Categories
Burudani

Mwanamuziki wa Tanzania CPwaa aaga Dunia

Mwanamuziki wa nchi ya Tanzania CPwaa ambaye alijulikana sana kwa mitindo kama vile Hip Hop, Rap na Crunk aliaga dunia jana akipokea matibabu katika hospitali ya Muhimbili Jijini Daresalaam.

CPwaa ambaye jina lake halisi ni Ilunga Khalifa anasemekana kuugua ugonjwa wa homa ya mapafu kwa muda.

Mwili wake tayari umezikwa nyumbani kwao katika eneo la Magomeni kulingana na tamaduni za dini ya kiisilamu.

Binamu yake Murad Omar Khamis aliyehojiwa alifichua kwamba Cpwaa amekuwa akiumwa kwa muda wa wiki mbili lakini akazidiwa jumatano na wakamkimbiza hospitali ambapo alilazwa kwenye chumba cha wagonjwa walio hali mahututi.

Alikata roho alfajiri jumapili tarehe 17 mwezi huu wa Januari mwaka 2021.

Wasanii wengi wa Bongo, akiwemo Ali Kiba na TID walifika nyumbani kwa mamake Cpwaa huko Magomeni kwa ajili ya kuifariji familia.

Cpwaa alikuwa akiimba kwenye kundi linalofahamika kama “Park lane” na lilikuwa la watu wawili, yeye na msanii Suma Lee.

Wakiwa pamoja walirekodi na kuzindua vibao kama vile Nafasi nyingine na Aisha lakini kundi hilo baadaye lilisambaratika.

Wasanii wengi na watu maarufu nchini Tanzania walimwomboleza kwenye mitandao ya kijamii kama vile mtayarishaji muziki kwa jina S2kizzy kwenye Instagram. Aliweka picha ya marehemu Cpwaa na kuandika, “RIP big brother Cpwaa. Gone too soon.”