Categories
Kimataifa

Baadhi ya Maseneta Marekani wadinda kuidhinisha ushindi wa Biden

Kundi la maseneta nchini Marekani limesema kuwa litakataa kutia saini stakabadhi za kuthibitisha ushindi wa Rais Mteule Joe Biden, ikiwa hakutabuniwa tume ya kuchunguza madai ya udanganyifu kwenye uchaguzi huo.

Maseneta 11 na maseneta wateule wakiongozwa na Ted Cruz wanataka ukabidhi wa mamlaka kwa Biden uahirishwe kwa siku 10 ili kuwezesha uchunguzi kufanywa kuhusu madai hayo.

Hata hivyo, huenda hatua hiyo isifanikiwe kwa kuwa maseneta wengi wanatarajiwa kumuidhinisha kwa kura Biden tarehe 6 mwezi huu.

Rais Donald Trump amekataa kwamba alishindwa kwenye uchaguzi wa urais uliopita na kudai kuwa kulifanyika udanganyifu, japo hajathibitisha madai hayo.

Juhudi zake za kufwatilia madai hayo zimekataliwa pakubwa na mahakama.

Hata hivyo, alishinda sehemu ndogo ya madai hayo kutokana na kura zilizopigwa kupitia posta katika Jimbo la Pennysylvnia, ambako Biden alishinda kura nyingi kumliko kwenye uchaguzi huo wa urais wa mwaka jana.

Jopo la maseneta katika majimbo muhimu lilithibitisha ushindi wa Biden kwa alama 306 ikilinganishwa na 232 za Rais Trump.