Gavana wa Kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho na mwenzake wa Kilifi Amason Jefwa Kingi wameanzisha mchakato wa kuleta pamoja viongozi na wakazi wa eneo la Pwani ili kuafikia azma ya umoja wa kisiasa wa eneo hilo huku uchaguzi mkuu ukikaribia.
Kwenye mazungumzo yaliyofanyika Jumatano katika eneo la Wundanyi, magavana hao walijumuika na wenzao wa eneo hilo, akiwemo Gavana wa Taita Taveta Granton Samboja na Gavana wa Tana River Dhadho Godhana kwa lengo la kutafuta mwelekeo wa pamoja wa kisiasa.
Viongozi hao walimteua Gavana Samboja kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kaunti za Pwani kwa muda wa miaka miwili katika harakati za kutafuta mwelekeo wa kisiasa wa eneo hilo ifikapo mwaka wa 2022.
“Ajenda kuu ni kuleta kaunti zote [za Pwani] pamoja kwa mambo ya maendeleo. Tumekubaliana kwa kauli moja kama magavana wa eneo la Pwani kwamba wakati huu hatutakuwa kwa menu tutakuwa kwa meza,” akasema Samboja baada ya kuteuliwa kwake.
Joho, ambaye ni Naibu Kinara wa Chama cha ODM, tayari ametangaza kuingia katika kinyang’anyiro cha kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao, huku akisema kwa miaka mingi, viongozi na wakazi wa Pwani wameunga mkono wagombea kutoka maeneo mengine ya nchi na ni wakati wao sasa kuunga mkono mgombea kutoka Pwani.
Kumekuwa na shinikizo kutoka kwa baadhi ya viongozi wa eneo hilo kuhusu haja ya kuundwa kwa chama cha kisiasa cha Pwani, eneo ambalo limejulikana kwa muda mrefu kuwa mojawapo ya ngome za chama cha ODM, chake Raila Odinga.
Hata hivyo, Gavana wa Kaunti ya Kilifi Amason Kingi ameonekana kupinga haja ya kuundwa kwa chama kipya, akihoji kwamba tayari kuna vyama kadhaa vyenye asili ya Pwani, hivyo basi itakuwa bora kama vyama hivyo vitakuja pamoja ili viunde mrengo wa kisiasa.
Akiongea kwenye hafla ya uzinduzi wa mradi wa shilingi milioni 60 wa ujenzi wa barabara katika eneo la Mariakani Kaunti ya Kilifi, Kingi alisema vyama vya KADU Asili, Shirikisho, Republican Congress na Umoja Summit vina mizizi ya eneo hilo na ipo haja ya kuvileta pamoja.
“Ikiwa tayari tumegawanyika mara nne, nikiongeza cha tano nitakuwa natela umoja ama nitakuwa nagawanya zaidi? Tumeanza safari ya kuleta hivi vyama pamoja na hivi karibuni tutapata mwavuli,” akasema.
Hata hivyo azma hiyo huenda ikakumbwa na changamoto kutokana na migawanyiko ya kisiasa iliyoshuhudiwa hivi karibuni, huku baadhi ya viongozi akiwemo Mbunge wa Nyali Mohammed Ali, wa Malindi Aisha Jumwa, wa Kilifi Kaskazini Owen Baya, miongoni mwa wengine wakionekana kumuunga mkono Naibu Rais William Ruto.