Categories
Kimataifa

Yoweri Museveni atangazwa mshindi katika uchaguzi mkuu wa Urais

Rais wa Uganda aliyetawala wa muda mrefu Yoweri Museveni, amechaguliwa tena kwa muhula wa sita.

Hayo ni kulingana na tangazo lililotolewa na tume ya uchaguzi nchini humo, huku kukiwa na madai ya udanganyifu wa kura kutoka kwa mpinzani wake mkuu Bobi Wine.

Museveni alipata karibu asilimia 59 ya kura, huku Bobi Wine akifuata kwa asilimia 35.

Awali, Wine ambaye ni mwana-Muziki wa zamani, aliahidi kutoa ushahidi wa kuonyesha kwamba kulikuwa na udanganyifu.

Hata hivyo, tume ya uchaguzi imekanusha kwamba kulikuwa na udanganyifu wowote kwenye uchaguzi huo wa siku ya Alhamisi.

Waangalizi wa uchaguzi huo wamekashfu hatua ya serikali kufunga huduma za internet, wakisema hatua hiyo ilihujumu imani.

Wine ameahidi kutoa ushahidi wa kuonyesha kulikuwa na udanganyifu mara tu huduma za internet zikirejeshwa.

Watu kadhaa waliuawa wakati wa ghasia zilizoghubika kampeini za uchaguzi huo.

Wanasiasa wa upinzani pia wameshtumu serikali kwa kuwahangaisha.

Museveni mwenye umri wa miaka -76 ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1986 – amesema anawakilisha udhabiti nchini humo.

Categories
Kimataifa

Museveni aongoza katika matokea ya awali ya kura za Urais

Rais Yoweri Museveni wa Uganda amechukua uongozi wa mapema kwenye matokeo ya mwanzo ya uchaguzi wa urais yaliotangazwa na tume ya uchaguzi nchini humo Ijumaa asubuhi.

Museveni amezoa kura-1,852,263 hiyo ikiwa ni asilimia-63.09 naye mpinzani wake mkuu, Robert Kyagulanyi al-maarufu Bobi Wine ana kura-821,875 hiyo ikiwa ni asilimia 28.36 ya kura zilizohesabiwa kutoka vituo-8,310 vya kupigia kura.

Kuna jumla ya vituo-34,684 vya kupigia kura nchini Uganda.

Wakati huo huo, tume ya uchaguzi nchini humo imetoa hakikisho kuwa matokeo ya uchaguzi yanawasilishwa moja kwa moja hadi kituo kikuu cha kujumulishia matokeo hayo licha ya kufungwa kwa huduma za internet kote nchini humo.

Mkuu wa tume hiyo, Simon Byabakama amesema wanatumia mbinu mbadala kuwasilisha matokeo hayo lakini hakufafanua.

Chini ya sheria za Uganda, tume ya uchaguzi inapasa kuthibitisha matokeo yaliowasilishwa kutoka wilaya zote na kuyatangaza rasmi saa 48 baada ya uchaguzi kukamilika.

Washindi wa viti vya ubunge watatangazwa katika vituo vya kujumulishia matokeo wilayani ilihali mshindi wa kiti cha urais atatangazwa katika kituo cha kitaifa cha kujumulishia matokeo mjini Kampala.

Categories
Burudani

Bobi Wine aangaziwa kwenye Spotify

Mwanamuziki wa nchi ya Uganda Bobi Wine ameangaziwa kwenye kipindi fulani cha sauti tu ambacho kimewekwa kwenye jukwaa la muziki na vipindi vya sauti kwa jina Spotify.

Mwanamuziki wa mtindo wa Rap nchini Marekani kwa jina Bas ndiye mtangazaji katika kipindi hicho kilichopatiwa jina la “The messenger” na kitaangazia maisha ya Bobi Wine.

Mbunge huyo wa eneo bunge la Kyandondo Mashariki nchini Uganda ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi Ssentamu anaangaziwa kwa sababu anawania urais nchini Uganda kwenye uchaguzi mkuu wa tarehe 14 mwezi huu wa Januari mwaka 2021.

Safari yake ya uanaharakati na kampeni za urais haijakuwa rahisi na kwa sasa anaonekana kuwa mpinzani mkuu wa rais wa sasa Yoweri Museveni.

Jukwaa la kimitandao la Spotify linatoa fursa kwa watu kupakua na kusikiliza muziki na vipindi popote walipo lakini barani Afrika, linapatikana katika nchi chache.

Afrika Kusini, Morocco, Misri, Algeria na Tunisia ndizo nchi pekee ambazo zimekubalia Spotify kufikia sasa na haijulikani litasambaa lini kwenye nchi nyingine za Afrika.

Hii ina maana kwamba hata Uganda ambayo ni nchi muhimu kwa kipindi hiki cha Bobi Wine haitapata kukisikiliza.

Kipindi kuhusu maisha ya Bobi Wine kimeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Dreamville Studios na Awfully Nice Productions na kilikuwa kipatikane kwa mara ya kwanza kwenye Spotify tarehe 5 mwezi Januari mwaka 2021 siku chache kabla ya uchaguzi mkuu nchini Uganda.

Categories
Kimataifa

Watu 16 wafariki katika ghasia za kushinikiza kuachiliwa kwa Bobi Wine

Watu-16 wameuawa kwenye ghasia za siku mbili nchini Uganda zilizofuatia kukamatwa kwa mgombeaji urais aliyepia msanii, Bobi Wine.

Watu hao waliuawa kwenye oparesheni ya maafisa wa usalama huku watu wengine 65 wakijeruhiwa na 350 kukamatwa.

Haijadokezwa watu hao walifariki kutokana na majeraha yapi.

Bobi Wine ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi alikamatwa siku ya Jumatano kwa kukiuka kanuni za kudhibiti msambao wa ugonjwa wa Covid-19.

Kyagulanyi aliye na umri wa miaka-38 amekashifiwa kwa kukaidi kanuni za kuzuia maambukizi ya Korona kwa kuruhusu umati wa watu kuhudhuria mkutano wake wa kampeni mashariki mwa nchi hiyo.

Msanii huyo ni miongoni mwa wagombeaji 11 wanaomopinga rais Yoweri Museveni ambaye amekuwa uongozini tangu mwaka-1986.

Wagombea urais wa upinzani nchini humo wamesitisha kampeni zao za ikulu, wakishinikiza kuachiliwa kwa mwenzao Bobi Wine.

Uchaguzi mkuu nchini Uganda utafanyika tarehe-14 Januari mwakani.

Categories
Kimataifa

Kukamatwa kwa ‘Bobi Wine’ nchini Uganda kwa sababisha maafa ya watu watatu

Maafisa wa polisi nchini Uganda wanasema watu watatu waliaga dunia  na wengine kadhaa kujeruhiwa jijini Kampala na katika miji mingine baada ya mwaniaji Urais, Robert Kyagulanyi, al-maarufu Bobi Wine, kukamatwa wakati wa mkutano wa kampeni.

Taarifa ya polisi hata hivyo haikueleza jinsi watu hao walivyoaga dunia.

Picha na video zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonesha waathiriwa wakiwa wamelala chini wakiwa wameloa damu huku ikionekana kana kwamba walipigwa risasi.

Ghasia zilizuka jijini Kampala kufuatia maandamano ya kushinikiza kuachiliwa kwa Bobi Wine anayezuiliwa Wilayani L’uuka’ baada ya polisi kumshutumu kwa kuandaa mkutano wa hadhara kinyume cha maagizo ya wizara ya afya ya kuzuia kusambaa kwa Korona.

Mwaniaji mwingine, Patrick Amuriat Oboi, pia amekamatwa.

Kwingineko mwaniaji urais nchini Uganda Mugisha Muntu amesitisha shughuli zake za kampeni hadi wawaniaji urais wa upinzani waliokamatwa siku ya Jumatano watakapoachiliwa huru.

Muntu ametoa wito wa kuachiliwa huru kwa Robert Kyangulanyi almaarufu Bobi wine na Patrick Amuriat ambao walikamatwa katika shughuli tofauti za kampeni.

Uchaguzi wa Urais utaandaliwa nchini Uganda mwezi Januari mwakani.

Categories
Burudani

Bobi Wine akamatwa punde baada ya kuidhinishwa kuwania Urais nchini Uganda

Mwanamuziki Bobi Wine wa nchi ya Uganda ambaye ni mbunge na sasa mwaniaji Urais anasemekana kukamatwa na polisi nchini humo punde baada ya kufika mbele ya Tume Huru ya Uchaguzi nchini Uganda ambapo aliidhinishwa kuwania Urais.

Kulingana na sauti ya mtu ambaye anaonyesha matukio mubashara kwenye ukurasa ulioidhinishwa wa Facebook wa Bobi Wine, haijulikani Mbunge huyo kwa jina Robert Kyagulanyi amepelekwa wapi.

Wafuasi wake wanaonekana kukusanyika kando kando ya barabara na kwa wakati mmoja wanarushiwa vitoza machozi na polisi.

Kabla ya hapo, polisi walikuwa wamemchagulia barabara ambayo angetumia hadi kwenye eneo la uteuzi na kulingana na maneno kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii alikuwa amekubaliana nao.

Kulingana naye alitaka mpango mzima wa uteuzi uende sawa hakutaka lolote liwe kikwazo.

Bobi aliidhinishwa kuwania Urais kupitia chama cha National Unity Platform “NUP” na sasa anajiunga na wengine walioidhinishwa jana ambao ni Rais wa sasa wa taifa la Uganda Yoweri Kaguta Museveni, Mugisha Muntu na Henry Tumukunde.

Kwa sasa Bobi Wine anawakilisha eneo bunge la Kyandondo Mashariki bungeni na pia ni muigizaji na mhisani ambaye husaidia wasiojiweza katika jamii.
Uchaguzi mkuu wa nchi ya Uganda unatarajiwa kuandaliwa Alhamisi tarehe 18 mwezi Februari mwaka ujao wa 2021.