Shirikisho la kandanda nchini FKF limepatwa na pigo baada ya mahakama ya kutatua migogoro michezoni nchini SDT kuamuru kurejeshwa ligini timu za Mathare United na Zoo Fc kusubiri uamuzi wa kesi iliyowasilishwa dhidi ya FKF na vialbu hivyo viwili wiki ijayo.
Mwenyekiti wa Mahakama hiyo maarufu kama SDT John Ohaga ametoa uamuzi huo mapema Alhamisi wa kuzirejesha timu hizo mbili kwenye ligi pamoja na kubatilisha uamuzi wa awali wa FKF wa kutamatisha kandarasi za wachezaji wote wa klabu hizo mbili .
Pia jaji Ohaga ameagiza Fkf iliruhusu wachezaji na maafisa wa vilabu hivyo kufanyiwa vipimo vya COVID 19 sawa na vilabu vingine saa 72 kabla ya kuanza mechi zao za ligi kuu .
Baraza kuu la FKF likikutana Desemba 9 na kuamuru kuzipiga marufuku timu hizo hadi pale zitakaposaini mkataba huo wa Star Times.
FKF ilizipiga marufuku timu hizo kushiriki ligi kuu ya FKF baada ya kudinda kusaini mkataba wa Star Times ambao ungewezesha mechi za timu hizo kupeperushwa mbashara na runinga hiyo ya China .
Shirikisho hilo pia linamchunguza mwenyekiti wa Gor Mahia Ambrose Rachier baada yake kaundika barua kwa Star Times kuondoa barua ya kwanza iliyoandikwa na aliyekuwa katibu mkuu Sam Ochola kusaini mkataba huo .
Zoo FC vs. Kenya Football Federation – Order (17 Dec 2020)
Mkataba wa FKF na Star Times umeibua hisia kali huku vilabu vya Ulinzi Stars,Mathare United ,Gor Mahia na Zoo Fc vikiupinga kwa kukiuka haki zao hatua iliyochangia kupigwa marufuku na kutimuliwa ligini kwa Mathare United na Zoo Fc .
Timu za Mathare na Zoo zilizuiwa kucheza mechi zao za kufungua msimu wa ligi wiki jana wakati Gor na Ulinzi wakiwa tayari wamecheza mechi 2 na moja mtawalia katika ligi kuu.
Mahakama ya SDT itakutana wiki ijayo kusikiza kesi hiyo na kutoa maelekezo zaidi huku ligi ya FKF ikiangia mechi za mzunguko wa nne mwishoni mwa juma hili.