Categories
Michezo

Shikanda ateuliwa kocha mpya wa Nzoia Sugar FcC

Klabu ya Nzoia Sugar Fc inayoshiriki ligi kuu ya Kenya imemteua  Ibrahim Shikanda kuwa kocha mpya ambapo atakuwa akisaidiwa na Sylvester Mulukurwa ambaye amekuwa akihudumu katika nafasi ya kaimu kocha .
Shikanda awali amekuwa na timu ya Nairobi Stima ikishiriki ligi ya Nsl na pia amekuwa naibu kocha wa Bandari Fc hadi mwishoni mwa msimu uliopita .
Timu hiyo yenye makao yake magharibi mwa Kenya ni ya 13 katika jedwali la ligi kuu  kwa alama 4 baada ya kwenda sare  mechi 4 kati ya 6 ilizocheza.
Mtihani wa kwanza kwa Shikanda katika benchi ya Nzoia Sugar Fc ni mwishoni mwa juma hili watakapochuana na Western Stima Fc.
Categories
Michezo

City Stars warejea ligini kwa madaha na kuifyonza Nzoia Sugar

Mabingwa wa ligi ya daraja ya pili nchini Kenya msimu jana , Nairobi City Stars walianza vyema maisha mapya ya ligi kuu FKF Jumapili adhuhuri baada ya kuwalabua Nzoia Sugar Fc magoli mawili bila jawabu katika uchanjaa wa kaunti ya Narok.

Nahodha Anthony Muki Kimani alifungua ukurasa kwa vijana hao wa mtaani Kawangware kwa bao la dakika ya 16 alipofyatua tobwe kutoka nje ya kijisanduku na dakika mbili baadae Oliver Maloba akakongomelea msumari wa mwisho kwenye jeneza na wakuza miwa Nzoia na kudumisha ushindi huo hadi kipenga cha mwisho.

City Stars walijihakikishia uhsindi baada ya penati ya  Nzoia sugar kupanguliwa na kipa wa City Stars  Steve Njuge katika kipindi cha pili.

Awali pambano hilo lilikuwa lipigwe uwanjani Nyayo kuanzia saa tisa alasiri , lakini likahamishiwa Narok huku mida ya kuchezwa pia ikirudishwa nyuma kutoka saa tisa hadi saa saba kutoka na mvua kubwa ambayo hunyesha kaunti Narok katika majira ya sasa.

Mvua kubwa ilikuwa ikinyesha katika kipindi cha kwanza ,kabla ya kupusa kunako kipindi cha pili .

Kwenye matokeo mengine   wahifadhi hela KCB waliisasambua Posta Rangers mabao 3-0 katika uwaja wa Utalii Derrick Otanga, Henry Onyango na  Enock Agwanda wakicheka na nyavu mara moja kila mmoja na kuendeleza matokeo bora ya   KCB ligini kutoka msimu jana.

Msimu mpya wa ligi kuu mwaka 2020/2021 ulianza rasmi Jumamosi huku ukitarajiwa kukamilika Mei mwakani.