Categories
Habari

Maafisa wa matibabu watoa ilani ya siku 14 kuanza mgomo

Maafisa wa Chama cha Taifa cha Matibabu wametishia kulemaza utoaji huduma katika taasisi za afya kote nchini katika muda wa siku 14 zijazo.

Maafisa hao wametishia kugoma ikiwa serikali haitashughulikia maslahi yao.

Kupitia kwa Mwenyekiti wao Peterson Wachira, chama hicho kinataka miongoni mwa mambo mengine ununuzi wa vifaa vya kujikinga wasiambukizwe katika viwango vyote vya utoaji huduma za afya na ulipaji mishahara ya wafanyakazi wote, waliopelekwa katika Kaunti chini ya mpango wa afya kwa wote.

Ilani hiyo imejiri huku mhudumu mwengine wa afya akiaga dunia kutokana na ugonjwa wa Korona huko Kisii, na kufikisha jumla ya maafisa wa matibabu waliopoteza maisha yao kwa Korona kuwa saba.

Wachira ametahadharisha kuwa ikiwa serikali itakwenda mahakamani kupinga mgomo huo, maafisa hao hawatakuwa na budi ila kutumia kipengee cha sheria kinachowaruhusu kuondoka kazini hadi mazingira ya kikazi yatakapoimarika.

Ilani hiyo inajiri huku serikali ikiwa tayari inakabiliwa na tishio lengine la mgomo kutoka kwa Chama cha Madaktari na Wataalamu wa Meno, KMPDU.