Categories
Burudani

Agnes amkana Uchebe!

Muda mfupi baada ya Shilole na Uchebe kutengana mwaka jana, Uchebe alijitokeza kutangaza kwamba ashajipatia mpenzi mpya kwa jina Agnes Suleiman ambaye ni muigizaji na mwanabiashara.

Uchebe na Agnes waliweka picha na video kwenye mitandao ya kijamii ambazo zilionyesha jinsi walikuwa wanapendana swala ambalo wengi walitilia shaka.

Oktoba 24 mwaka 2020, Agnes na Uchebe walihojiwa kwenye kipindi cha Mashamsham cha kituo cha redio cha Wasafi Fm ambapo walisema kwamba wanapendana. Agnes aliulizwa ni kwa nini alikubali kuingia kwa mahusiano na mwanaume ambaye ashasemekana kwamba alikuwa akimpiga mke wake wa awali akasema kwamba sio ukweli, uchebe sio mpenda vita.

Agnes na Uchebe kwenye studio za Wasafi Media

Waliulizwa pia ikiwa ni uhusiano walibuni tu kwa ajili ya kujipatia umaarufu na wakakana na Agnes akammiminia sifa Uchebe kwamba ni mtu anayempenda na kumjali.

Alisimulia kwamba walikutana kwa mara ya kwanza na Uchebe ambaye ni fundi gari wakati alipeleka gari lake likatengenezwe na Uchebe akampokea vyema na kumpa huduma nzuri na mapenzi yakaota.

Kulingana na simulizi yake wakati huo kwenye Wasafi Fm, Uchebe alimpa gari lake akaenda nalo nyumbani akabaki na lake akilitengeneza na baadaye akampelekea nyumbani kwake.

Sasa mwanadada huyo Agnes amejitokeza kusema kwamba uhusiano wake na Uchebe ni kitu ambacho kilipangwa tu. Akihojiwa na Dizzim Online, mwanadada huyo alisema kwamba Uchebe alimwomba waigize ili kumkera Shilole aliyekuwa mke wa Uchebe.

Agnes anasema Uchebe alivunjika moyo sana baada ya kuachwa na Shishi Baby na ndio maana akaamua kujionyesha kama ambaye yuko sawa ila hakuwa sawa.

Alisongwa na mawazo kiasi cha kutoweza kuendelea na kazi yake ya gereji kwa muda.

Kulingana naye, kuonekana kwake hadharani na Uchebe, kumemharibia jina na wengi wanaamini ameshapita naye lakini anasema anataka watanzania wajue kwamba hakuwahi kuwa na uhusiano halisi wa mapenzi na Uchebe.

Categories
Burudani

Shilole afurahia matokeo mazuri ya binti yake

Kila mzazi huridhika mtoto wake anapofanya vizuri kwenye mitihani shuleni kwani huwa wanawekeza hela nyingi katika elimu yao na mwanamuziki na mjasiriamali wa Tanzania Zena Yusuf Mohamed maarufu kama Shilole anapitia kipindi hicho.

Matokeo ya mtihani wa kidato cha nne yalitangazwa maajuzi nchini Tanzania na jana Shishi Baby alikuwa mwingi wa furaha huku akimsherehekea binti yake mkubwa.

Msichana huyo kwa jina Joyce, alipata Division 1 ya alama 16 na Shilole anasema kupitia Instagram kwamba aliambiwa kwamba hivyo binti yake amepita.

Anaanza kwa kumshukuru Mungu na kuelezea furaha yake kisha anelezea jinsi hakupata nafasi ya kusoma na akaapa kuelekeza juhudi kwa binti zake ili wawe yule mwanamke ambaye alitazamia kuwa awali lakini hakuweza.

Anasema pia kwamba kuzaliwa na malezi ya mwanake Joyce yalikuwa magumu ila sasa mambo yamebadilika.

Shishi ambaye anamiliki mkahawa kwa jina “Shishi Foods” anakumbuka pia wanafunzi, waalimu na wafanyikazi katika shule ya mtakatifu Christina huko tanga alikokuwa akisoma binti yake.

Aliowakumbuka pia ni wateja wa Shishi food na mashabiki wake wa muziki.

Baadaye pia alisherehekea matokeo ya binti yake wa pili ya kidato cha pili. Rahma naye alipata Division 1 ya alama 12. Shilole anaonelea kwamba angepata nafasi ya kusoma angekuwa anapita kama binti zake hivi sasa.

Categories
Burudani

Shishi Baby Vs Vanessa Mdee

Mwanamuziki wa Tanzania Shilole au ukipenda Shishi Baby amelinganisha hafla yake ya kuvishwa pete ya uchumba na ile ya mwanamuziki mwenza Vanessa Mdee huku akicheka.

Kwenye akaunti yake ya Instagram, mmiliki huyo wa Shishi Foods aliweka video ya hafla yake na ile ya Vanessa Mdee na akaandika, “Kweli mpaka muda huu nimeangalia video hii nimecheka mbavu sina!! Hivi mbona nilianguka vile? By the way Happy New Year.”

Vanessa na mchumba wake Rotiki wanaonekana wenye raha wanacheka wakikumbatiana huku Vanessa akionyesha pete aliyovishwa kwa waliohidhuria hafla ya kuchumbiwa.

Kwa upande mwingine Shishi anaonekana akiishiwa nguvu, kuanguka na kuketi chini mpenzi wake Rommy 3D asiweze kumuinua anasalia tu kumpanguza machozi.

Vanessa Mdee ambaye awali alikuwa anaonekana kutovutiwa na ndoa, alibadili mawazo siku chache baada ya kukutana na Rotimi mwanamuziki na muigizaji nchini Marekani. Aliamua kuacha muziki kugura Tanzania na kuenda kuishi na mpenzi wake huko Atlanta nchini Marekani.

Vanessa na Rotimi

Uchumba wa Shilole na mpiga picha Rommy 3d umekuwa ukitiliwa shaka na wengi wa mashabiki wake nchini Tanzania kwa kile kinachosemekana kuwa hatua ya kulazimisha na kwamba Shilole alijinunulia pete hiyo.

Shilole na Rommy 3d

Hata hivyo Shilole amekana madai hayo akisema ni penzi la zamani amerudia na kwamba wanapendana sana.

Uchumba huu wao ulijiri miezi michache baada ya Shilole kuacha ndoa yake na fundi wa magari Uchebe kwa madai kwamba alikuwa akimdhulumu ilhali yeye ndiye alikuwa akitafutia familia.

Mwaka huu mpya wa 2021 wanamuziki hao wa Tanzania Shilole na Vanessa Mdee wanatazamiwa kufunga ndoa na wapenzi wao.

Categories
Burudani

Happy Birthday Shihi Baby!

Leo ni siku ya kuzaliwa ya mwanamuziki wa Tanzania Shilole au ukipenda Shishi Baby. Kupitia Instagram, Shishi ambaye pia ni mjasiriamali alishukuru kwa mwaka 2020 hata kama umekuwa wa changamoto nyingi.

Alikumbusha umma kwamba mwaka huu alionja joto la jiwe la ndoa lakini pia ni mwaka ambao pia ameonja tamu ya mapenzi.

Kulingana naye biashara zake zimeendelea kukua licha ya magumu ya mwaka huu ambapo alishukuru wateja wake wote na wanaopenda muziki wake.

Hakuisahau serikali ya muungano wa Tanzania ambayo alisema inatoa mazingira bora kwa wafanyibiashara.

Alishukuru Mungu kwa Binti zake wawili Joyce na Rahma ambao anasema wameendelea kumpa furaha hata wakati anapitia magumu huku akiwakumbuka wote wanaomzunguka, ndugu, jamaa na marafiki.

Shilole alimalizia kuwaalika wote kwenye mkahawa wake kwa jina Shishi Food kuanzia saa moja jioni ambako inaonekana ataandaa sherehe na kuzungumza na wanahabari.

Mwanamuziki huyu amezindua kibao kipya hii leo kwa jina “My Photo” ambacho amemhusisha Baba Levo ambaye ni mwanamuziki na mtangazaji wa Wasafi Fm.

Kulingana naye wimbo huo ni wa kusimulia magumu ya ndoa aliyoyapitia. Baba Levo anaimba,” Welcome bwana Shem (shemeji), tunakukubali sana bwana shem, usimpige sister Bwana Shem, wewe mpige picha bwana shem …”

Inaonekana kwamba wimbo huo pia ni wa kumsifia mpenzi wa sasa wa Shilole ambaye yeye humrejelea kama mpiga picha wake.

Categories
Burudani

Shishi Baby aomba ukuu wa Wilaya

Mwanamuziki na mjasiriamali wa nchi ya Tanzania Zena Yusuf Mohamed maarufu kama Shilole au ukipenda Shishi Baby ametoa ombi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli.

Wakenya wanamfahamu dada huyo kutokana na video iliyosambazwa awali kwenye mitandao ya kijamii ambapo alishindwa kutamka neno, “Subscribe”.

Mwanadada huyo ambaye anamiliki mkahawa kwa jina Shishi Food anasema anatamani sana kuwa mbunge lakini kwa sasa anaomba Rais ampe ukuu wa wilaya.

Amewahi kuwa mwenyeji wa watu mashuhuri kwenye mkahawa huo wake, wa hivi punde zaidi akiwa mwanamuziki tajika wa Congo, Koffi Olomide.

Shishi anakubali kwamba hana kisomo, aliachia darasa la saba, lakini ana kipaji cha uongozi na ikiwa Rais ataona vyema ampatie kazi hiyo ya kusimamia wilaya.

Mwanamuziki huyo alitaja Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Bi. Jokate Urban Mwegelo wa miaka 33 ambaye awali alikuwa mtangazaji na mfanyibiashara akisema ikiwa atapatiwa kazi ataifanya kama anavyoifanya Jokate kwa kujitolea.

Siku za hivi karibuni Shilole amekuwa akijitahidi sana kujitafutia yeye na binti zake pale ambapo amekuwa akitangazia kampuni kadhaa biashara zao na inaaminika kampuni hizo zinamlipa vizuri.

Amekuwa pia akihusishwa kwenye tamasha linaloendeshwa na wasafi media ya Diamond Platnumz almaarufu “Tumewasha na Tigo”.

Alijihusisha pia kikamilifu na kampeni za chama cha CCM kabla ya uchaguzi mkuu na sasa inasubiriwa kuona ikiwa Rais Magufuli ataridhia ombi lake.

Categories
Burudani

Shishi Gang

Mwanamuziki wa nchi ya Tanzania Shilole ambaye pia ni mjasiriamali anaonekana kuendelea vizuri katika kazi yake. Juzi, punde baada ya tangazo la mwanamuziki mwenza Diamond Platnumz, Shishi naye alisema kwamba ana tangazo maalum ambalo angelitoa kwenye kikao na wanahabari jana Alhamisi, tarehe 26 mwezi Novemba mwaka huu wa 2020 saa kumi na moja jioni.

Muda ulipowadia, Shishi ambaye jina lake halisi ni “Zena Yussuf Mohamed”, alipasua mbarika. Alizindua rasmi kampuni yake kwa jina “Shishi Gang”. Kulingana naye, kampuni yake itahusika na mambo mengi sio tu usimamizi wa wanamuziki.

Jina la kampuni yake linakaribia kufanana na la kampuni ya Harmonize, “Konde Gang” ambayo alianzisha baada ya kugura “Wasafi Classic Baby, WCB” yake Diamond Platnumz.

Alisema kwamba ataandikisha wasanii wa aina mbali mbali hata wachoraji na waigizaji na kampuni hiyo pia huenda ikahusika na uuzaji magari, mashamba na vitu vingine.

Shishi ambaye anamiliki mkahawa kwa jina “Shishi Food” aliwavunja mbavu waliohudhuria kikao chake na wanahabari kutokana na kiingereza chake.

Katika kikao hicho pia, alimtambulisha msanii wa kwanza kwa jina la Instagram, @ronze_officiall au Ronze tu.

Ronze amerekodi na kuzindua vibao kadhaa kulingana na akaunti yake ya Youtube na cha hivi punde zaidi kinaitwa “Chereko”.

Shilole aliomba mashabiki wampokee kijana huyo walivyompokea yeye katika ulingo wa muziki. Shishi ni mmoja kati ya wanamuziki ambao hawako chini ya kampuni ya WCB lakini wamealikwa na Diamond kwenye ziara ya Wasafi Media.

Maajuzi Shishi alitembelewa na mwanamuziki wa Congo Koffi Olomide katika mkahawa wake, na mwisho wa siku, Le Grand Mopao alisifia chakula chake.

Categories
Burudani

Shishi baby amlenga Uchebe kwenye wimbo

Mwanamuziki wa Tanzania kwa jina Shilole au ukipenda Shishi Baby maajuzi alizindua kibao kinachojulikana kama ‘Akutake nani’ ambapo ameshirikishwa na mwanamuziki Mzee wa Bwax.

Bwax ndio anaanza wimbo huo ambapo maneno yake yanaonekana kumsuta mwanadada ambaye sasa anaonekana kupoteza thamani yake. Anamtaja Shilole, Amber Lulu na hata mwanamuziki mwingine kwa jina Gigy Money kati ya wengine.

Anamwambia kwamba mafuta anayojipaka kwa nia ya kujichubua yamemkataa. Anatumia maneno kama “Wewe dada sura mpya mwili wa zamani, akutake nani?”.

Anapoingia na sehemu yake Shilole anaimba, ” Pochi kubwa hauna hela we kaka akutake nani? Ushazoea ki – ben 10 kuwekwa ndani wewe akutake nani. Mademu wote wamekukimbia akutake nani? Unajiita brother man hatukuoni kwenye Facebook, unajiita sharobaro hatukuoni whatsapp …”

Shishi na Bwax wanajibizana kwenye wimbo huo lakini wanaofahamu matukio kwenye maisha ya Shilole wanasema kwamba anamlenga aliyekuwa mume wake Uchebe.

Uchebe ni fundi wa magari ambaye wengi wanaamini mapato yake ni ya chini na kwamba ni Shishi aliyekuwa aligharamia maisha ya hali ya juu aliyokuwa akiishi wakiwa pamoja.

Shishi alimwacha Uchebe kwa kile ambacho alikitaja kuwa dhulma za kijinsia na ni baada ya picha zake kutoka zikionyesha akiwa na makovu kwenye uso.

Alipohojiwa Shishi alidhibitisha kuachana na Uchebe akisema kwamba bwana huyo alikuwa anampiga kiholela hata bila makosa.

Categories
Burudani

Amini wazo lako!!! Ushauri wa Shishi

Siku chache baada ya kutangaza kwamba angependa kuandika kitabu, Shishi mwanamuziki, muigizaji na mjasirismali nchini Tanzania ameibuka na ushauri.

Kwenye akaunti yake ya Instagram, Bi. Zuwena Muhamed au Shilole aliweka picha yake nzuri na maneno ya ushauri kwa mashabiki wake.

“Siku zote amini katika Wazo lako, Wazo lolote likitekezwa linageuka kuwa Fursa, Fursa Yeyote ikitumika vyema inageuka kuwa Mtaji, Mtaji wowote ukitumika vyema unageuka kuwa utajiri !! Siku ya Kwanza Kuwaza Kuwa Muimbaji nilipingwa sana lakini leo Hii nimekuwa Shishi sababu nilisimama na wazo langu, Nilipotaka Kuanzisha Shishi Food kuna walioliona kuwa ni wazo Dogo ama Brand yangu Haifanani na kuwa Mama Ntilie lakini Nilisimama na Wazo langu… Leo Hii Shishi Food imeajiri watu, Inahudumia Watu na Imeniongezea Kipato kwa Kiasi kikubwa sana!! Anza kuamini katika Wazo lako”

Shilole aliachana na mume wake Uchebe maajuzi baada ya kile alichokitaja kuwa dhulma. Akitangaza kuachana na mume wake Shilole aliachia picha zikimwonyesha akiwa na makovu usoni.

Tangu wakati huo Shishi anaonekana kujigundua na lengo ni kujiendeleza maishani. Yeye ni kati ya wasanii wengi nchini Tanzania ambao wanakipigia debe chama cha CCM kwenye kampeni zinazoendelea za uchaguzi mkuu.

Uchebe hakusema lolote kuhusu swala hilo na ameonekana kuwa karibu sana na mwanamuziki Diamond Platinumz isijulikane Wana mipango gani.

Categories
Burudani

Nitaandika kitabu, Shilole

Mwanamuziki wa Tanzania ambaye pia ni mjasiriamali na muigizaji Shilole au ukipenda Shishi amedokeza kwamba anapanga kuandika kitabu kuhadithia maisha yake.

Kupitia akaunti yake ya Intagram Shilole ameandika,

“Nafikiria kuandika kitabu, Nafikiria kuacha alama, Nafikiria kuelezea mapiti na magumu yaliyonijenga leo hii kuwa Shishi!! Haikuwa rahisi hata kidogo lakini pia hanuna gumu unapoamua kutokata tamaa, kuweka juhudi, kumweka Mungu Mbele na kukimbiza ndoto zako.”

Ama kweli Shilole ameyapitia! Jina lake halisi ni ” Zena Yusuf Mohammed” na Shilole au Shishi ni la muziki na biashara.

Shishi anamiliki kampuni kwa jina “Shishi foods” ambayo hujishighulisha na kupika na kuuza vyakula.

Tarehe nane mwezi Julai mwaka huu Shishi aliachia picha kwenye Instagram akiwa na makovu usoni na kufunguka kwamba aliyekuwa mume wake kwa jina “Uchebe” alikuwa akimchapa.

Baada ya hapo Shishi alitangaza kwamba wameachana na Uchebe ambaye anasema alikuwa na wivu kupita kiasi.

Shishi na Uchebe

Kwamba hakuwa anataka Shishi awe katika eneo ambalo atahusiana na watu sana sana wanaume na kazi yake kama msanii inalazimu iwe hivyo.

Alizaliwa tarehe 20 mwezi Disemba mwaka 1987 akalelewa na mamake pekee hakuwahi kujua babake. Mamake aliaga Shilole akiwa mdogo na kapitia mengi ikiwemo kukosa elimu na kuolewa mapema.

Anajivunia kuwa msanii wa kike wa kwanza nchini Tanzania kufikisha wafuasi milioni moja kwenye mtandao wa Instagram. Shilole aliwavunja wengi mbavu wakati alianza kujiita Shishi Trump akidai kwamba Rais wa marekani ni babake mlezi na walikuwa wakizungumza mara kwa mara kwa simu.

Wakati mmoja Shilole alitembea Kenya ambapo aliitwa kwa kipindi cha vichekesho cha mchekeshaji kwa jina “Chipukizi’ ikabainika kwamba hakielewi kiingereza vizuri ila anajikaza.

Video yake nyingine ambayo ilisambazwa sana ni ile ambayo anashindwa kutamka neno”Subscribe” kwa nia ya kualika mashabiki kwenye channel yake ya youtube.