Nchi ya Tanzania inapoendelea kujitayarisha kwa uchaguzi mkuu wa Jumatano wiki ijayo, mabadiliko yanaendelea kushuhudiwa. Wapiga kura wapatao milioni 29 watapiga kura siku hiyo kuchagua Rais na Wabunge baada ya kukamilika kwa kipindi cha siku 64 cha Kampeini.
Serikali ya Tanzania sasa imeingilia wanaotumia mitandao ya kijamii na simu za rununu. Jana serikali hiyo ya Chama Cha Mapinduzi yaani CCM ilitoa ilani kwa kampuni za mawasiliano ya rununu inayozitaka kusitisha mara moja huduma za kutuma jumbe kwa watu wengi kwa wakati mmoja na za kupiga simu kwa watu wengi kwa wakati mmoja.
Marufuku hiyo ni kati ya tarehe 24 mwezi huu wa Oktoba na tarehe 11 mwezi Novemba mwaka huu wa 2020.
“kwa kuzingatia athari ya utumizi mbaya wa jumbe nyingi kwa pamoja na simu kwa watu wengi kwa wakati mmoja kwa uchaguzi mkuu, na kulingana sheria ya tatu ya ratiba ya pili ya sheria ya mamlaka ya kusimamia mawasiliano nchini Tanzania, mamlaka hii inawaagiza mfunge kwa muda huduma hizo.” ndiyo baadhi ya maneno kwenye barua iliyotumwa kwa kampuni za mawasiliano.
Mkurugenzi mkuu wa mamlaka inayosimamia mawasiliano nchini Tanzania Bwana James Kilara alifafanua kwamba wanaotumia jumbe hizo kwa ajili ya usalama, maswala ya serikali na huduma za fedha wanakubaliwa kuendelea.
Kabla ya hapo kuliibuka tetesi kwamba jumbe zozote fupi ambazo zilikuwa na jina Tundu Lissu au herufi za kuashiria majina ya mgombea huyo wa urais kupitia CHADEMA hazikuwa zinaenda.