Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi Benson Mutura ameapishwa kuwa Kaimu Gavana wa kaunti hiyo.
Mutura amechukua nafasi ya Mike Sonko ambaye aliondolewa mamlakani kwa misingi ya kutumia vibaya mamlaka na kukiuka katiba.
Mbunge huyo wa zamani wa Makadara atahudumu kwa siku sitini kabla ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC, kuandaa uchaguzi mdogo wa kumchagua gavana mpya.
Shughuli ya kuapishwa kwake imeongozwa na Jaji Jairus Ngaah katika Makao Makuu ya kaunti hiyo.
Katika hotuba yake baada ya kuapishwa, Mutura amesema kuwa atafanya kila juhudi kulainisha maswala mbalimbali katika kaunti ya Nairobi na kudhihirisha uongozi ambao umekuwa ukikosekana tangu uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2017.
Mutura amesema kuwa anachukua usukani katika kaunti ambayo haina pesa kutokana na utata kuhusiana na kupitishwa kwa bajeti, huku akiongeza kuwa hakuna pesa za kulipa mishahara na bima ya matibabu.
Ametoa wito kwa maafisa wakuu katika kaunti hiyo kumsaidia anapojaribu kurekebisha maswala mbali mbali katika kaunti hiyo kwa siku sitini ambazo amepewa kuhudumu katika wadhifa wa Kaimu Gavana.