Categories
Kimataifa

Jeshi la Nigeria lakana kuwaua waandamanaji

Jeshi la Nigeria limekanusha madai kuwa liliwaua waandamanaji wasio na silaha kwenye mkutano jijini Lagos mnamo mwezi uliopita.

Wanajeshi hao wamedai kuwa walikuwa wakitumia bunduki ambazo hazikuwa na risasi kwenye makabiliano na raia.

Afisa mmoja mkuu, Brigedia Jenerali Ahmed Taiwo aliwasilisha ushahidi wa kanda ya video kuthibitisha madai yake yaliyotolewa kwa jopo la wachunguzi.

Shirika la Kimataifa la kutetea haki, Amnesty International linasema watu 12 waliuawa wanajeshi walipofyatua risasi wakati wa maandamano ya kupinga ukatili wa polisi katika mtaa wa mabwenyenye wa Lekki, jijini Lagos.

Walioshuhudia waliliambia Shirika la Utangazaji la BBC kuwa wanajeshi waliwafatulia waandamanaji risasi.

Waandamanaji wengine 1,000 walikuwa wamekusanyika kwenye lango la kukusanya ushuru katika barabara ya kueleke mtaa wa Lekki mnamo tarehe 20 Oktoba kuzuia magari kutumia barabara hiyo kuu.

Askari waliripotiwa kuonekana kuweka vizuizi katika barabara ya kuelekea eneo la maandamano muda mfupi kabla ya risasi kuanza kufyatuliwa.

Shambulizi hilo lilitokea baada ya siku kadhaa za maandamano dhidi ya kitengo cha polisi cha Kupambana na Ujambazi, SARS, ambacho mienendo ya maafisa imekashifiwa vikalina na raia wa nchi hiyo.

Categories
Kimataifa

Polisi nchini Nigeria waamriwa kukomesha ghasia nchini humo

Mkuu wa Polisi nchini Nigeria ameamuru kutumiwa rasilimali zote za idara ya polisi kukomesha ghasia na wizi wa ngawira nchini humo.

Mohamed Adamu amesema wahalifu wanatumia nafasi ya maandamano ya kupinga ukatili wa polisi kusababisha ghasia, jambo ambalo halikubaliki.

Maafisa wa polisi wameamriwa kukomesha ghasia, mauaji, uporaji na uharibifu wa mali ya umma.

Maandamano ya kupinga ukatili wa polisi yalianza tarehe 7 mwezi Oktoba.

Maandamno hayo ambayo yalijumuisha hasa sana vijana, yalitaka kikosi maalum cha polisi cha kukomesha wizi wa kimabavu SARS  kibanduliwe.

Rais Muhamaddu Buhari aliamuru kubanduliwa kwa kikosi hicho, ambacho kimelaumiwa kwa kusababisha mauaji ya kiholela, mateso na unyang’anyi wa mali.

Hata hivo baada ya siku kadhaa maandamano ya kutaka marekebisho makubwa yafanywe  yangali yanaendelea nchini humo.

Categories
Kimataifa

Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria aagiza kukomeshwa kwa ghasia nchini humo

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari ametoa wito wa kukomeshwa kwa ghasia zinazokumba taifa hilo.

Hata hivyo Rais huyo hakugusia madai ya mauaji ya waandamanaji yaliotekelezwa na maafisa wa polisi ambayo yameshtumiwa na jamii ya kimataifa na kuibua machafuko Jijini Lagos.

Rais Buhari aliwatahadharisha waandamanaji dhidi ya kuvuruga usalama.

Hii ni mara ya kwanza kwa rais Buhari kuzungumzia kuhusu ghasia hizo ambapo aliwalaumu watu aliosema wameteka maandamano hayo na kuendeleza ajenda zao.

Rais huyo mwenye umri wa miaka 77 aliwahimiza vijana kukomesha maandamano na kushauriana na serikali ili kutafuta suluhu kuhusu hali hiyo.

Jiji la Lagos limeshuhudia visa vya milio ya risasi, uporaji mali na kuteketezwa kwa gereza moja tangu maafisa wa usalama walipokabiliana na waandamanaji wanaoshinikiza mabadiliko ya uongozi na kukomeshwa kwa dhuluma za polisi katika jiji hilo lenye wakazi milioni 20.

Marekani, Muungano wa Afrika, Muungano wa Ulaya na Uingereza ni miongoni mwa mataifa yaliyoshutumu matumizi ya nguvu kuwatawanya waandamanaji.

Categories
Kimataifa

Polisi nchini Nigeria washtumiwa kwa mauaji ya waandamanaji Lagos

Watu kadhaa waliokuwa wakiandamana kulalamikia dhuluma za maafisa wa polisi wameripotiwa kuuawa au kujeruhiwa jijini Lagos, Nigeria.

Walioshuhudia wanadai kuwa watu 12 wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya wanajeshi kuwafyatulia risasi wakati wa maandamano hayo.

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu, Amnesty, limesema limepokea taarifa za kuaminika kuhusu mauaji hayo.

Rais Muha-Mmadu Buhari amewahimiza raia wa nchi hiyo kuwa watulivu huku amri ya kutotoka nje ikitangazwa katika jiji la Lagos na maeneo mengine.

Hali ya wasi wasi imeendelea kushuhudiwa katika maeneo mbali mbali ya mji wa Lagos baada ya polisi kulazimika kufyatua risasi hewani ili kuwatawanya waandamanaji wanaokaidi amri hiyo.

Maandamano dhidi ya kikosi cha kukabiliana na wizi wa mabavu, SARS, ambacho tayari kimevunjiliwa mbali, yamekuwa yakiendelea nchini Naijeria kwa majuma kadhaa.

Categories
Kimataifa

Nigeria kuchunguza madai ya dhuluma za polisi

Serikali ya Nigeria imeagiza kubuniwa kwa majopo ya majaji katika majimbo yote 36 kuchunguza madai ya dhuluma za polisi.

Majopo hayo yatapokea na kuchunguza malalamishi kuhusu dhuluma za polisi, zikiwemo zile zinazohusishwa na kikosi maalum cha kukabiliana na wizi wa kimabavu, al maarufu, Sars kilichovunjwa.

Majopo hayo pia yatachunguza visa vya maafisa wa polisi kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandaanaji tangu maandaano yalipoanza juma lililopita.

Hii ni pamoja na jopo huru la uchunguzi lililobuniwa na tume ya kitaifa ya kutetea haki za binadamu nchini humo.

Maelfu ya raia wa nchi hiyo wamekuwa wakiandamana kwenye miji mikuu kulalamikia dhuluma za polisi.

Wametoa wito marekebisho ya idara ya polisi na kushtakiwa kwa wale wanaotekeleza  dhuluma hizo.

Categories
Burudani

Safari bado! Davido

Mwanamuziki wa Nigeria kwa jina Davido anasema bado safari yao ya kupinga ukatili wa kikosi cha polisi wa kupambana na wizi wa kimabavu haijakamilika.

Kwa wiki kadhaa raia nchini Nigeria wamekuwa wakishinikiza kuvunjiliwa mbali kwa kikosi kwa jina SARS baada ya ukatili wake kukithiri.

Maandamano dhidi ya kikosi hicho yaliandaliwa kwa siku kadhaa na kwenye mitandao ya kijamii wasanii na watu wengine maarufu hata waigizaji wa Nollywood waliendesha Kampeni kali.

Jana inspekta jenerali wa polisi nchini Nigeria alitangaza kuvunjiliwa mbali kwa kikosi cha SARS jambo ambalo lilipokelewa vyema na wengi.

Mwanamuziki Wizkid hakuficha furaha yake na kwenye Instagram aliandika kwamba wameshinda vita dhidi ya kikosi hicho cha polisi ila wasanii wenzake Davido na Burna Boy hawakubaliani naye.

Davido aliandika, “It’s far from over … we never win anything.” kumaanisha kwamba vita bado haijaisha na hawajashinda lolote.

Burna Boy naye aliandika, “They have now allegedly disbanded SARS but so much more needs to be done!! SARS is more than a ‘unit’ its a mindset built from lack of repercussions for the law enforcement. It is not over yet family!”

“We just de start”

Maanake “Wamevunjilia mbali kikosi cha SARS lakini ni mengi yanastahili kufanywa!! SARS ni zaidi ya kikosi, ni mawazo yaliyojengwa kutokana na ukosefu wa hatua kuchukuliwa dhidi ya kutotii sheria. Bado hayajaisha. Ndio tumeanza.

Watu wa Nigeria walikereka na kuanza maandamano baada ya video kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha polisi wa kikosi cha SARS wakidhulumu watu hadi kuwapiga risasi na kuwaua.