Categories
Burudani

Shishi Gang

Mwanamuziki wa nchi ya Tanzania Shilole ambaye pia ni mjasiriamali anaonekana kuendelea vizuri katika kazi yake. Juzi, punde baada ya tangazo la mwanamuziki mwenza Diamond Platnumz, Shishi naye alisema kwamba ana tangazo maalum ambalo angelitoa kwenye kikao na wanahabari jana Alhamisi, tarehe 26 mwezi Novemba mwaka huu wa 2020 saa kumi na moja jioni.

Muda ulipowadia, Shishi ambaye jina lake halisi ni “Zena Yussuf Mohamed”, alipasua mbarika. Alizindua rasmi kampuni yake kwa jina “Shishi Gang”. Kulingana naye, kampuni yake itahusika na mambo mengi sio tu usimamizi wa wanamuziki.

Jina la kampuni yake linakaribia kufanana na la kampuni ya Harmonize, “Konde Gang” ambayo alianzisha baada ya kugura “Wasafi Classic Baby, WCB” yake Diamond Platnumz.

Alisema kwamba ataandikisha wasanii wa aina mbali mbali hata wachoraji na waigizaji na kampuni hiyo pia huenda ikahusika na uuzaji magari, mashamba na vitu vingine.

Shishi ambaye anamiliki mkahawa kwa jina “Shishi Food” aliwavunja mbavu waliohudhuria kikao chake na wanahabari kutokana na kiingereza chake.

Katika kikao hicho pia, alimtambulisha msanii wa kwanza kwa jina la Instagram, @ronze_officiall au Ronze tu.

Ronze amerekodi na kuzindua vibao kadhaa kulingana na akaunti yake ya Youtube na cha hivi punde zaidi kinaitwa “Chereko”.

Shilole aliomba mashabiki wampokee kijana huyo walivyompokea yeye katika ulingo wa muziki. Shishi ni mmoja kati ya wanamuziki ambao hawako chini ya kampuni ya WCB lakini wamealikwa na Diamond kwenye ziara ya Wasafi Media.

Maajuzi Shishi alitembelewa na mwanamuziki wa Congo Koffi Olomide katika mkahawa wake, na mwisho wa siku, Le Grand Mopao alisifia chakula chake.