Mabunge kadhaa ya kaunti yanatarajiwa kupigia kura mswada wa marekebisho ya katiba wa mwaka 2020 wiki hii.
Bunge la Kaunti ya Meru litapiga kura hiyo wiki hii baada kufanywa mkutano wa hadhara wa uhamasisho siku ya Jumanne, huku kaunti za Nairobi, Laikipia na Embu zitakamilisha mikutano ya uhamasisho siku ya Jumatano.
Aidha, Wawakilishi wa Wadi huko Nakuru, Murang’a, Nyeri na Tharaka Nithi wanatarajia kuupiga kura mswada huo wa marekebisho ya katiba wiki hii baada kukamilishwa uhamasisho wa umma siku ya Alhamisi.
Kaunti za Siaya, Homa Bay na Kisumu tayari zimepitisha mswada huo wa marekebisho wa katiba wa mwaka 2020, huku ile ya Baringo ikiwa ya kwanza kuukataa mswada huo.
Kaunti ya Migori inatarajiwa kukamilisha shughuli hiyo wiki hii, huku chama cha ODM kikielezea matumaini kwamba kaunti za Kisii na Nyamira pia zitaidhinisha mswada huo.
Kaunti zina muda wa miezi mitatu kuchunguza kwa makini mswada huo kabla kufanya maamuzi.
Ni sharti angalau mabunge ya kaunti 24 kati ya yote 47 yaidhinishe mswada huo kabla ya kuwasilishwa katika Bunge la Kitaifa kujadiliwa na kupigiwa kura.
Ikiwa wabunge wataupitisha basi utawasilishwa kwa raia kwa kura ya maamuzi.
Huku hayo yakijiri, Seneta maalum Judith Pareno amewataka wanawake kuunga mkono mpango wa BBI, akihoji kuwa unawapa uwezo mwingi katika maswala ya maendeleo na uongozi.
Akiongea katika kijiji cha Mashuuru, Kaunti Ndogo ya Kajiado Mashariki alipongoza mkakati wa mashinani wa BBI, Pareno aliwahimiza wanawake kupuuzilia mbali miegemeo ya vyama vyao vya kisiasa na badala yake kuunga mkono mpango wa BBI.
Aliwaelimisha mamia ya wakazi wa sehemu hiyo kuhusu mpango huo akisema kuwa baadhi ya wanasiasa wameingiza uongo kwenye mpango huo.
Pareno aliwataka hasa wanawake wa kiMaasai kujiunga kwenye makundi ili kuwania nyadhifa za kuchaguliwa kwenye uchaguzi mkuu ujao.