Maseneta sasa wanataka kamati maalum kuhusu maswala ya usalama wa taifa, ulinzi na uhusiano wa kimataifa, kuchunguza kwa haraka madai ya utoaji wa hongo katika shughuli inayoendelea ya kuwasajili makurutu kujiunga na Vikosi vya Ulinzi nchini (KDF).
Kwenye taarifa iliyowasilishwa mbele ya Bunge la Senate na Seneta wa Kaunti ya Narok Ledama Ole Kina, maseneta hao wanadai kuwa baadhi ya maafisa wanaosimamia shughuli hiyo ya usajili wameigeuza kuwa biashara.
Maseneta hao wameitaja hali hiyo kuwa tisho kwa usalama wa taifa, na matumizi mabaya ya rasilimali za kitaifa.
Maseneta walidai kuwa maafisa hao wa usajili wanaitisha pesa nyingi za hadi shilingi laki saba, ili kuwasajili wahusika.
Wametoa wito wa kudumishwa kwa uwazi na uadilifu katika shughuli hiyo ya usajili, na hatua kali kuchukuliwa dhidi ya maafisa wafisadi wa usajili.
Wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo tarehe 8 mwezi huu katika Makao Makuu ya Idara ya Ulinzi jijini Nairobi, Naibu Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi Luteni Jenerali Levi Mghalu alitoa hakikisho kuwa usajili huo utakuwa wa huru na haki.
Mghalu alitoa wito kwa Wakenya kuepukana na matapeli wanaoitisha pesa kwa kudai kuwa na ushawishi katika mchakato huo.
“Wakenya wanakumbushwa kwamba kutoa hongo au vitendo vyengine vya ufisadi ni kinyume cha sheri. Yeyote atakayepatikana akitoa hongo ili apate nafasi kwenye zoezi hili la usajili atajilaumu mwenyewe. Nia yetu ni kuandaa zoezi la usajili lililo huru na haki,” alionya Mghalu.
Kumekuwa na malalamishi kutoka kwa umma kwamba zoezi hilo, linalotarajiwa kutamatika kesho Ijumaa tarehe 19 Februari, halifanyiki kwa njia huru, huku Wakenya wengi wakipoteza maelfu ya pesa kwa watu wanaodai kuwa na uwezo wa kushawishi matokeo ya usajili huo.