Kamati ya kitaifa ya mpango wa BBI imewapongeza wanachama wa mabunge ya kaunti kote nchini kwa kupitisha mswada wa marekebisho ya katiba wa mwaka 2020.
Kwenye taarifa, kamati hiyo imesema wawakilishi wadi wametekeleza wajibu wao wa kihistoria kwa kukubaliana na mchakato wa marekebisho hayo ya katiba yatakayowezesha taifa hili kusonga mbele.
“Pia tunawashukuru kwa kuisikiliza sauti ya wananchi wakati wa maamuzi yao kuhusu mswada wa marekebisho ya katiba wa mwaka 2020,” imesema taarifahiyo.
Kamati hiyo pia imewasifu Wakenya kwa kujitolea kwa wingi na kushiriki katika vikao vya ukusanyaji maoni ya umma kuhusu mswada huo, huku wakipuuzilia mbali habari za uongo zinazoenezwa na wanaopinga mchakato huo.
Wanakamati hao wanasema kupitishwa kwa mswada huo kote nchini ni ishara kwamba wananchi wa Kenya wamezungumza kwa sauti moja.
“Ushindi huu mkubwa unaashiria umaarufu wa BBI na ni ishara ya uungwaji mkono wa mswada wa BBI wakati wa kura ya maamuzi,” wakasema.
Na huku mswada huo ukielekea katika hatua ya mbele, kamati hiyo imewaomba wabunge kuzipa kisogo propaganda zinazoenezwa na kuwaiga wawakilishi wadi kwa kupitisha mswada huo katika Bunge la Kitaifa.
Hayo yanajiri huku mabunge zaidi ya kaunti yakiendelea kujadili mswada huo ambao tayari umetimiza masharti ya kikatiba ya kuungwa mkono na angalau mabunge 24 ya kaunti ili kuingia kwenye awamu nyengine.
Kufikia sasa mabunge 41 yamepitisha mswada huo, huku Bunge la Kaunti ya Migori likisalia la pekee lililokataa mswada huo.
Macho sasa yanaelekezwa kwa kaunti tano zilizosalia, ambazo hazijapigia kura mswada huo zikiwemo Nandi, Elgeyo Marakwet, Uasin Gishu, Mandera na Kilifi.
Sheria inasema mabunge ya kaunti yanafaa kuidhinisha rasimu ya mswada huo katika kipindi cha miezi mitatu baada ya kuwasilishwa.
Mswada huo sasa utawasilishwa kwa Spika Justin Muturi wa Bunge la Kitaifa na Ken Lusaka wa Seneti ili kupitishwa kabla ya kuwasilishwa kwa Rais Uhuru Kenyatta ambaye atatia saini na kuuwasilisha kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwa ajili ya kuandaa kura ya maamuzi.