Categories
Burudani

Redio inayoongozwa na wanawake Afrika Kusini

Mwanamuziki wa muda mrefu nchini Afrika Kusini Yvonne Chaka Chaka alifungua kituo cha redio cha mitandaoni ambacho kinaendeshwa na wanawake.

Stesheni hiyo kwa jina “WOMan Radio” imekuwa wazo la mwanamuziki huyo ambaye pia ni mwigizaji kwa muda mrefu. Mwaka 2016 ndio kwanza alifikiria hilo lakini akaliweka kando kidogo kwani anasema data ya kuingia kwenye mitandao ya kijamii ni ghali nchini Afrika kusini.

Yvonne akiwa mbele ya bango la Kituo chake cha Redio

Anasema alitiwa moyo na waziri wa mawasiliano nchini Afrika Kusini Bi. Stella Thembisile ambaye alimkumbusha kwamba yeye ana ufuasi hata nje ya Afrika kusini.

Yvonne anasema alichochewa sana na hitaji la kuwapa kina dada uwezo na wakiwa wanaweza kujisimamia itakuwa rahisi pia kwa wanaume kuhusiana nao.

Kulingana naye kituo hicho kinatoa nafasi kwa kina dada kusimulia hadithi zao ili kuwatia moyo wanawake wengine, kuwapa ushauri, mafunzo na hata mawazo ya biashara.

Mwimbaji huyo wa wimbo “Umqombothi” anasema kuna wanawake ambao wanadhulumiwa kwenye ndoa au mahusiano na hawajui na kituo hicho kitawafungua macho watu kama hao.

Alifafanua kwamba kituo hicho ambacho kilianza rasmi mwezi Oktoba hakikuundwa kwa sababu ya kudhalilisha wanaume.

Kitahusisha pia wanawake kutoka nchi mbali mbali barani Afrika na alitaja nchi kama vile Kenya na Uganda ila kwa sasa watangazaji wote ni raia wa Afrika Kusini.

Categories
Burudani

Zari Hassan asuta kakake Diamond

Mwanamitindo Zari Hassan, mzaliwa wa Uganda anayeishi na kufanya biashara nchini Afrika kusini amegadhabishwa na matamshi ya kaka wa kambo wa Diamond Platinumz kwa jina Ricardo Momo. 

Ricardo alihojiwa na hapo ndipo alimwaga mtama kuhusu mahusiano ya Zari na Diamond Platinumz. Kulingana naye, Zari ndiye alianza kumnyemelea Diamond kwa kutaka kufurahia mali yake na umaarufu. 

Lakini Zari anakana hayo akisema kwamba Ricardo anafaa kufanya utafiti kabla ya kusema mambo kwani sio ukweli anaonelea kuwa kaka huyo wa Diamond anatafuta ufuasi kwenye mitandao ya kijamii kwa kutumia jina lake. 

Hata hivyo Zari amekiri kwamba yeye ndiye kwanza alimpigia Diamond simu akitaka huduma zake kama mwanamuziki kwenye sherehe ambayo alikuwa ameandaa, Diamond akamwelekeza kwa meneja wake na ikatokea kwamba hangeweza kuhudhuria na kutumbuiza kwenye sherehe ya Zari kwani alikuwa na kazi kipindi hicho chote.

Baada ya hapo, Zari anasema walikutana tena kwenye ndege wakisafiri na hapo ndipo walibadilishana nambari za simu na Diamond akawa ndiye mwenye kuwasiliana na Zari kwa sana kwa kutuma jumbe kila mara. Mwanadada huyo anasema alikuwa na pesa hata kabla ya kukutana na Diamond. 

Zari na Diamond walikuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi ambao una matunda ambayo ni watoto wawili, wa kike Tiffah na wa kiume Nillan.

Walitengana baada ya kile kinachosemekana kuwa uzinzi kwa upande wa Diamond.

Alipohojiwa yapata mwaka mmoja uliopita, Diamond alikiri kwamba yeye ndiye alikuwa na makosa mengi kwenye uhusiano wake na Zari.

Zari pia anakoseshwa kwa kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na Peter Okoye mwanamuziki wa Nigeria na mwalimu wake wa mazoezi wakati akiwa kwenye uhusiano na Diamond.

Categories
Burudani

Shindano la muziki la “Old Mutual amazing Voices”

Awamu ya pili ya shindano la ‘Old Mutual Amazing Voices’ imeanza na kwa sasa makundi ya muziki yanahitajika kuwasilisha video zao kwa uteuzi kwenye jukwaa lililoko kwenye tovuti ya shindano.

Mwaka huu mambo ni tofauti kidogo kutokana na janga la virusi vya Corona ulimwenguni kote. Mwaka jana makundi yalijitokeza mbele ya majaji ambapo waliteua makundi 12 kuingia kwa shindano hilo.

Shindano hilo huwa la vipindi kumi na vitatu vya runinga na linahusu makundi ambayo hayajakiandikisha na kampuni yoyote ya kusimamia wanamuziki kutoka nchi za Afrika.

Ghana, Kenya, Zimbabwe na Afrika Kusini zilimenyana mwaka jana ambapo kundi la Kenya kwa jina ‘Wanavokali’ liliibuka mshindi na kutia kibindoni dola laki moja za kimarekani ambazo ni sawa na shilingi milioni kumi za Kenya.

Waimbaji kwenye kundi hilo ni Ythera, Riki Msanii, Chepkorir, Lena Gayah, Rui na Mellah.

Mwaka huu nchi ya Ghana imeongezeka kwenye orodha ya zile ambazo ziko mbioni kushinda dola hizo laki moja.

Makundi yanahitajika kuingia kwenye ukaguzi wa uteuzi kupitia kutuma video zinazoonyesha uwezo wao kwa kuimba na kutumbuiza. Zoezi la ukaguzi lilianza tarehe ishirini na nane mwezi Oktoba mwaka huu na litaendelea hadi tarehe 26 mwezi Novemba mwaka huu wa 2020.

Shindano linahusu aina tatu za muziki ambazo ni muziki wa injili, muziki wa pop na mtindo wa R&B.