Kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga ametetea pendekezo la kuanzisha afisi ya kupokea malalamishi ya umma katika idara ya mahakama kwenye ripoti ya mpango wa maridhiano, BBI.
Raila amesema kuwa afisi hiyo itahakikisha kwamba idara ya mahakama inawawajibikia Wakenya.
Amesema kuwa afisi hiyo huru itasuluhisha malalamishi ya Wakenya kuhusiana na hukumu zinazotolewa kwa njia isiyo na usawa na pia mienendo isiyofaa ya majaji, mahakimu na maafisa wengine wa idara ya mahakama.
Raila, ambaye aliandamana na Waziri wa Usalama wa Kitaifa Fred Matiang’i na mwenzake wa Ugatuzi Eugene Wamalwa, amekanusha madai kwamba ripoti ya BBI inanuia kuanzisha urais wenye mamlaka makuu.
Ametoa wito kwa viongozi kukomesha propaganda kuhusiana na ripoti ya BBI.
“Kuna madai kwamba mapendekezo haya yananuia kuanzisha rais mwenye mamlaka makuu. Kuanzishwa kwa afisi ya kupokea malalamishi ya umma katika idara ya mahakama ni kwa manufaa ya wananchi,” akasema Raila.
Viongozi kadhaa wa maeneo ya Nyanza na Magharibi waliokuwepo miongoni mwao Mwenyekiti wa Baraza la Magavana, Wycliffe Oparanya na Gavana wa Trans Nzoia, Patrick Khaemba wametoa wito kwa wakenya kuunga mkono ripoti hiyo kwa wingi.