Timu ya Kenya itakayoshiriki makala ya 32 ya michezo ya Olimpiki imepigwa jeki baada ya kamati ya Olimpiki nchini NOCK kusaini mkataba wa miaka mitano na kampuni ya kamari ya Kenya Charity Sweepstake ,mkataba wa kima cha shilingi milioni 10.
Pesa hizo zitatumika kuiandaa timu ya Kenya kwa michezo ya mwaka huu ya Olimpiki kuanzia Julai 23 mjini Tokyo Japan na Olimpiki ya mwaka 2024 mjini Paris Ufaransa .
Rais wa Nock Paul Tergat ana imani kuwa pesa hizo zitaiwezesha timu ya Kenya kupata maandalizi bora .
“Kwa miaka iliyopita,na haswa mwaka huu tumekuwa na matayarisho mazuri kwa michezo ya Olimpiki tukilenga ufanisi . Ndio maana tunawaomba wakenya wote kutuunga mkono ili tupate matokeo bora mwaka huu “akasema Tergat
Kulingana na mkataba huo asilimia 10 ya pato kutokana kwa Kenya Charity Sweepstake itawekwa katika akaunti ya NOCK.
Jumla ya wanamichezo 83 wa Kenya wamefuzu kwa michezo hiyo wakiwemo wanariadha 17,mchezaji Taekwondo mmoja,mabondia wawili,timu raga kwa wachezaji 7 upande kwa wanaume na wanawake,na timu ya voliboli kwa akina dada kila timu ikiwa na wachezaji 12 kwa jumla wakiwa 36.
Kenya italenga kuboresha matokeo ya mwaka 2016 mjini Rio De Janeiro ilikozoa dhahabu 6 fedha 6 na shaba 1 na pia matokeo bora zaidi iliyowahikusajili mwaka 2008 mjini Beijing ya dhahabu 6 fedha 4 na shaba 6.