasanii wa kampuni ya Wasafi na wengine wa nje na orodha kamili itatolewa baadaye.

Wasimamizi wa mauzo kutoka kampuni za Tigo na Pepsi pia walizungumza kwenye kikao hicho na wanahabari ambapo waliahidi wateja wao mengi mazuri kwenye msafara huo.