Categories
Habari

Rais Kenyatta na Suluhu waahidi kuondoa vikwazo vya kibiashara kati ya Kenya na Tanzania

Rais Uhuru Kenyatta amesema wafanyabiashara wa Tanzania wanaotaka kufanya biashara nchini Kenya hawatahitajika kuwa na visa.

Akiongea kwenye kongamano la kibiashara katika Hoteli ya Serena jijini Nairobi, Rais Kenyatta aliagiza waziri husika kushirikiana na mwenzake wa Tanzania kuondoa vikwazo vya ushirikiano wa kiuchumi kwenye mpaka wa Kenya na Tanzania.

Rais Kenyatta na mwenzake wa Tanzania Samia Suluhu Hassan wameandaa kikao hicho na wafanyibiashara wa Kenya na Tanzania ambapo wameahidi kuondoa vikwazo vya kufanya biashara baina ya nchi hizo mbili.

Naye Rais wa Tanzania Samia Suluhu ametangaza mageuzi kadhaa yatakayotekelezwa na serikali yake ili kurahisisha biashara kati ya mataifa hayo mawili.

Suluhu, aliye ziarani hapa nchini kwa siku ya pili, amewakaribisha nchini kwake wawekezaji kutoka Kenya, huku akisema ziara yake inanuiwa kuimarisha urafiki wa kihistoria na undugu uliopo kati ya watu wa nchi hizi mbili.

Alisema wakati wa utawala wake atajizatiti kuboresha uhusiano wa jadi baina ya Kenya na Tanzania, hususan katika nyanja ya kichumi, huku akikubaliana na Rais Kenyatta kuhusu haja ya kubuni mazingira bora ya ukuaji wa sekta ya kibinafsi ili ichangie kikamilifu istawi wa kiuchumi.

Rais huyo wa Tanzania pia alisema kuwa sababu yake nyingine ya ziara yake ni kujitambulisha. Alisema Kenya ni miongoni mwa mataifa ya kwanza yaliyomtambua kama rais baada ya kuapishwa kufuatia kifo cha mtangulizi wake Hayati John Pombe Magufuli.

Rais Suluhu alitoa shukurani kwa serikali na raia wa Kenya kwa kusimama na Tanzania wakati nchi hiyo ilipopoteza rais wake wa tano.

Alisema uamuzi wa Rais Kenyatta wa kuhudhuria hafla ya mazishi ya kiserikali ya Rais Magufuli ni ishara ya udugu wa kweli, ambao uliashiria upendo kwa nchi ya Tanzania.

Kwa upande wake Rais Uhuru Kenyatta alimhakikishia Rais Suluhu kuwa Kenya itaendelea kushirikiana na Tanzania ili kuafikia ruwaza ya utangamano kikamilifu wa kanda hii kuambatana na matakwa ya waanzilishi wa jumuia ya Afrika Mashariki.

Rais Kenyatta alimshukuru Rais Suluhu kwa kukubali mwaliko wake, akisema hatua hiyo inaashiria haja yake ya kuendelea kuboresha na kuimarisha ujirani mwema.

 

Categories
Habari

Rasi wa Tanzania Samia Suluhu kuzuru Kenya Jumanne

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwasili humu nchini kwa ziara rasmi ya siku mbili kuanzia siku ya Jumanne.

Msemaji wa Ikulu Kanze Dena Mararo amesema kuwa Rais Uhuru Kenyatta atamkaribisha rais huyo wa Tanzania katika Ikulu ya Nairobi.

Mwezi uliopita, Kenya ilimtuma Waziri wa Michezo Amina Mohamed kwenda nchini Tanzania kwa mazungumzo ya kuimarisha uhusiano baina ya mataifa haya mawili.

Rais Suluhu alisema kuwa serikali yake imejitolea kusuluhisha changamoto mbali mbali zilizoko baina ya Tanzania na Kenya.

Wakati wa ziara ya Amina nchini Tanzania, Suluhu aliagiza tume ya pamoja ya kudumu kukutana na kuratibu mipango ambayo inaweza kuimarisha uhusiano baina ya mataifa haya mawili.

Suluhu aliapishwa mwezi February na kuwa rais wa kwanza mwanamke nchini Tanzania kufuatia kifo cha aliyekuwa rais wa taifa hilo Dkt. John Pombe Magufuli.

Ziara ya Suluhu nchini Kenya itakuwa yake ya pili tangu kuapishwa kwake kama rais, baada ya kuzuru taifa la Uganda na kukaribishwa na rais wa huko Yoweri Museveni.

Categories
Burudani

Nazizi afafanua kuhusu ukoo wake

Nazizi Hirji amekuwa kwenye ulingo wa muziki nchini Kenya kwa muda mrefu na sasa ameingilia utangazaji wa redio. Maajuzi aliamua kufafanulia wafuasi wake kwenye mitandao ya kijamii kuhusu ukoo wake na alikotoa jina lake.

Alianza kwa kusema kwamba babake ambaye anaitwa Firoz Hirji ni mtoto wa baba wa asili ya kihindi na mama mtanzania. Babake Firoze ambaye ni babu yake Nazizi ni mzaliwa wa Kolkata nchini India na mamake ambaye ni nyanya ya Nazizi alitoka Mbeya nchini Tanzania.

Kulingana na mwanamuziki huyo, babake aliamua kumpa jina la nyanyake, “Nazizi” ambalo limeundwa kutoka kwa maneno mawili, ‘Na’ na ‘Zizi’.

‘Na’ hutumika kuonyesha ni kifungua mimba huku ‘zizi’ ambalo ni la kiswahili likimaanisha ukumwa wa mzizi yaani ‘root’ kwa kiingereza.

Wengi wa wafuasi wa mwanamuziki huyo wamekuwa wakiamini kwamba “Nazizi” ni jina tu ambalo alijitafutia kwa ajili ya kazi ya muziki ila sasa amefafanua.

Anaridhika kwamba wazazi wake walimchagulia jina la kiafrika wakati ambapo wazazi wengi walipendelea majina ya kizungu.

Mtangazaji huyo wa redio aliaelezea pia kuhusu tamaduni ya ukoo wake ya kina mama kupanua shimo za masikio ambazo hutumika kuvaa hereni au ukipenda vipuli ambayo ameanza kutekeleza maajuzi.

Kitu ambacho wengi wangependa kufahamu sasa ni jinsi familia hiyo ilijipata nchini Kenya.

Categories
Burudani

Idris Sultan aigiza kwenye filamu inayoonyeshwa na Netflix

Muigizaji, mchekeshaji na mtangazaji wa redio wa nchi ya Tanzania Idris Sultan ni mmoja wa waigizaji kwenye filamu iitwayo “Slay” ambayo inapatikana kwenye jukwaa la mitandaoni la Netflix.

Filamu hiyo ya mtayarishi na muigizaji Elvis Chuks wa Nigeria ilianza kuonyeshwa kwenye Netflix rasmi jana tarehe 26 mwezi Aprili mwaka 2021.

Wakati wa kutangaza ujio wa filamu hiyo kupitia mitandao ya kijamii, kampuni ya “Naija on Netflix” ilikosea uraia wa Idris pale ilipomtaja kuwa mkenya jambo ambalo lilisababisha muigizaji huyo ahamasishe watanzania kwenye mitandao ya kijamii kuweka picha za bendera ya Tanzania kwenye tangazo hilo hadi likarekebishwa.

Idris ambaye alishinda shindando la “Big Brother Africa-Hotshots” mwaka 2014 anajivunia kuwa muigizaji wa kwanza wa Tanzania kuwa kwenye filamu ambayo inapatikana kwenye jukwaa la Netflix.

Idris ambaye huvalia nadhifu alishinda pia kwenye tuzo za mitindo ya mavazi za “Abryanz Style and Fashion Awards” zinazoandaliwa nchini Uganda.

Mwaka 2016 alishinda tuzo la mwanahabari anayevalia nadhifu zaidi kitengo cha wanaume na mwaka 2017 akashinda tuzo la mtu maarufu anayevalia nadhifu zaidi katika kitengo cha wanaume vile vile.

Slay ni filamu ambayo inahadithia maisha ya wasichana ambao wanawinda wanaume wa umri mkubwa na wasichana ambao hujionyesha kana kwamba wanatoka kwenye familia tajiri ilhali wanaishi kwa umasikini.

Waigizaji wengine kwenye filamu hiyo ambayo imetayarishiwa nchini Afrika Kusini ni Ramsey Noah na Fabian Lojede wa Nigeria na Amanda Dupont, Dawn Thandeka, Enhle Mbali, Lilian Dube, Trevor Gumbi, Tumi Morake, Leroy Gopal, Joe Kazadi na Kabomo Vilakazi wote wa taifa la Afrika kusini.

Categories
Burudani

Shilole na Rommy wafunga ndoa

Mwanamuziki wa Tanzania Shilole kwa jina halisi Zena Yusuf Mohammed na mpenzi wake Rajab Issa maarufu kama Rommy3d ambaye ni mpiga picha wamefunga ndoa.

Shilole alichapisha picha moja tu ya tukio hilo akisema kwamba wamemaliza salama na kwamba sasa anaweza kuitwa “Mrs Rajab Issa”.

Arusi hiyo haikutangazwa sana ilivyokawaida ya watu maarufu nchini Tanzania na imejiri wakati ambapo waisilamu wakiwemo Shishi na Rommy wanaadhimisha mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Mwezi Januari wakihojiwa na Zamaradi Mketema, wapenzi hao walifichua kwamba wangefunga ndoa kabla ya mwaka huu kufika mwisho lakini arusi imefanyika mapema kuliko matarajio ya wengi.

Rommy3d alimvisha Shilole pete ya uchumba mwisho wa mwaka jana kwenye sherehe ya siku yake ya kuzaliwa baada ya kumvua ya zamani ambapo Shilole alibubujikwa na machozi akisema ameteseka sana.

Baadaye kuliibuka tetesi kwamba Shilole alijinunulia pete hiyo kwani Rommy3d hawezi kumudu bei yake.

Mpiga picha huyo rasmi wa Shilole alisema kwamba alijuana na Shilole kama miaka 11 iliyopita wakati alikuwa muigizaji naye akawa anatumika kama mtu wa kushika taa katika maandalizi ya filamu ambayo Shilole alikuwa anaigiza.

Mwaka 2009 Shilole na Rommy3d walikuwa na uhusiano wa kimapenzi ambao ulidumu kwa muda wa mwaka mmoja. Uhusiano huo ulifika mwisho kutokana na kile wanachokitaja kuwa changamoto za maisha.

Wawili hao wameanza uhusiano wa kimapenzi baada ya Shilole kuachana na Uchebe ambaye alikuwa akimdhulumu ilhali yeye ndiye alikuwa anamtunza.

Rommy3d ni mpiga picha wa kampuni changa ya muziki ya Shilole ambayo alizindua mwaka jana na ina msanii mmoja kwa jina Pablo Chill.

Categories
Kimataifa

Suluhu alionya Bunge la Tanzania dhidi ya kumfananisha na Pombe

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amelitaka bunge la nchi hiyo kukomesha mijadala ya kumlinganisha na mtangulizi wake Marehemu John Pombe Magufuli.

Suluhu amesema ametamaushwa na hatua ya bunge hilo ya kujadili tofauti kati yake na marehemu Magufuli badala ya kuangazia ajenda kuu za serikali.

Rais Suluhu, ambaye amesifiwa kwa ujasiri wake wa kuleta mabadiliko nchini humo, amesema yeye na mtangulizi wake Magufuli walikuwa na malengo sawa na kwamba azma yake ni kuendeleza ruwaza ya marehemu Magufuli.

Alisema kuwa inasikitisha kuwa bunge linashawishiwa na jumbe zinazopachikwa kwenye mitandao ya kijamii na hivyo kuwahimiza wabunge kuzingatia jukumu lao kuu la kujadili na kupitisha bajeti za serikali.

Rais Suluhu alisema hayo kwenye mkutano wa kitaifa ulioandaliwa na viongozi wa kidini kwa ajili ya kumbukizi ya marehemu Magufuli na kuwaomboea viongozi wapya.

Categories
Burudani

Awilo Longomba aingilia uigizaji

Mwanamuziki wa nchi ya Congo Awilo Longomba yuko nchini Tanzania ambako atasalia kwa muda wa mwezi mmoja kwa ajili ya kuigiza kwenye filamu.

Awilo alielezea kwamba aliombwa na kampuni ya BJB films awe kwenye filamu hiyo na akakubali wito. Filamu hiyo inaitwa “A Life To Regret” na ni wazo lake mtayarishaji filamu Billy Jeremiah Brown (BJB).

Billy Jeremiah Brown ni mzaliwa wa Burundi lakini anaishi na kufanya kazi uingereza na kazi ambayo anatayarisha kwa sasa nchini Tanzania huenda ikazinduliwa mwezi Agosti mwaka huu.

Mwanamuziki Awilo Longomba alisema kwamba yuko tayari pia kushirikiana na wanamuziki wa Tanzania ambapo alialika yeyote aliye na wazo la wimbo wa pamoja awasiliane naye.

Mchekeshaji na muigizaji wa nchi ya Zimbabwe mwanadada Mai Titi naye anaigiza kwenye filamu hiyo ya A Life To Regret ambayo ni filamu yake ya kwanza.

Mai Titi mchekeshaji wa Zimbabwe

Mai kwa jina halisi Felistus Murata, ambaye pia ni mwanamuziki alielezea kwamba filamu yao inahusu migogoro kati ya mama wa kambo na mwanawe wa kike wa kambo. Yaani ni mke anaolewa na mume ambaye tayari ana watoto na anawadhulumu watoto hao wa mume wake.

Matayarisho ya kuunda filamu hiyo yalianza mwaka 2018 pale ambapo BJB films ilianza kutafuta watakaoigiza na ndipo Mai TT na Awilo walikutana na wawakilishi wa kampuni hiyo.

Mai naye kama Awilo yuko tayari kushirikiana na wanamuziki wa Tanzania.

Categories
Kimataifa

Suluhu azuru Uganda kwa mwaliko wa Museveni

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amezuru nchi ya Uganda kwa hafla ya makubaliano ya usafirishaji mafuta kutoka nchini Uganda hadi kwenye bandari ya Tanga nchini Tanzania.

Mkataba huo unatarajiwa kufanikisha ujenzi wa bomba la mafuta la urefu wa kilomita 1,440 kutoka eneo la Albertine nchini Uganda hadi kwenye bandari hiyo.

Bomba hilo litakalogharimu dola za Marekani bilioni 3.55 litakuwa ndilo refu zaidi linalotumia umeme ulimwenguni.

Kufikia sasa Uganda imegundua mapipa bilioni 6.5 ya mafuta.

Utiaji saini mkataba huo uliahirishwa mwezi jana kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli.

Categories
Burudani

Nandy atoa video ya kwanza ya nyimbo zake za injili

Mwanamuziki Nandy wa nchi ya Tanzania alitoa nyimbo kadhaa za injili mwanzo wa mwezi wa tatu mwaka huu ambazo zinapatikana kwenye majukwaa kadhaa ya mtandao.

Nyimbo hizo ni, Wanibariki, Umenifaa, Nipo naye, Asante na Noel Song na ndiyo kazi aliyoiachia baada ya ile aliyofanya na mwanamuziki wa Congo Koffi Olomide.

Kwa sasa mwanadada huyo anaonekana kuzamia kazi ya kuundia nyimbo hizo video na mwisho wa msimu wa pasaka yaani Jumatatu Kuu, alichapisha video ya wimbo “Wanibariki”.

Video yenyewe ni kama filamu kwani inaanza ikionyesha Nandy akiwa mdogo na mamake kwenye kibanda chake cha kuuzia chakula wakisaidia mtoto mvulana ambaye alikuwa ameumia usoni na alikuwa na njaa.

Nandy ndiye alitangulia kumwona mvulana huyo akamwonyesha mamake kisha mama akamwita, akaosha kidonda chake na kumpa chakula.

Baadaye mama anaonekana akiwapa watoto hao wawili mafundisho ya Biblia.

Ifikapo katikati, video inaonyesha Nandy ambaye sasa amekuwa mtu mzima akiwa na mamake kwenye kibanda chao cha kupika na kuuza chakula.

Ghafla mama anazirai na kukimbizwa hospitalini ambapo Nandy anapatiwa bili ya laki tatu unusu asijue jinsi ya kuilipa.

Siku moja akiwa ameketi kwenye sehemu ya kusubiria huduma hospitalini akapatiwa risiti na mhudumu mmoja ambayo ilionyesha kwamba ada zote za mamake zilikuwa zimelipwa.

Anapofika chumbani alikolazwa mamake, anampata akizungumza kwa furaha na daktari wake kisha anamwonyesha alama usoni mwa daktari na kumkumbusha kwamba ni yule mvulana walimhudumia awali.

Categories
Kimataifa

Mpango kuapishwa kesho kusaidiana na Suluhu Tanzania

Makamu wa Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, anatarajiwa kuapishwa kesho Jumatano tarehe 31 mwezi Machi, 2021.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, hafla ya kuapishwa kwa Dkt. Mpango itaandaliwa katika Ikulu ya Dododma, mwendo wa saa tisa alasiri.

Mapema leo, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alimpendekeza Mpango, ambaye ndiye Waziri wa Fedha nchini humo, kushikilia wadhifa wa Makamu wake.

Kufuatia pendekezo hilo la Suluhu, jina la Mpango liliwasilishwa kwenye kikao maalum cha Halmashauri ya Kitaifa ya Chama cha Mapinduzi, ambacho ndicho chama tawala nchini humo, kwa kuzingatia matakwa ya katiba ya nchi hiyo.

Baadaye jina hilo likawasilishwa Bungeni na Spika wa Bunge la nchi hiyo Job Ndugaia, ambapo Wabunge walishangilia wakati jina la Mpango lilipotajwa, kabla kuliunga mkono kwa asilimia 100, kwani jumla ya kura zote 363 zilizopigwa zilipitisha uteuzi wake.

Dkt. Mpango alikuwa mmoja wa mawaziri wawili walioteuliwa upya na Hayati Rais John Pombe Joseph Magufuli wakati alipozindua baraza lake jipya la mawaziri kufuatia ushindi wake kwenye uchaguzi uliopita.

Dkt. Philip Mpango atakuwa Makamu wa Rais Samia Suluhu, aliyechukua hatamu za uongozi wa taifa hilo kutokana na kifo cha aliyekuwa Rais John Pombe Magufuli.