Categories
Burudani

Sijawahi kumroga mume wangu!

Ndivyo alivyojitetea mwanamuziki wa Tanzania Queen Darleen ambaye kwa muda mrefu alichukuliwa kuwa dadake Diamond Platnumz kuhusu uhusiano wake na mume wake Isihaka.

Minong’ono ilikuwa imesheheni mitandao ya kijamii awali kwamba kamshikia dawa ya mapenzi ndiposa anampenda na kusahau mke wake wa kwanza.

Queen ni mke wa pili wa Isihaka na wakati fulani kulinuka ugomvi kati yake na mke wa kwanza ambaye anaitwa Sabra na wakati fulani alipohojiwa Darleen akasema anajua ameolewa yeye peke yake wengi wakadhani labda mke wa kwanza kaachwa.

Lakini jana wanandoa Isihaka na Darleen walifafanua kwamba wako wote kwenye ndoa hiyo na ndipo alisema kwamba hajawahi kumtafutia mume wake dawa ya mapenzi ili awe naye. Aliendelea kwa kusema kwamba akiamua kumroga basi atakuwa mke pekee kwenye ndoa hiyo.

Walikuwa wakihojiwa kwenye kituo cha redio cha Wasafi FM ambacho kinaendeleza mahojiano ya wapenzi na wanandoa mwezi huu wa mapenzi.

Isihaka alisema kwamba huwa anagawa siku zake za wiki kati ya wake zake wawili, siku nne kwa mke mkubwa na tatu kwa mke mdogo.

Darleen naye alielezea kwamba anamjali mume wake sana ndio maana lazima amheshimu mke mwenza kwani mume wake anampenda sana mke mkubwa. Hiyo alisema ndiyo sababu aliacha kupachika picha za Isihaka kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii kila mara.

Mwanadada huyo ambaye ni mwanamuziki chini ya Kampuni ya WCB ya Diamond Platnumz alisifiwa sana na mume wake ambaye alisema kwamba anajua sana kutekeleza majukumu yake kama mke na kwamba anapokuwa nyumbani yeye sio Queen Darleen bali ni Mwanahawa kwani hata mavazi hubadilika wakiwa pamoja.

Categories
Burudani

Siku 40 za mtoto Balqis Isihaka ulimwenguni

Balqis Isihaka ni mtoto wa kike wa mwanamuziki wa nchi ya Tanzania Queen Darleen na Isahaka mtoro. Queen Darlene ni dadake Diamond Platnumz lakini hakuhudhuria arusi ya wawili hao mwisho wa mwaka jana kwani alikuwa amesafiri.

Darlene ni mke wa pili wa mwanabiashara Isihakia.

Jumamosi tarehe 21 mwezi Novemba mwaka huu wa 2020, mtoto huyo alitimiza siku arobaini tangu kuzaliwa na ilikuwa sherehe ya kipekee.

Imekuwa kawaida kwa wafuasi wa dini ya kiisilamu kwa mama na mtoto kukaa nyumbani kwa siku arobaini za kwanza na zinapokamilika, sherehe inafanyika.

Mojawapo ya mambo ambayo hufanyika kwenye sherehe hiyo ni kunyolewa kwa mtoto kwani nywele ambayo alizaliwa nayo inachukuliwa kuwa chafu kwa hivyo inaondolewa ili kutoa nafasi kwa nywele safi kumea.

Sherehe ya jumamosi ilisheheni mbwembwe za kipekee na ilikuwa ya wageni waalikwa tu na hata kwenye tangazo mahali pa tukio hapakutajwa . Diamond Platnumz alifika akiwa ameandamana na meneja wake ambaye sasa ni mbunge wa Morogoro Kusini na watu wengine wengi japo kwa kuchelewa.

Walipohojiwa, wazazi wa mtoto huyo walisema tayari ameanza kupata kazi za mauzo.

Wengi walidhania kwamba Diamond hangehudhuria kwani alikuwa akiunda muziki studioni na gwiji wa muziki toka Congo Koffi Olomide.

Mwanamuziki aliyepia mwanamitindo Gigy Money naye alihudhuria sherehe ya mtoto Balqis. Queen Darleen na Diamond Platnumz wana baba mmoja ambaye anajulikana kama Abdul Juma, mzee huyo pia alihudhuria sherehe ya mjukuu wake.

Darleen na Diamond awali hawakuwa na uhusiano mzuri na mzee Abdul Juma lakini wakati fulani waliridhiana. Tukio la jumamosi lilionyeshwa mubashara kwenye runinga ya Wasafi.