Categories
Michezo

Tusker yailewesha Rangers wakati Sharks wakikosa heshima ugenini Mumias

Wagema mvinyo Tusker Fc wamewaka hai ya kunyakua taji ya 12 ya ligi kuu ya Kenya na ya kwanza tangu mwaka 2016 baada ya kuinyofoa Posta Rangers magoli 4-1 katika mchuano wa ligi hiyo uliopigwa Alhamisi Alasiri katika uwanja wa  kimataifa wa Kasarani.

John Macharia  aliwaweka wenyeji Tusker  uongozini kwa bao la dakika ya 38 ,kabla ya Ezekiel Okware kuisawazishia Rangers dakika moja baadae, huku  John Meja akiwaweka tena wana mvinyo uongozini kwa bao la pili katika dakika ya pili ya nyongeza kipindi cha kwanza.

Katika kipindi cha pili Tusker waliendeleza mashambulizi na kudhihirisha mchezo mzuri huku wakiongeza bao la tatu dakika ya  67 kupitia kwa Luke Namanda kabla ya Mejja kupiga jingine  dakika ya 84.

Ushindi huo umehahikisha Tusker wanaendelea kushikilia kukutu uongozi wa jedwali la ligi hiyo kwa pointi 29 kutokana na mechi 12 ,wakishinda 9 kwenda sare 2 na kupoteza mmoja wakifuatwa na Kenya Commercial Bank kwa alama 25 ingawa  vinara hao wa ligi wakiwa wamecheza mechi 2 zaidi.

Katika mkwangurano mwingine Kariobangi Sharks wamekwea hadi nafasi ya tatu ligini kufuatia ushindi wa bao 1 kwa bila ugenini dhidi Vihiga United uwanjani Mumias Complex Erick Kapaito akipachika bao la pekee na la ushindi  katika dakika ya 79 .

Bao hilo limehakikisha Kapaito anaendelea kuongoza msimamo wa ufungaji magoli akiwa amebusu nyavu mara 13 huku ushindi huo ukiwaweka Sharks kwa alama 21.

Categories
Michezo

Wafalme wa kutoka sare Ulinzi Stars wasajili sare ya nne ligini dhidi ya Bidco United

Timu ya wanajeshi ya Ulinzi Stars imelazimishwa kutoka sare tasa dhidi ya Bidco United katika mchuano wa ligi kuu uliochezwa Jumatano alasiri  katika uwanja wa Afraha kaunti ya Nakuru.

Sare hiyo ilikuwa ya tatu mtawalia na ya nne  kwa Ulinzi kusajii msimu huu wakiwa wamezoa alama 7 kutokana na mechi 6 za ufunguzi wakati bidco United  wakishikilia nambari 8 kwa alama 8.

Katika pambano jingine la ligi kuu Zoo Fc  na Posta Rangers pia walitoka sare ya 1-1 pia katika uwanja wa Afraha ,Collins Neto  akipachika bao la dakika ya 42 kwa Zoo ,kabla Dennis Oalo kusawazisha  kwa wageni Rangers dakika ya 68 ya mchezo.

Ilikuwa mechi ya pili kwa Zoo kucheza baada ya kutoka sare  ya 1-1 dhidi ya Bandari Fc wikendi iliyopita ,wakichelewa kuanza msimu sawa na Mathare United baada ya kufungiwa kushiriki ligini na Fkf kabla ya mahakama kuamrisha warejeshwe kwenye ligi kufuatia hatua ya timu hizo mbili kudinda kusaini mkataba wa Star Times.