Categories
Burudani

Sound from Segerea – Dullvani amtania Rayvanny

Mchekeshaji na muigizaji wa Tanzania Dullvani ambaye jina lake halisi ni Abdallah Sultan amemkejeli msanii wa muziki Rayvanny kutokana na shida aliyojipata ndani hivi karibuni.

Dullvani ametengeneza “Cover” ya albamu ya muziki ambayo anafananisha na ile ya Rayvanny. Yake ameiita “Sound from Segerea” ya Rayvanny ikijulikana kama “Sound From Africa”.

Ameweka picha yake karibu na orodha ya nyimbo zilizoko kwenye albamu hiyo ambayo inamwonyesha akiwa kizuizini. Segerea ni jina la jela ya serikali mjini Dar Es Salaam nchini Tanzania.

Kwa kifupi, Dullvani anaonekana kutania Rayvanny baada yake kukamatwa na kuachiliwa kwa dhamana kwa kosa la kujihusisha kwa vitendo vya kimapenzi na mtoto kwa jina Paula Kajala na ikiwa atapatikana na hatia kwenye kesi hiyo huenda akafungwa jela.

Wimbo wa kwanza kwenye albamu ya Dullvani ni Sound From Segerea ambao amemshirikisha Babu Seya mwanamuziki ambaye aliwahi kufungwa jela kwa kuhusika kingono na watoto wa shule kisha baadaye akaachiliwa kupitia kwa msamaha wa Rais wa Tanzania.

Kuna nyimbo ambazo ameorodhesha za kuchekesha tu kama vile “Sitaki tena wanafunzi” ambao amemshirikisha Diamond Platnumz, mwingine unaitwa “Bad Valentine” na hapa anaonekana kurejelea siku ya wapendanao ambayo ilikuwa jumapili iliyopita wakati Rayvanny aliachilia kibao kifupi kwa jina “Valentine”.

Ametaja pia watu wengine kama vile Mange kimambi ambaye amekuwa mstari wa mbele kulaani vitendo vya Rayvanny na mtoto Paula ila sasa amebadili msimamo na kuacha kujihusisha na kisa hicho.

Categories
Uncategorised

Hamisa Mobeto na Rayvanny waachiliwa huru

Wasanii wa Tanzania Hamisa Mobeto na Rayvanny wameachiliwa huru baada ya kulala usiku mmoja katika kituo cha polisi cha Oyster bay.

Kaimu Kamanda wa Polisi katika Mkoa wa Kinondoni Japhet Kibona, alisema ni kweli wasanii hao Hamisa Mobetto na Rayvanny walikuwa wameshikwa na polisi wa kituo cha Oyster Bay lakini wameachiliwa kwa dhamana huku uchunguzi ukiendelea.

Hamisa na Vanny boy wanasemekana kuitwa na polisi wa kituo hicho jana jioni kutokana na majukumu yao kwenye sakata inayohusu mtoto kwa jina Paula Majani ambaye anajiita Paula Kajala kwenye mitandao ya kijamii.

Rayvanny alichapicha video ambazo zilimwonyesha akibusu mtoto huyo ambaye anastahili kuwa katika kidato cha tano sasa.

Ni kweli kwamba amezidi umri wa miaka 18 lakini anachukuliwa kama mali ya serikali ya muungano wa Tanzania hadi atakapotimiza umri wa miaka 21 na kukamilisha elimu ya shule ya upili.

Inasemekana kwamba polisi walivutiwa na sakata hiyo kwenye mitandao ya kijamii na ndipo wakamwita muigizaji Frida Kajala na mtoto wake Paula ambao walisindikizwa na Harmonize ambaye ni mpenzi wa Frida na baadaye Hamisa Mobeto na Rayvanny wakaitwa.

Watu wengi maarufu nchini Tanzania wamelaani kitendo cha Rayvanny cha kuvujisha video zake na Paula huku Frida Kajala naye akinyoshewa kidole cha lawama kuhusu jinsi anamlea mwanawe.

Hamisa Mobeto naye ameonywa dhidi ya kuchapisha picha na video za mtoto huyo kwenye mitandao ya kijamii.

Categories
Burudani

Maoni ya Baba Levo

Msanii na mtangazaji wa Tanzania Baba Levo ametoa maoni yake kuhusu sakata ya msanii mweza Rayvanny na msichana kwa jina Paula Majani ambayo inaendelea kwenye mitandao ya kijamii.

Baba Levo ambaye ni mtangazaji kwenye kituo cha redio kinachomilikiwa na Diamond Platnumz Wasafi Fm, alihojiwa na wanahabari ambapo alisema kwamba Paula ambaye wengi wanadhani ni mtoto wa shule sio mwanafunzi kwani yuko nyumbani wakati wanafunzi wengine wa kidato cha tano wamesharejea shuleni.

Alisema pia kwamba Paula, mtoto wa mwigizaji Frida Kajala Masanja na Bwana Majani ameshafikisha umri halali wa utu uzima wa miaka 18.

Haya yanatokana na video ambayo mwanamuziki Rayvanny aliiweka kwa muda kwenye akaunti yake ya Instagram akimbusu mwanadada huyo kwa jina Paula kitendo ambacho kimeghadhabisha wengi nchini Tanzania ambao ni wasanii, watu maarufu na ni wazazi vile vile.

Mama Paula, Frida Kajala alielekezewa lawama kwa kutomlea mtoto wake vizuri kwa maadili yanayostahili naye akaelekeza kidole cha lawama kwa Hamisa Mobeto. Hamisa alijitetea kiasi cha kutoa ithibati ya video ambayo inaonyesha akiwa na Paula kwenye gari siku ambayo alimpeleka kupata chakula cha mchana.

Frida anasema kwamba siku hiyo hiyo ndiyo Hamisa alimpeleka kwa Rayvanny ambapo walimywesha pombe na mengine yakaendelea.

Baba Levo alifichua kwamba babake Paula kwa jina P Funk Majani alichoka na visa vyake na akanawa mikono na kuachia mamake malezi.

Msanii huyo anashauri kwamba Paula aachwe aolewe na Rayvanny kwani wameonyesha wanapendana na kwamba Rayvanny ana uwezo wa kifedha anawenza kumtunza vywema.

Inasubiriwa kuona jinsi sakata hii itaisha huku kukiwa na tetesi kwamba mamake Paula na msanii Harmonize walionekana jana wakikwenda kwenye kituo cha polisi na wengi wanakisia kwamba alikwenda kumshtaki Rayvanny.

Rayvanny alizindua kibao kwa ajili ya siku ya wapendanao na maneno ya wimbo huo yanaonekana kumzungumzia Paula.

Categories
Burudani

Sound from Africa yaangaziwa kwenye mabango Marekani

Kazi ya hivi karibuni ya mwanamuziki wa Tanzania Rayvanny kwa jina “Sound from Africa” inaendelea kufanya vyema baada ya kuzinduliwa jana tarehe mosi mwezi Februari mwaka 2021.

Kanda hiyo yenye vibao 23 imewekwa kwenye bango kuu katika eneo la Times Square mjini New York Marekani na hilo limemjaza Rayvanny furaha anapoendelea kupona kutokana na majeraha aliyopata jukwaani tarehe 30 mwezi Januari mwaka huu nchini Tanzania.

Vanny Boy ambaye pia hujiita Chui, amepachika video na picha za bango hilo la Marekani likiwa na picha ya albamu yake kwenye akaunti yake ya Instagram.

Mwanamuziki huyo ambaye anajulikana kwa mtindo wake wa kuvaa koti kubwa za baridi zenye kofia anaomba koti moja kama hiyo kwenye maneno aliyoambatanisha na picha hizo pamoja na video.

kanda hiyo ndiyo ya kwanza kutoka kwa mwanamuziki Rayvanny ambaye alijiunga na WCB mwaka 2018 baada ya bendi yao ya “Yamoto” kusambaratika.

Ameendelea kufanya kazi na kampuni hiyo ya WCB kinyume na matarajio ya wengi hasa baada ya msimamizi wake Diamond Platnumz kufichua kwamba Rayvanny alikuwa ameanzisha kampuni yake ya muziki.

Mwisho wa mwaka jana, Diamond alisifia studio ambazo Rayvanny alikuwa akijenga huku akisema zikikamilika zitakuwa bora zaidi Afrika Mashariki.

Wakati huo Diamond alisema kwamba ikiwa Rayvanny angetaka kuondoka WCB angemruhusu lakini Rayvanny alikana tetesi za kugura WCB.

Alisema kwamba kampuni yake mpya itakuwa na wanamuziki ila yeye atasalia chini ya usimamizi wa WCB.

Categories
Burudani

Rayvanny azindua albamu yake mpya

Leo tarehe mosi mwezi Februari mwaka 2021, Raymond Shaban Mwakyusa mwanamuziki wa Tanzania maarufu kama Rayvanny amezindua albamu yake kwa jina “Sound From Africa”.

Mwimbaji huyo anayefanya kazi ya muziki chini ya kampuni ya WCB, ameweka albamu hiyo kwenye majukwaa mbali mbali ya mitandaoni.

Rayvanny ameshirikisha wanamuziki wengine wengi kwenye albamu hiyo yenye nyimbo 23 ambazo ni, Sound from Africa, Tetema, Senorita, Kelebe, chuchumaa remix, tingisha, Number One, Juju, Koroga, Rotate, Bebe, Baby, Bailando, Twerk, Zuena, Lala, Mama, Kiuno, Marry me, Zamani, Waongo, Juu na Woza.

Wanamuziki walioshirikishwa humo ni kama vile Diamond Platnumz, Jah Prayzah, GIMS, Innos B, Frenna, Aminux, Nasty C na Saida Kroli kati ya wengine wengi.

Habari kuhusu kuzinduliwa kwa albamu hii, zimewadia muda mfupi baada ya taarifa kuhusu ajali aliyopata Rayvanny akiwa jukwaani kutumbuiza ambayo ilitamatisha ghafla tamasha la “Wasafi Tumewasha na Tigo”.

Kulingana na video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, Rayvanny anaonekana kama ambaye aliteleza na kutanguliza kicha anapoanguka.

Vanny Boy aliweza kuinuka baada ya kuanguka na alisaidiwa kuondoka jukwaani na mtumbuizaji mwenza. Mkubwa wa Wasafi Media Diamond Platinumz alisitisha sherehe ya baadaye iliyokuwa imepangwa huku akihimiza mashabiki kutumia muda huo kushukuru Mungu na kumwombea Rayvanny.

Categories
Burudani

Rayvanny kuzindua albamu

Msanii wa Bongo Fleva Raymond Shaban Mwakyusa almaarufu Rayvanny ama ukipenda vanny Boy ametangaza kwamba ataachilia albamu yake ya kwanza hivi karibuni.

Vanny ambaye anafanya kazi ya muziki chini ya kampuni ya Diamond Platnumz Wasafi Classic Baby – WCB alianza muziki mwaka 2011 akiwa shule ya upili lakini hajawahi kuzindua albamu.

Alijiunga na WCB rasmi mwaka 2015 na mwaka 2016 akaachilia kibao “Kwetu” ambacho kilivuma sana Afrika mashariki.

Mwezi wa pili mwaka 2020 Rayvanny alizindua EP yake kwa jina “Flowers” ambayo ilifanya vyema kwenye mitandao ya kijamii.

EP au ukipenda ‘Extended Play’ ni mkusanyiko wa nyimbo ambazo hazitoshi kuitwa albamu. Mwanamuziki huyo ameteuliwa kuwania na kushinda tuzo kadhaa.

Ni kati ya wanamuziki wanaofanya vizuri katika WCB na mkubwa wake Diamond aliwahi kufichua kwamba alikuwa akijenga studio zake za muziki isijulikane kama atagura WCB alivyofanya Harmonize.

Diamond alisifia sana studio hizo akisema kwamba zikikamilika zitakuwa bora zaidi Afrika mashariki.

Rayvanny amejulikanisha ujio wa albamu hiyo kwa jina “Sound From Africa” kupitia picha na video ambazo amekuwa akiweka kwenye mtandao wa Instagram lakini hajatangaza tarehe rasmi ya kuiachilia.

Categories
Burudani

Eric Omondi na Sauti Sol wang’ara kwenye tuzo za AEAUSA

Wasanii wa Kenya Eric Omondi ambaye ni mchekeshaji na kundi la wanamuziki la Sauti Sol ndio wasanii pekee wa Kenya ambao walishinda tuzo kwenye tuzo za burudani Afrika huko Marekani au ukipenda African Entertainment Awards USA.

Erick Omondi ameng’aa kwenye kitengo cha mchekeshaji bora barani Africa ambapo alikuwa akishindana na mkenya mwenzake Eunice Mamito.

Omondi amekuwa akijirejelea kama Rais wa wachekeshaji wote barani Afrika na ushindi huu wake ni thibitisho kwamba kweli yeye ni kiongozi wa fani ya uchekeshaji barani humu.

Wengine ambao alikuwa akishindana nao ni Bovi wa Nigeria, Patrick Salvado na Anne Kansiime wa Uganda, Eddie Kadi wa Congo, Daliso Chaponda wa Malawi, Loyiso Gola wa Afrika Kusini, Gilmario Vemba na Calao show wote wa Angola.

Sauti Sol nao walishinda kwenye kitengo cha kundi bora la muziki Afrika huku wakiwabwaga, Best life Music wa Burundi, Weusi na Navy Kenzo kutoka Tanzania, B2C ya Uganda, R2 bees na Dope Nation wa Ghana, Toofan kutoka Togo, Calema wa nchi ya Sao Tome and Principe na mwisho Mobbers kutoka Angola.

Hafla ya kutuza washindi wa mwaka 2020 wa tuzo za AEAUSA ilifanyika jana tarehe 20 mwezi Disemba mwaka 2020 saa nne usiku saa za Afrika Mashariki.

Wasanii wa Tanzania Diamond Platnumz na Rayvanny waling’aa kwenye vitengo vya wanaume vya msanii bora wa kiume barani Afrika na msanii bora wa kiume katika eneo la Mashariki, kusini na kaskazini mwa Afrika mtawalia.

Tazama picha ya orodha ya washindi wa tuzo hizo za AEUSA mwaka 2020 zenye vitengo 24. Hongera kwa washindi.

Categories
Burudani

Ni ushauri tu, Baba Levo baada ya kumchamba Harmonize

Mwanamuziki na mtangazaji wa Tanzania Baba Levo anasema kwamba yeye hana ubaya na mwanamuziki Harmonize na kwamba yeye anampa ushauri tu.

Akizungumza wakati akihojiwa, Baba Levo alitoa orodha yake ya wasanii wanne wa kwanza nchini Tanzania. Kulingana naye Diamond Platnumz ni Nambari moja, anafuatiwa na Ali Kiba, wa tatu ni Rayvanny kisha Harmonize anaingia wa nne.

Mtangazaji huyo wa Wasafi Fm alisema kwamba anajaribu tu kumkanya Harmonize aache kung’ang’ana kushindana na Diamond ashindane na Rayvanny ambaye anasema ndiye wa kiwango chake.

Kwenye mahojiano hayo, Baba Levo alifichua kwamba Diamond anamiliki nyumba za kupangisha 126 Jijini Dar Es Salaam pekee.

Harmonize na Diamond awali walikuwa marafiki na yeye ndiye alikuwa msanii wa kwanza kuwahi kusajiliwa na kampuni ya Diamond ya muziki Wasafi Classic Baby (WCB) lakini baadaye akagura na kuanzisha yake kwa jina Konde Music.

Tangu wakati aligura, wengi wanasema kwamba Harmonize anajaribu sana kusababisha ushindani kati yake na Diamond Platnumz.

Diamond naye alisema ushindani ni muhimu katika sekta ya muziki nchini Tanzania lakini hajaonekana kujibu ushindani huo wazi wazi.

Harmonize alitoa wimbo kwa jina “Ushamba” na kwenye video akatumia jamaa mmoja anayefanana sana na Diamond Platnumz na akaima maneno yanayoonekana kumlenga Diamond Platnumz.

Wimbo huo ndio ulisababisha minong’ono ya jinsi Harmonize analazimisha ushindani lakini alijitetea akisema ni burudani tu.

Categories
Burudani

Octopizzo apendekezwa kuteuliwa kuwania tuzo za Grammy

Octopizzo ambaye ni mwanamuziki wa nchi ya Kenya ana raha baada ya kupiga hatua katika sanaa yake. Hii ni baada ya kupendekezwa kuteuliwa kuwania tuzo za kifahari za nchi ya marekani za Grammy.

Mwanamuziki huyo kwa jina halisi Henry Ohanga sasa yuko kwenye orodha ya wasanii wanaofikiriwa katika kuwania tuzo za Grammy mwaka 2021.

Hii huwa hatua ya kwanza katika tuzo hizo na baada ya hapo washirika katika “Grammy Academy” watapiga kura kuteua wawaniaji wa tuzo kutoka kati ya wengi waliopendekezwa.

Wimbo wake kwa jina “Another Day” unapendekezwa kuwania tuzo la rekodi bora ya mwaka, huku “Kamikaze ukipendekezwa kuwania tuzo la “Best melodic rap” pamoja na huo wa “Another day”.

Wimbo wake ambao amehusisha Sailors kwa jina “Che che” unapendekezwa kuwania tuzo la “Best Rap Performance”.

Octopizzo alitangaza hayo kupitia akaunti yake ya Twitter.

Wasanii wa Afrika Mashariki ambao pia wako kwenye orodha ya wanaofikiriwa kuwania tuzo za Grammy ni wanamuziki wa kampuni ya Wasafi au ukipenda WCB nchini Tanzania, Diamond Platinumz, Zuchu, na Rayvanny.

Nyimbo za Diamond “Jeje” na “Baba Lao” zinapendekezwa kuwania tuzo la Video bora ya mwaka huku albamu ya Rayvanny kwa jina “Flowers” ikipendekezwa kuwania tuzo la Albamu ya muziki wa dunia bora ya mwaka.

Zuchu anapendekezwa kwa kuwania tuzo la mwanamuziki bora mpya.

Alipohojiwa na Grammys Diamond alisema ikiwa atashinda tuzo la Grammy kwanza ataomba na kushukuru Mungu kwa wiki nzima kisha aandae onyesho kubwa bila malipo nchini Tanzania.

Categories
Burudani

Rayvanny Kuondoka Wasafi?

Fikra kuhusu uwezekano wa mwanamuziki kwa jina la usanii “Rayvanny” au ukipenda “Vanny Boy” kuondoka kwenye kampuni ya Wasafi inayomilikiwa na Diamond Platinumz, zinatokana na usemi wa Diamond mwenyewe.

Wakati wa mahojiano yake kwenye kipindi cha ‘The Switch’, kwenye Wasafi FM siku ya jumanne, Diamond alifichua kwamba hivi karibuni Rayvanny anazindua kampuni yake ya kusimamia wanamuziki.

Diamond alisema ameona Studio ambazo Rayvanny anaandaa na kulingana naye zikizinduliwa zitakuwa bora kuliko zote nchini Tanzania.

Alipoulizwa kuhusu uhuru wa wanamuziki walio chini ya Wasafi kuondoka na kujiendeleza, Dianond alisema wana uhuru wa kufanya vile.

Mwimbaji huyo wa kutokea eneo la Tandale alisema kila mara huwa anawahimiza wanamuziki walio chini yake waishi vizuri na watu na watafute kujiendeleza kifedha.

“Iwe mfano ni mimi, nimefika hapa nilipo halafu wakati mmoja unikute kule Tandale nakuomba shilingi mia jamani! ikiwa ni mimi sitakupa!” Alisema mwanamuziki huyo.

Maneno yake yanaonekana kuwa kinaya kwani hadi sasa, kampuni ya Wasafi haijamwachilia kikamilifu mwanamuziki Harmonize ambaye aligura na kuanzisha kampuni yake kwa jina “Konde Music”.

Harmonize alifichua kwamba mkataba wake na WCB unamhitaji alipe milioni mia tano pesa za Tanzania kabla apate hakimiliki za nyimbo zake na kuandikisha hakimiliki yake mwenyewe.

Kulingana naye amelazimika kuuza mali nyingi kulipa deni hilo lakini bado hajalimaliza.

Inasubiriwa kuona ikiwa Rayvanny atagura Wasafi au atasalia tu akiendeleza biashara yake kando au atagura na ikiwa atagura safari yake itakuwa rahisi au ngumu kama ya Harmonize?