Categories
Michezo

Tanzania yagura CHAN baada ya kuwahemesha Guinea

Taifa Stars ya Tanzania iligura michuano ya CHAN mwaka 2020 nchini Cameroon kifalme baada ya kuwahemesha vigogo wa Afrika magharibi Guinea na kulazimisha sare ya magoli 2-2 katika mechi ya mwisho ya kundi D jumatano usiku katika uwanja wa Reunification mjini Doula.

Yakhouba Barry aliwaweka Syli Nationale ya Guinea uongozini kwa bao la penati ya dakika 4 kabla ya Taifa Stars kujibu kupitia kwa Baraka Majogoro aliyefyatua fataki kutoka umbali wa miguu 20  iliyomduwaza kipa wa Guinea kunako dakika ya 23 na kipindi cha kwanza kuishia sare ya 1-1.

Kipindi cha pili Tanzania waliendelea kucheza mchezo wa kuridhisha na pasi za kuonana ndiposa Edward Manyama akapachika goli la pili  kupitia kichwa dakika ya 68 ,bao lililopangua mchezo wa Guinea walionusia hatari ya kubanduliwa.

Hata hivyo mabadiliko ya kiufundi kutoka kwa kocha wa Guinea yaliongeza makali huku vijana hao kutoka Afrika magharibi wakiongeza mashambulizi yaliyozaa matunda pale Victor Kantabadouno alipouchupia mpira na kupiga bao la pili  dakika ya 82 ,goli ambalo liliwahakikishia uongozi wa kundi D na kuwabandua Tanzania.

Katika mechi nyingine ya kundi D uwanjani Limbe Namibia walitoka sare tasa dhidi ya Zambia.

Guinea waliongoza kundi hilo kwa pointi 5 wakifuatwa na Zambia pia kwa alama 5 wakati Tanzania ikiibuka ya tatu kwa alama 4 nayo Namibia ikashika nanga kwa pointi moja.

Categories
Michezo

Tanzania yasajili ushindi wa kwanza CHAN na kuitimua Namibia

Taifa Stars ya Tanzania ilisajili ushindi wa kwanza katika michuano ya CHAN inayoendelea baada ya kuwaangusha Namibia goli 1-0 katika mechi ya kundi D iliyochezwa Jumamosi usiku katika uwanja wa Limbe.

Farid Mussa ambaye pia alitawazwa mchezaji bora alifunga bao hilo katika dakika ya 65 alitumia makosa ya mabeki wa Namibia walioshindwa kuondosha mpira katika lango lao na kufyatua mkwaju ulimwacha hoi kipa wa Namibia Kamaijanda Ndisiro.

Namibia maarufu kama Brave warriors walijaribu kwa udi na uvumba kurejesha bao hilo bila mafanikio huku kipa wa Taifa Stars Aishi Manula akipangua mikwaju mingi ya Wanamibia.

Matokeo hayo yanafufua matumaini ya Tanzania kufuzu kwa robo fainali wakihitaji ushindi dhidi ya Guinea Jumatano ijayo ili kufuzu kwa robo fainali.

Katika mechi ya awalia ya kundi hilo Jumamosi jioni Zambia walihitaji bao la dakika ya 87 ili kujinusuru na kulazimisha sare ya 1-1 dhidi ya Guinea na kuacha kundi hilo wazi kwa nafasi ya kutinga robo fainali.

Victor Kantabadouno aliwaweka Guinea kifua  mbele kwa bao la dakika ya 58  kabla ya Spencer Sautu kusawazishia Zambia dakika ya 87.

Mechi za Kundi A zinakamilika Jumapili usiku Mali wakichuana Zimbabwe nao  Burkinafasso wapimane nguvu na  wenyeji Cameroon .

Mechi hizo zitabaini timu mbili zitakazofuzu kwa robo fainali ya Jumamosi na Jumapili ijayo.

Categories
Michezo

CHAN kuingia siku ya 4 mjini Limbe Tanzania wakifungua pazia na Zambia

Chipolopolo ya Zambia watafungua ratiba ya kundi D ya michuano ya Chan Jumanne usiku dhidi ya Taifa Stars ya Tanzania saa moja usiku katika uwanja wa Limbe Omnisport mjini Limbe Cameroon.

Tanzania wanashiriki michuano ya CHAN kwa mara ya 2 baada kushiriki kwa mara ya kwanza mwaka 2009 walipotoka sare moja ,kushinda mchuano mmoja na kupoteza mmoja.

Upande wao Chipolopolo wanacheza CHAN kwa mara ya 4 na ya 3 mtawalia baada ya kushiriki miaka ya 2016 na 2018 ambapo waliibuka wa tatu mwaka 2009 huku wakicheza hadi robo fainali mwaka 2016 na 2018.

Baadae saa nne usiku Brave Warriors ya Namibia watashuka uwanjani Limbe Omnisport dhidi ya Syli Nationale ya Guinea .

Guinea wanacheza CHAN kwa mara  ta tatu mtawalia  baada ya kukosa makala matatu ya wkanza  na waliibuka wa nne mwaka 2016 kabla ya kuyaaga mashindano katika  hatua ya makundi mwaka 2018.

Namibia wanashiriki CHAN kwa mara ya pili baada ya kubanduliwa na wenyeji Moroko katika robo fainali mwaka 2018 mabao 2-0.

Mechi 6 zimepigwa kufikia sasa  na mabao 4 kufungwa  nazo  mechi mbili kuishia sare tasa.

Mechi za mzunguko wa pili hatua ya makundi kuanza Jumatano ambapo watakaosonga mbele na wale watakaoanza kufunganya virago wakianza kubainika.

 

Categories
Michezo

Samatta apiga bao la tatu Fernabahce

Nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania Ali Mbwana Samatta alifunga bao lake la tatu katika klabu ya Ferbahce ya Uturuki msimu huu huku akichangia ushindi wa magoli 3-1 nyumbani dhidi ya Ankaragucu Jumatatu usiku.

Sammata  alipachika bao hilo kunako dakika ya 34 ya mchezo alipopokea  pasi katika eneo la D na kumhadaa kipa .

Likuwa bao la tatu msimu huu kwa  Samatta msimu huu ,huku ushindi huo ukiichupisha  Fernabahce hadi nafasi ya pili kwenye jedwali kwa alama  38 sawa na Besiktas.

Mshambulizi huyo alijiunga na Ferbahce  Septemba mwaka jana kwa mkataba wa miaka minne  akitokea Aston Villa kwa kima cha Euro miloni 6 na awali alikuwa na Racing Genk ya Ubelgiji alikosakata mechi 121 na kupachika mabao  76 huku akichangia mengine 20.

Categories
Michezo

Simba anguruma na kuweka historia ya kutinga makundi ya ligi ya mabingwa

Klabu ya Simba imeandikisha historia baada ya kusajili wa ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Platinum Fc ya Zimbabwe  na kufuzu hatua ya makundi ya kombe la ligi ya mabingwa Afrika katika mchuano wa marudio uliosakatwa Jumatano jioni katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar.

Difenda Erasto Nyoni aliwanyanyua mashabiki  takriban 30,000 wa wekundu wa msimbazi waliofurika uwanjani   kwa bao la kwanza kupitia mkwaju wa penati wa dakika ya 40  huku wakienda mapumziko kwa uongozi huo.

Kipindi cha pili Mnyama Simba alirejea kwa uchu wa mashambulizi yaliyozalisha goli la pili lililopachikwa kimiani na beki Shomari Kapombe katika dakika ya 61 naye Juma Bocco akapiga bao la tatu dakika ya 91 huku Cletus Chama akifunga karamu kwa bao la nne dakika ya 94.

Simba watakuwa wakipiga hatua ya makundi ya kombe hilo lenye donge nono  kwa mara ya pili na ya kwanza tangu mwaka 2003 ikiwa pia timu ya pekee kutoka Afrika Mashariki kucheza hatua hiyo.

Simba walikuwa wamepoteza duru ya kwanza bao 1-0 ugenini hivyo basi wapiga delji hadi hatua ya makundi kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-1 dhidi ya Platinum.

Categories
Michezo

Simba alenga kurudia Historia na kutinga makundi ya Ligi ya mabingwa

Timu ya Simba Sports  Club ya Tanzania inaazimia kufuzu kwa  hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa Afrika Jumatano jioni   katika uwanja wa Benjamin Mkapa nchini Tanzania itakapowaalika Platinums kutoka Zimbabwe.

Simba walipoteza bao 1-0 kutokana na mkumbo wa kwanza mjini Harare wanahitaji ushindi wa mabao 2-0 ili kuingia hatua ya makundi ya kombe hilo yenye donge nono.

Beki kisiki wa Kenya Joash Onyango ameenza pambano hilo akilenga kupiga soka hatua ya makundi baada  ya kujaribu mara kadhaa biloa mafanikio akiwa na Gor Mahia ya Kenya.

Wekundu wa Msimbazi wanalenga kufuzu kwa hatua ya makundi kwa mara ya pili katika historia yao baada ya kucheza hatua hiyo kwa mara ya kwanza mwaka 2003.

 

 

Categories
Michezo

Tanzania na Djibouti zafuzu nusu fainali ya CECAFA na kunusia kipute cha AFCON U 17

Tanzania na Djibouti zimejikatia tiketi ya nusu fainali kuwania kombe la Cecafa kwa  chipukizi walio chini ya umri wa miaka 17 nchini  Rwanda , baada ya kutoka sare ya baoa 1-1 katika mechi ya mwisho ya kundi B iliyosakatwa Ijumaa alasiri katika uga wa Umuganda mjini Rubavu.

Abdek Mouhoumed,wa Djibouti alijifunga bao la dakika ya 33 na kuwaweka Serengeti Boys uongozini  kabla ya Moktar Djama Ali kukomboa bao hilo zikisalia dakika 10 mechi ikamilike.
Kufuatia matokeo hayo Tanzania ambao walikuwa wamewabana wenyeji Rwanda magoli 3-1 kwenye mchuano wa ufunguzi wameongoza  kundi hilo kwa pointi 4 huku Djibouti iliyotoka sare na wenyeji ikiibuka ya pili kwa alama 2.
Tanzania  itachuana  na timu ya pili kutoka kundi A katika nusu fainali huku Djibouti ikiweka miadi na viongozi wa kundi A katika semi fainali ya pili  Jumapili kabla ya fainali kusakatwa Disemba 22.
Mataifa mawili bora katika hiyo michuano yatafuzu kuwakilisha ukanda huu katika kipute cha AFCON Juni mwaka ujao nchini Moroko.
Categories
Michezo

Viboko wa Uganda waitafuna Tanzania na kunyakua kombe la CECAFA 2020

Timu ya Uganda kwa Chipukizi walio chini ya umri wa miaka 20 maarufu kama Hippos ,ndio mabingwa wa mwaka huu wa kombe la Cecafa  baada ya kuwadhalilisha wenyeji Tanzania mabao 4-1 katika fainali iliyosakatwa Jumatano jioni katika uwanja wa Black Rhino Academy eneo la Karatu mjini Arusha Tanzania.

Richard Basangwa, Steven Sserwadda,  Ivan Bogere na  Kenneth Semakula waliiwajibikia Uganda kwa bao moja kila mmoja ,huku Abdul Suleiman akifunga bao la maliwazo kwa Ngorongoro Heroes kupitia penati.

Viboko hao wa Uganda wangeongoza mabao 3-1 kufikai mapumziko lakini mshmabulizi mwiba Ivan Bogere  akapaishia penati ya dakika ya 45 .

Ilikuwa  mechi ya kulipiza baada ya Tanzania kunyakua kombe la Cecafa mwaka jana ,michuano hiyo ilipoandaliwa nchini Uganda.

Hata Hivyo  timu zote mbili za Uganda na Tanzania zimejikatia tiketi kucheza fainali za Afcon mwaka ujao nchini Mauritania katika mala ya 15.

Kuelekea fainali Uganda iliikomoa Kenya mabao 3-1 katika semi fainali wakati Tanzania wakiwaadhibu Sudan Kusini magoli 2-1 pia katika nusu fainali.

Iilikuwa kombe la 4 la Cecafa kwa uganda tangu mashindano hayo yatangulizwe mwaka 1971,wakiibuka mabingwa miaka ya 1973,2006,2010 na 2020 na kuwa taifa lenye ufanisi mkubwa katika michuano hiyo.

Uganda pia kwa mara ya kwanza wanashikilia vyokombe vyote vya Cecafa kwa wakati mmoja vikiwa nia:-Cecafa kwa wavulana wasiozidi umri wa miaka 15 ,Wasichana walio chini ya umri wa miaka 17,Wavulana walio chuini ya miaka 17 ,wanaume walio chini ya umri wa miaka 20,kombe la Cecafa Kagame linaloshikiliwa na KCCA na kombe la Cecafa senior challenge cup wanaloshikilia Ugand Cranes.

 

 

 

 

Categories
Michezo

Viboko wa Uganda kukabiliana na Ngorongoro Heroes ya Tanzania fainali ya CECAFA

Fainali ya kuwania  kombe la Cecafa kwa vijana  chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 itapigwa Jumatano  alasiri baina ya mabingwa watetezi Tanzania dhidi ya Uganda katika uwanja wa Black Rhino Academy eneo la Karatu mjini Arusha Tanzania.

Wenyeji Tanzania maarufu kama Ngorongoro Heroes  walianza safari ya michuano  hiyo katika kundi A  kwa kuipakata  Djibouti magoli 6-1 ,kabla ya kuimenya Somalia mabao 8-1 katika pambano la mwisho na hatimaye  kuibandua Sudan Kusini bao 1-0 kwenye nusu fainali.

Upande mwingine  Viboko wa Uganda au Hippos walianza kundi B kwa kutoka sare tasa dhidi ya Sudan Kusini kabla ya kuigaragaza  Burundi mabao 6-1 katika mechi ya mwisho na kuitema kenya mabao 3-1 kwenye nusu fainali.

Uganda na Tanzania tayari zimejikatia tiketi kupiga fainali za 15 za kuwania kombe la Afcon mwaka ujao nchini Mauritania kwa kufika fainali.

Tanzania wakipiga fainali ya mwaka jana dhidi ya Kenya

Fainali ya Jumatano  itashuhudia Tanzania wakilenga kuhifadhi ubingwa wa mwaka uliopita wakati Waganda pia wakipania kulipiza kisasi kwa kukosa kunyakua kombe hilo wakiwa nyumbani mwaka uliopita.

Kenya na Sudan Kusini zitamenyana kuanzia saa sita adhuhuri katika mechi ya kuwania nafasi ya tatu na nne katika uwanja wa Black Rhino Academy eneo la Karatu mjini Arusha.

 

 

Categories
Michezo

Tanzania wakwea ndege kupiga kipute cha AFCON mwakani

Mabingwa watetezi wa kombe la Cecafa kwa chipukizi walio chini ta umri wa miaka 20 Tanzania wamefuzu kwa kipute cha Afcon mwaka ujao nchini Mauritania, baada ya kuishinda Sudan kusini bao 1-0 katika nusu fainali ya Cecafa iliyopigwa Jumatatu jioni katika uwanja wa Black Rhino Academy kijini Karatu mji wa Arusha Tanzania.

Baada ya kipindi cha kwanza kumalizika kwa sare tasa timu zote mbili zilirejea kipindi cha pili kwa lengo la kushinda na kutinga michauno ya Afcon mwakani kwa mara ya  kwanza ,huku kosa la mabeki wa Sudan Kusini kunako dakika ya 58 likimpa fursa Kassim Haruna aliyefunga bao kwa wenyeji maarufu kama Ngorongoro Heroes.

Licha ya Sudan kujaribu kila mbinu jitihada zao zilizimwa na kuwapa Tanzania tiketi ya kupiga Afcon mwaka ujao  .

Ngorongoro Heroes watashuka dimbani Black Rhino Jumatano hii kuzindua uhasama wa jadi na Uganda Hippos katika fainali ya kombe hilo walilonyakua mwaka jana nchini Uganda.

Sudan Kusini kwa upande wa pili wa sarafu watapambana  na Kenya Jumatano adhuhuri kuwania nafasi ya tatu na nne.