Categories
Burudani

Professor Jay arejelea muziki

Joseph Haule maarufu kama Professor Jay amerejelea muziki baada ya kugonga mwamba kwenye siasa na uongozi nchini Tanzania.

Jay ambaye ana umri wa miaka 45 sasa ni mmoja wa wanamuziki waanzilishi wa muziki wa kizazi kipya nchini Tanzania. Aliendeleza kazi hiyo ya muziki iliyompa umaarufu hadi mwaka 2015 alipowania kiti cha ubunge katika eneo la Mikumi na kushinda.

Akihudumu kama mbunge kazi ya muziki aliisimamisha kabisa. Mwaka jana kwenye uchaguzi mkuu nchini Tanzania, Professor Jay na wengine wengi wa chama cha “CHADEMA” walibwagwa. Aliyemshinda katika ubunge wa Mikumi ni Dennis Lazaro wa chama cha CCM.

Tangu wakati huo amesalia kimya hadi maajuzi alipojitokeza tena kwenye ulingo wa muziki kupitia kwa mwanamuziki mwenzake Stamina.

Stamina amemshirikisha Jay kwa ngoma yake mpya kwa jina “Baba” ambayo ilizinduliwa rasmi jana tarehe 13 mwezi Januari mwaka 2021.

Professor Jay alitangaza ujio wa kibao hicho kipya kwenye akaunti yake ya Instagram huku akihimiza mashabiki wakakitazame kwenye akaunti ya Stamina ya You tube.

Duru zinaarifu kwamba sasa jay ambaye anaigiza kama babake Stamina kwenye video ya wimbo huo amerejelea muziki kikamilifu.

Stamina anafungua wimbo huo akimpigia babake simu huku akimzomea na kumlaumu kwa matatizo anayopitia maishani.

Anamuuliza ni kwa nini hakumpeleka mamake akaavye mimba yake kwani anasikia aliikataa hiyo mimba.

Analaumu babake pia kwa ufukara anashangaa ni kwa nini wanaishi nyumba ya kupangisha na hamiliki hata shamba.

Anapoingia babake, anamwelezea kwamba vipimo vilionyesha kwamba yeye sio babake mzazi ila aliamua tu kumlea kama baba mzazi na anashangaa ni kwa nini hakusoma ajitengenezee maisha mazuri.

 

Categories
Burudani

Roma Zimbabwe kuacha kazi ya muziki

Mwanamuziki wa nchi ya Tanzania kwa jina Roma Zimbabwe au ukipenda Roma Mkatoliki kwa jina halisi Ibrahim Mussa ametangaza kwamba ataacha kazi ya muziki hivi karibuni.

Kupitia Instagram, Roma alielezea kwamba alitoa wimbo wa kwanza mwaka 2007 na wimbo wake wa mwisho utatoka karibuni.

Aliendelea kwa kushukuru wote ambao wameunga mkono kazi yake kwa muda wa miaka 13 sasa.

Kabla ya hapo, Roma alikuwa ameandika maneno mengi kwenye Instagram kulalamikia kile ambacho anasema ni wanamuziki wenza kuharibu biashara ya sekta ya muziki.

Analalamikia hatua ya wengi wa waandalizi wa tamasha kuandaa tamasha bila kiingilio kwa raia wa nchi hiyo hata kama wanamuziki ambao wanatumbuiza wanalipwa.

Kwenye lalama zake alifichua kwamba wanamuziki walifanya kampeni wakati wa uchaguzi mkuu nchini Tanzania bure. “Kuzoesha mashabiki kwamba wanaweza kuona wanamuziki wengi bila malipo tunaharibu kiwanda.” aliandika Roma.

Roma Zimbabwe huwa anatumia muziki kuendeleza uanaharakati. Mwaka 2018, alitoa kibao kwa jina “Anaitwa Roma” na ndani yake alikuwa amekashifu serikali kwa maovu ambayo yalikuwa yakiendelea katika kilimo cha korosho ambalo ni zao la kipekee ambalo huuzwa nje ya Tanzania.

Waziri wa sanaa na habari wakati huo Harrison Mwakyembe alijibu wimbo huo akisema kwamba Roma hakuwa na vyeti vya masomo ili kumwezesha kukashifu serikali lakini awali Roma alikuwa mwalimu.

Roma alikuwa akifanya kazi na mwanamuziki Stamina na kundi lao lilijulikana kama “Rostam” jina ambalo liliundwa kutokana na majina yao ya kisanii.

Walianza kazi rasmi mwaka 2010 na tangu wakati huo miziki yao ilichukuliwa kama ya kuikashifu serikali ya Tanzania.

Mwanamuziki huyo pia amechapisha video fupi ya wimbo kwa jina “Diaspora” na kuandika

“WIMBO WANGU MPYA NA WA MWISHO, NITAUACHIA MUDA WOWOTE KUANZIA SASA!! ASANTENI KWA KUWA NAMI NA SUPPORT MLIYONIPA KATIKA MIAKA 13 YA CAREER YANGU KWENYE SANAA YA MUZIKI!!”