Categories
Habari

Wauguzi 69 wafurushwa kutoka nyumba za serikali ya Kaunti ya Taita Taveta

Serikali ya Kaunti ya Taita Taveta imeanza operesheni ya kuwafurusha wauguzi 69 kutoka kwa nyumba za serikali baada ya muda wa kuhama waliopewa kukamilika.

Wauguzi hao ni sehemu ya wahudumu wa afya zaidi ya 400 ambao wamegoma tangu mwezi Desemba mwaka uliopita.

Maafisa wa serikali ya kaunti hiyo wamevamia jengo wanamoishi wauguzi hao na kuanza kuwafurusha pamoja na familia zao.

Kundi la maafisa hao lilikuwa likitembea kutoka nyumba moja hadi nyengine wakiwatoa kwa nguvu wauguzi hao pamoja na vyombo vyao vilivyokuwa ndani.

Wakati wa operesheni hiyo, maafisa hao pia wamehakikisha kwamba nyumba hizo ambazo wauguzi hao walikuwa wakiishi zimefungwa baada ya kuwatoa.

Operesheni sawia na hiyo pia ilikuwa inatekelezwa sambamba katika Kaunti Ndogo za Voi, Mwatate, Wundanyi na Taita.

Huko Voi, wauguzi waliofurushwa walikuwa wanahangaika huku wakitafuta makazi mapya na kuitaja hatua hiyo kuwa ya kinyama.

“Hatukupewa hata ilani ya kutoka. Wamewasili tu na kutufurusha,” akasema mmoja wa waathiriwa hao.

Hata hivyo serikali ya kaunti hiyo, kupitia Waziri wa Afya John Mwakima, imekanusha madai hayo na kusema kwamba walitoa ilani na kuwapa wauguzi hao hadi tarehe 5 Februari watafute makazi kwengine.

Mgomo huo wa wahudumu wa afya ulianza mwishoni mwa mwaka uliopita na kulemaza huduma za afya katika kaunti hiyo.

Huduma za maabara na kutoa ushauri ndizo zinazopatikana baada ya madaktari na wafanyikazi wa maabara kutamatisha mgomo wao kufuatia maelewano na serikali hiyo.

Categories
Habari

Arejea nyumbani na majeraha kutoka ‘ziara ya kishetani’ milimani Taita

Hisia mseto ziliwapata wakazi wa kijiji cha Bungule, eneo la Voi katika Kaunti ya Taita Taveta, pale mwanaume mmoja aliporejea nyumbani baada ya kutoweka kwa siku kadhaa katika hali ya kutatanisha.

Granton Maghanga, mwenye umri wa makamo, aliripotiwa kutoweka mnamo tarehe 27 mwezi uliopita, mwendo wa saa kumi na mbili jioni.

Hali hiyo iliwasababishia hofu jamaa wake pamoja na majirani ambao walianza mara moja operesheni ya kumsaka katika maeneo hatari yenye milima na mabonde lakini juhudi zao zikaambulia patupu.

Wana-Kijiji wakimsaka Granton: Picha kwa hisani ya Jackson Mnyamwezi

Wiki moja baadaye, Maghanga anasemekana kurejea nyumbani mwenyewe akiwa amejeruhiwa miguuni na pia alikuwa amepoteza simu yake ya rununu.

Alipelekwa katika Zahanati ya Mwakwasinyi ambako alitibiwa majeraha hayo.

Baada ya kurudi tena katika fahamu zake za kawaida, Maghanga alisimulia aliyopitia wakati wa kutoweka kwake.

Anasema alitembea mwendo mrefu kutoka nyumbani, hali akiongozwa na sauti ya mtu ambaye hakumuona hadi katika Milima ya Bungule.

Alipofika kilele cha milima hiyo, sauti iliyokuwa ikimuongoza ilimshawishi aingie ndani ya kidimbwi cha maji chenye kina kirefu lakini akakataa.

Baadaye sauti hiyo ilinyamaza na akaanza safari ya kurejea nyumbani japo alikuwa hajui njia ya kumuelekeza.

Alipitia vichakani, kwenye mabonde na mawe na hatimaye kwa bahati nzuri akawasili nyumbani kwake akiwa na uchovu mwingi, usingizi na majeraha.

Hali hiyo iliwalazimu jamaa wake kualika viongozi wa kidini ambao walimfanyia maombi ya kumueka huru ili asipatwe na hali sawia na hiyo.

Kisa hicho kilitokea siku chache tu baada ya mwanaume mwengine wa eneo hilo kutoweka na baadaye mwili wake kupatikana mtoni.

Categories
Habari

Ruto ahimiza umoja kwenye kikao na viongozi wa Taita Taveta

Naibu Rais William Ruto amewataka viongozi kuungana katika juhudi za kusaidi taifa hili kufufua tena uchumi wake baada ya kusambaratishwa na janga la COVID-19.

Ruto ametoa wito huo wakati wa kikao na viongozi kutoka Kaunti ya Taita Taveta, wakiongozwa na Mbunge wa Taveta Naomi Shaban, Jones Mlolwa wa Voi, Lydia Haika wa Taita Taveta, aliyekuwa Gavana John Mruttu na aliyekuwa Mwakilishi wa Wanawake Joyce Lay.

“Lazima tuvunje vizuizi vyote vya kisiasa, tuungane na tuweke mawazo na rasilimali zetu pamoja ili tusaidie katika kuinua maisha ya mamilioni ya Wakenya,” amesema.

Huo ulikuwa mkutano wa pili wa aina hiyo baada ya Naibu Rais kuandaa kikao na viongozi kutoka Kaunti za Uasin Gishu na Trans-Nzoia huko Sugoi mwanzoni mwa wiki hii.

Haya yanajiri huku baadhi ya viongozi wanaomuunga mkono Ruto wakimtetea kufuatia madai kwamba alisajili chama cha kisiasa ambacho ananuia kukitumia kwenye azma yake ya kuwania urais mwaka wa 2022.

Viongozi hao, wakiongozwa na Mbunge wa Soy Caleb Kositany, Gavana wa Nandi Stephen Sang na Mbunge wa Aldai Cornel Serem, wamesema kuwa Ruto ana haki ya kujihusisha na chama chochote cha kisiasa apendacho.

Categories
Habari

Kampeni za chaguzi ndogo za siku ya Jumanne kusitishwa Jumamosi usiku

Wagombea wa nyadhifa mbali mbali za kuchaguliwa wana muda wa hadi Jumamosi usiku kukamilisha kampeini zao kabla ya kufanywa chaguzi ndogo katika maeneo matano humu nchini.

Tume ya mipaka na uchaguzi nchini-IEBC iliratibu shughuli hiyo kuanza tarehe 15 mwezi Oktoba na kumalizika tarehe 12 mwezi Disemba,saa 48 kabla ya shughuli ya upigaji kura kuanza.

Chaguzi hizo zitafanywa kumchagua mbunge mpya wa eneo bunge la Msambweni,wawakilishi wapya wa Wadi za Kahawa Wendani katika kaunti ya Nairobi,Kisumu kaskazini na Lake View kaunti ya Kisumu,Dabaso kaunti ya  Kilifi na Wadi za Wundanyi/Mbale katika kaunti ya Taita Taveta.

Tume hiyo imesema vituo vya kupigia na kuwianisha kura vitafukizwa dawa kabla ya shughuli hiyo kuanza siku ya Jumanne.

Afisa mkuu wa uchaguzi wa Mswambweni Yusuf Abubakar alisema kuwa shughuli ya kutoa mafunzo kwa maafisa 450 watakaohudumu kwenye vituo vya kupigia kura itakamilika Jumamosi.

Alisema shughuli za miezi miwili ya kampeini ziliendeshwa bila vurugu na amewahakikishia wapiga kura 69,003 waliosajiliwa kwamba upigaji kura utafanywa kwa kuzingatia taratibu za wizara ya afya za kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19.

Categories
Habari

Watu watatu wanaswa wakisafirisha kilo 950 za bangi katika barabara ya Nakuru- Nairobi

Maafisa wa upelelezi kutoka kituo cha polisi cha Parklands Jumatano asubuhi waliwakamata washukiwa watatu na kunasa kilo 950 za bangi iliyokuwa ikisafirishwa.

Mifuko hiyo 19 ya bangi ya kilo 50 kila moja ilikuwa imefichwa ndani ya magunia 100 ya mahindi ambayo washukiwa walidai walikuwa wakisafirisha kutoka Uganda hadi Voi kaunti ya Taita Taveta.

Lori walilotumia lenye nambari ya usajili KBZ 406S, lilinaswa katika kituo cha biashara cha Kekopey kwenye barabara kuu ya kutoka Nakuru hadi Nairobi.

Lori hilo lilikuwa na watu watatu, dereva na wanawake wawili wanaoaminika kuwa wenye bangi hiyo.

Afisa mkuu wa polisi katika kituo cha Parklands, David Chebii alisema maafisa wa kitengo cha idara ya upelelezi cha huduma za kukabiliana na uhalifu  wamekusanya sampuli ambazo baadaye zilipelekwa katika maabara ya serikali.

Kitengo hicho chenye makao katika kituo cha polisi cha Parklands kimeimarisha vita dhidi ya bidhaa haramu na zile ghushi kote nchini kufuatia agizo la serikali.

Ripoti ya jopo la BBI inapendekeza kuimarisha usalama wa dawa na chakula ili kuwalinda wakenya dhidi ya vyakula na dawa zenye madhara.

Categories
Habari

Vijana wa ODM huko Pwani waapa kupambana na waasi wa chama hicho

Viongozi wa vijana katika chama cha ODM Ukanda wa Pwani, wamepinga vikali wito wa kuundwa kwa chama cha kisiasa cha Pwani unaotolewa na viongozi wanaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto.

Vijana hao wamesema eneo hilo ni ngome ya ODM na wakaapa kulilinda kutokana na wenye nia ya kulivamia na kugawanya wakazi kisiasa.

Wamesema haya kwenye mkutano na wajumbe wa ODM kutoka eneo zima la Pwani uliofanyika katika Ukumbi wa Arabuko Sokoke Jamii Villas, Kaunti ya Kilifi.

Wamewakashifu wabunge Owen Baya wa Kilifi Kaskazini na Aisha Jumwa wa Malindi kwa kampeni zao za kushinikiza kuundwa kwa chama kipya cha Pwani na pia wakaapa kutwaa ushindi kwenye chaguzi tatu ndogo zijazo katika eneo hilo.

Chaguzi hizo ni ule wa Ubunge wa Msambweni Kaunti ya Kwale na Uwakilishi Wodi za Dabaso na Wundanyi katika Kaunti za Kilifi na Taita Taveta mtawalia, ambazo zimeratibiwa kufanyika tarehe 15 Desemba mwaka huu.

Wamemsihi kinara wa ODM Raila Odinga na naibu wake Ali Hassan Joho watulie na kuwapa nafasi vijana hao wadhihirishe ubabe wao wa kisiasa katika chaguzi hizo tatu ndogo.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari iliyosomwa naye Mwenyekiti wa Vijana wa ODM Kaunti ya Taita Taveta Patricia Mwashighadi, vijana hao wameamua kuwa katika msitari wa mbele kwenye chaguzi hizo.

“Chama cha ODM kimekita mizizi katika eneo la Pwani, kinaazimia kuleta mafanikio kwa wananchi na kimestahimili changamoto za kutetea haki zao,” amesema Mwashighadi katika taarifa hiyo.

Mwashighadi ameongeza kuwa vijana hao wameazimia kuzuru nyanjani kwa zoezi la kusajili wakazi na kuuza sera za chama hicho ili kutimiza ajenda ya demokrasia na maendeleo.

Categories
Habari

Wakazi wa Mwatate kunufaika na mradi wa maji wa shilingi milioni 88.6

Serikali ya kaunti ya Taita-Taveta, imezindua mradi wa maji uiliogharimu shilingi  million 88.6.

Mradi huo wa maji utahudumia zaidi ya wakaazi elfu- 15, wa vijiji kadhaa vilivyoko katika maeneo kame ya kaunti ndogo ya Mwatate.

Mradi huo kwa jina Nyangoro-Mwakitau, ambao ulifadhiliwa kwa pamoja na Hazina ya ustawi wa sekta ya maji (WSTF), na serikali ya kaunti hiyo, utahudumia wakaazi wa maeneo ya Mwashoti, Mwambota, Mwakitau, Godoma, Kwa-Mnengwa na Overseer, ambayo kwa muda mrefu yamekabiliwa na uhaba mkubwa wa maji.

Akizindua rasmi mradi huo, Gavana Granton Samboja alisema umekusudiwa kuhudumia ma-elfu ya wakaazi na pia kuboresha hali yao ya kiuchumi.

Mradi huo ni sehemu ya mpango wa ushirikiano kati ya serikali ya kitaifa na zile za Kaunti katika kutatua tatizo la uhaba wa maji huko Mwatate.

Kwa upande wake afisa mkuu mtendaji wa hazina (WSTF) Ismail Shaiye alihimiza wakaazi kusaidia kulinda mabomba ya maji na aina nyinginezo za miundo msingi dhidi ya wezi ili kuhakikisha wanapata maji ya kutosha bila kutatizwa.

 

Categories
Habari

Raila: BBI italeta maendeleo kote nchini

Kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga amewahimiza wakenya kukubali mpango wa maridhiano ya kitaifa almaarufu Building Bridges Initiative (BBI) akisema utafungua uwezo wa kiuchumi wa taifa hili na kuleta maendeleo.

Waziri huyo Mkuu wa zamani alisema mpango wa BBI unakusudia kuwaunganisha wakenya na utapekela maendeleo katika maeneo yaliyoachwa nyuma kimaendeleo nchini.

“BBI inanuia kuhakikisha kila mmoja ananufaika na maendeleo. Itatokomeza ufisadi na ukabila ambazo zimehujumu maendeleo ya taifa hili,” alisema Raila.

Kwa mujibu wa Raila hatua ya bunge la Senate ya kushindwa kuafikiana kuhusu mfumo wa ugavi wa mapato kwa kaunti  ni miongoni mwa baadhi ya maswala muhimu ambayo yatasuluhishwa na mpango huo wa BBI.

“Bunge la Senate limeshindwa kuafikia mfumo wa ugavi wa mapato kwa kaunti ilhali kiwango hicho ni aslimia 10 ya bajeti yote ya kitaifa. Mpango wa BBi unapendekeza asilimia 35 ya bajeti ya kitaifa kupelekwa kwa kaunti. Hii itasitisha swala la mfumo wa ugavi wa mapato,” alisema kiongozi huyo wa ODM.

Raila aliongeza kuwa serikali inajizatiti kupata pesa zote zilizopatikana kwa njia ya ufisadi na kuzitumia kwa miradi ya maendeleo ya kitaifa

Raila aliyasema hayo Jumatano katika kijiji cha Mwakishimba kilichoko kaunti ndogo ya Wundanyi  wakati wa ziara yake ya siku mbili katika kaunti ya Taita Taveta.

Hii ni ziara ya kwanza ya Raila katika eneo hilo kupigia debe mpango wa maridhiano wa BBI.

Kiongozi huyo wa ODM alikuwa ameandamana na Naibu gavana wa Taita Taveta Majala Mlaghui, mbunge wa Voi Johnes Mlolwa spika wa bunge la kaunti hiyo pamoja na wawakilishi wadi wa eneo hilo.