Categories
Habari

Watu 57 wahukumiwa kuhudumia jamii kwa kukiuka masharti ya kudhibiti Covid-19

Watu 57 wamehukumiwa kuhudumia jamii kwa muda wa wiki moja na mahakama moja ya Kibra kwa kukiuka masharti ya wizara ya afya ya kudhibiti msambao wa Covid-19.

Watu hao walikamatwa na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Milimani Jijini Nairobi, kabla ya kuachiliwa chini ya uangalizi wa halmashauri ya Usimamizi wa jiji la Nairobi NMS, kwa kipindi hicho cha huduma kwa jamii.

Huku ikitoa hukumu hiyo, Mahakama hiyo ya Kibra ilisema halmashauri ya NMS,itasimamia shughuli hiyo katika taasisi mbali mbali na mitaa ya Jiji la Nairobi.

Watu hao 57 wanatarajiwa kuripoti kutoa huduma hiyo kwa jamii saa mbili asubuhi hadi saa kumi na moja jioni kila siku.

Majukumu yao yanajumuisha kusafisha soko la Marikiti na lile la Muthurwa, mzunguko wa Globe,mto Nairobi pamoja na majukumu mengine jinsi watakavyoelekezwa.

Aidha wale watakaokiuka watakamatwa upya na kushtakiwa kisha wataadhibiwa vikali Kulingana na taarifa ya halmashauri ya NMS.

Categories
Uncategorised

Familia 66,000 kunufaika na mpango wa afya kwa wote Jijini Nairobi

Halmashauri ya ustawi wa jiji la Nairobi imeanzisha shughuli ya kuhusisha umma katika mpango wa afya kwa wote katika kaunti zote ndogo 17 katika kaunti yaNairobi.

Shughuli hiyo ni mojawapo ya hatua za kubainisha familia 66,000 zitakazonufaika na mpango wa afya kwa wote kwa matayarisho ya kuanzishwa kwa shughuli ya kuimarisha sekta hiyo itakayoanza tarehe mosi mwezi Machi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa shughuli hiyo, Mkurugenzi mkuu wa halamashauri ya ustawi wa jiji la Nairobi Meja Jenerali Mohammed Badi alisema mpango huo unalenga kila familia, lakini utaanzishwa katika familia za wale wasiojimudu zinazoishi katika mitaa ya mabanda.

Meja Jenerali Badi pia alisema mpango unahusisha ustawishaji barabara katika mitaa ya mabanda, ili kurahisisha uokoaji wakati wa hali ya dharura, pamoja na uzinduzi wa hospitali 24 zaidi katika kaunti ya Nairobi

Categories
Habari

NMS yazindua mpango wa kutoa misaada ya barakoa shuleni

Halmashauri ya Usimamizi wa Huduma katika Jiji la Nairobi, NMS, imezindua shughuli ya utoaji barakoa shuleni ikilenga shule zote za kaunti ndogo 17.

Halmashauri hiyo inasema kila mwanafunzi atapokea barakoa mbili kupitia mchango uliotolewa na kampuni ya Kings Collection.

Kwenye taarifa, halmashauri hiyo imesema wafanyikazi wa Kaunti ya Nairobi tayari wametoa barakoa 700 kwa wanafunzi wa shule ya msingi ya Kwa Reuben, barakoa 2,000 kwa wanafunzi wa shule ya Our Lady of Nazareth na zengine 2,000 kwa wanafunzi wa shule ya St. Elizabeth Makadara.

Aidha, shughuli ya uhamasisho kuhusu ugonjwa wa COVID-19 inaendelea ikiongozwa na maafisa wa afya wa Kaunti ya Nairobi.

Categories
Habari

Wizara ya fedha yapata idhini ya kutoa pesa kwa kaunti ya Nairobi

Kaimu gavana wa Nairobi Benson Mutura ametia saini amri ya gavana ambayo inaipa wizara ya fedha idhini ya kutoa pesa kwa kaunti hiyo.

Hatua hiyo imejiri saa chache baada yake kuapishwa kuwa kaimu gavana kuchukua mahala pa Mike Sonko aliyeondolewa mamlakani kwa misingi ya matumzii mabaya ya mamlaka na ukiukaji wa katiba.

Gavana huyo aliyeng’atuliwa alikuwa amekataa kutia saini amri hiyo na hivyo kutatiza utekelezaji shughuli katika kaunti hiyo tangu mwezi oktoba.

Amri hiyo sasa inatoa idhini ya utekelezaji  wa bajeti ya kaunti ya Nairobi katika kipindi cha matumizi ya pesa za serikali cha mwaka 2020-21 ya shilingi bilioni-37.5.

Katika bajeti hiyo halmashauri ya usimamizi wa eneo la jiji la  Nairobi ilitengewa shilingi bilioni 27.1 ambapo aliahidi kushirikiana kwa karibu na halmashauri hiyo kwa minajili ya utoaji huduma bora kwa kaunti hii.

Mara tu pesa hizo zitakapotolewa kwa hazina ya mapato ya kaunti, wafanyikazi wa kaunti na bunge la kaunti hiyo watalipwa mishahara yao.

Mutura atashikilia wadhifa huo wa gavana hadi tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) itakapotekeleza uchaguzi mdogo wa gavana mpya katika muda wa siku 60.

Categories
Habari

Hatma ya Gavana Sonko kuamuliwa na maseneta 47

Hatima ya Gavana Sonko kuponea shoka la kutimuliwa imo mikononi mwa Bunge la Senate ambapo maseta 47 watamsikiza kabla ya kukata kauli.

Hata hivyo kulingana na hali ilivyo itakuwa vigumu kwa bunge hilo kumwokoa Gavana Sonko kulingana na mchanganuzi wa siasa Zacharia Baraza.

Kwa mjibu wa Baraza kubuniwa kwa shirika la NMS  linaloongozwa na jenerali Badi ilikuwa makusudi ili wakati atakapotimuliwa Gavana huyo kusiwe na pengo la utoaji huduma kwa wakaazi wa Nairobi.

“Ukiangalia yaonekana kuna mkono ambao unasukuma hoja hiyo na itakuwa vigumu kwa kunusurika na hata kubuniwa kwa shirika la NMS ilikuwa kuhakikisha kuwa utoaji huduma hakutaathirika hata endapo atafurushwa”akasema Baraza

Mchanganuzi huyo pia amesema utendakazi wa gavana huyo umeathirika pakubwa na kundi la watu walio na ajenda zao maarufu kama Cartels  huku Gavana huyo akishindwa kuwathibiti.

“Uongozi wa Gavana umeathirika pakubwa na cartels ambao ameshindwa kuwathibiti na hata mwenyewe amekuwa akitoa wengine na kuwajumuisha wengine katika serikali yake”akaongeza Baraza

Bunge la Senate linatarajiwa kukutana na kumsikiza Gavana huyo kabla ya kupiga kura kuamua endapo atanusurika au atabanduliwa.

 

Categories
Burudani

Eric Omondi ahuisha tishio la kutohamisha studio zake

Mchekeshaji Eric Omondi ambaye anajiita Rais wa wachekeshaji barani Afrika ametimiza tishio lake la kutohama eneo ambalo amefungua studio zake huko Lavington.

Hii ni baada ya shirika linalosimamia eneo la jiji la Nairobi NMS kuweka ilani kwenye lango la studio hizo tarehe 30 mwezi Novemba na kuwataka wenyeji kuhama kisa na sababu biashara hiyo imewekwa katika eneo la makazi.

Siku hiyo Eric alikashifu hatua hiyo akiisema kuwa kikwazo kwa vijana ambao wanajaribu kujitafutia riziki. Na jumamosi tarehe 5 mwezi Disemba mwaka huu wa 2020, Eric Omondi alichapisha video ikionyesha watu wakipaka rangi lango la studio zake kufuta ilani ya NMS.

Mchekeshaji huyo aliongeza kusema kwamba wameweka camera za CCTV katika sehemu tofauti za studio hizo ambazo pia ni afisi yake akisema wako tayari kukamata wezi maanake ni wezi tu ambao hutekeleza kazi zao usiku.

Kufikia sasa Eric anasisitiza kwamba hajapokea mawasiliano rasmi kutoka kwa shirika la kusimamia eneo la jiji la Nairobi kuhusu ilani ya kuhama.

Msemaji wa shirika hilo la NMS Bi. Rose Gakuo alijibu madai hayo akisema jambo hilo linashighulikiwa na NMS itatoa taarifa karibuni.

Mchekeshaji huyo ambaye ameanzisha shindano la kina dada kwa jina “wife Material” huku akitafuta mke, anasema studio hizo ni za kuendeleza kazi yake, kazi ya wasanii waliobobea na wale ambao wanaanza sanaa.

Alizipa studio hizo majina ya waigizaji maarufu Mzee Ojwang’ na Mama Kayai.

Categories
Burudani

Studio za Eric Omondi zafungwa

Studio za Eric Omondi ambazo mchekeshaji huyo alizindua hivi maajuzi zimefungwa na shirika la kusimamia eneo la jiji la Nairobi NMS.

Kulingana na NMS, studio hizo ambazo pia zina afisi za kampuni ya Eric Omondi ziko katika eneo la makazi la Lavington na hivyo anahitajika kuzihamishia kwingine.

Kupita Instagram Eric alijulikanisha hilo akisema kwamba haendi popote atasalia katika eneo hilo, kwani kufikia sasa wamepokea maombi kutoka kwa vijana wengi ambao wangependa kurekodi nyimbo zao katika eneo hilo na ni bila malipo.

Eric anaashiria pia kwamba kuna mwanamke mmoja ambaye anamshuku kwa kuandika maneno ya kuharamisha biashara yake kwenye lango la kuingia akimpa ilani ya kufuta maneno hayo na kuomba msamaha.

Anasema mwanamke huyo alihudhuria hafla ya kuzindua studio hizo na hajui anayemtumia mwanadada huyo.

Mchekeshaji huyo pia anashangaa ni kwa nini biashara yake pekee ndiyo inamulikwa katika eneo la makazi ambalo lina shule kadhaa, studio za Coke na afisi za Azam Tv.

Haya yanajiri siku chache baada ya Eric Omondi kutofautiana na Dakta Ezekiel Mutua Mkurugenzi mkuu wa bodi ya kuorodhesha filamu nchini Kenya KFCB.

Mutua anafahamika kwa kujaribu kuhakikisha maadili yanaendelezwa kwenye ulingo wa burudani nchini Kenya na alizungumza dhidi ya vitendo vya Eric ambapo amekuwa akisambaza picha na video akiwa nusu uchi.

Baadaye Eric alimfokea Bwana Mutua akimwambia aache kutamka jina lake kila mara.

Categories
Habari

Siogopi kung’atuliwa mamlakani,Mike Sonko afoka

Gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko amesema kuwa hahofishwi na njama ya baadhi ya wabunge wa bunge la kaunti ya Nairobi ya kutaka kumwondoa mamlakani.

Kwenye ujumbe katika ukurasa wake wa twitter gavana huyo anayekumbwa na utata alisema yuko tayari kuacha kazi akiongeza kusema kuwa kuna maisha hata baada ya siasa.

Alisema hataweka sahihi yake kutoa pesa kwa halmashauri ya huduma za usimamizi wa jiji la Nairobi.

Sonko alisema kuwa baadhi ya wabunge wa bunge la kaunti hiyo siku ya Alhamisi waliwasilisha hoja katika buneg hilo kutaka kumwondoa mamlakani.

Kiongozi wa wachache katika bunge la kaunti ya Nairobi Michael Ogada aliyewasilisha ilani ya hoja ya kutaka kumwondoa mamlakani anamshtumu gavana Sonko kwa matumizi mabaya ya mamlaka, mienendo isiyofaa na ukiukaji wa sheria mbalimbali.

Shutma hizo ni pamoja na ukiukaji wa katiba au sheria yoyote inayozungumziwa chini ya kanuni za ukiukaji wa sheria ya serikali ya kaunti hiyo ya mwaka 2012, sheria ya mwaka 2015 ya ununuzi na uuzaji wa bidhaa na huduma za umma, sheria ya usimamizi wa fedha za umma, mienendo isiyofaa miongoni mwa makosa mengine.

Masaibu ya gavana Sonko yanahusiana na hatua yake ya kukataa kutia saini mswada wa matumizi ya fedha wa kaunti hiyo uliotengea halmashauri ya usimamizi wa eneo la jiji la Nairobi kiasi cha shilingi bilioni-37.2 hali inayotishia kukwamisha shughuli zake.

Categories
Habari

Shirika la huduma la jiji la Nairobi NMS, lawapandisha vyeo maafisa 68 wa matibabu

Wataalam wa Matibabu wanaohudumu chini ya Shirika la Huduma za eneo la Nairobi  (NMS)  wamepandishwa vyeo  kufuatia agizo ka mkurugenz wa halmashauri hiyo.

Maafisa   68  ambao walipokea barua ya  kupandishwa vyeo ni pamoja  wataalam  wa maabara, wauguzi, wakunga  na  wafanyikazi wa afya wa jamii miongoni mwa wengine.

Hadi sasa Halmashauri hiyo imeongeza jumla ya wafanyikazi wa afya  hadi 108 na itaendelea  kuwapandishwa vyeo kila mwezi.

Akihutubia wafanyikazi wa matibabu ambao wamefaidika na kupandishwa vyeo katika afisi za  halmashauri hiyo  katika  jumba la  Mikutano ya Kimataifa la  Kenyatta, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa  Halmashauri hiyo Kangethe Thuku alisema  halmashauri hiyo itaendelea kushughulikia maswala yanayoathiri wafaanyakazi wa afya katika kaunti ya Nairobi.

Kulingana na Thuku hatua hiyo itawezesha utoaji bora wa huduma kwa wakaazi wa Nairobi. Aliwahimiza madaktari kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Maswala mengine yaliyoshughulikiwa katika mkutano huo ni malipo ya mshahara kwa wauguzi kutekelezwa  kabla ya tarehe 30 kila mwezi, swala ambalo lilikuwa likishughulikiwa, na malipo ya ada za kisheria pamoja na malipo ya wafanyakazi kwa vyama  vyao vya ushirika vya akiba na mikopo..

Categories
Habari

Halmashauri ya Usimamizi wa Jiji la Nairobi yapima wakaazi Korona

Shughuli ya upimaji wa COVID-19 kwa wingi katika Kaunti ya Nairobi imeingia siku ya pili hivi leo katika kaunti zote 17 ndogo za Nairobi.

Halmashauri ya Usimamizi wa eneo la jiji la Nairobi NMS jana ilianzisha shughuli ya upimaji huo bila malipo wa siku mbili.

Akiongea mtaani Kibra, Afisa Mkuu wa Afya katika kaunti ya Nairobi, Dkt. Ouma Oluga alisema kuwa shughuli hiyo ililenga kuwapima zaidi ya watu 200 kwa siku katika kila kaunti ndogo.

Alisema kuwa hatua hiyo inanuiwa kuweka hatua zifaazo huku nchi hii ikinuia kupunguza visa vya maambukizi ya ugonjwa huo.

Dkt. Oluga alisema kuwa halmashauri hiyo inatumai kuwapima takriban watu 6,000 kufikia leo wakati shughuli hiyo itakapokamilika.

Alitoa wito kwa wakazi wa Nairobi kujitokeza kwa wingi akisema kuwa hakuna yeyote atakayekosa kupimwa.

“Ni muhimu sana kwa jiji la Nairobi na hasa sehemu ambazo zina watu wengi kwamba watu wachukulie swala hili kwa uzito,” akahimiza Oluga.

Shughuli hiyo ni ya pili katika mpango sawa na huo uliotekelezwa na halmashauri hiyo ambapo ya kwanza ilitekelezwa mwezi Mei.

Kulegezwa kwa baadhi ya vikwazo vya kuthibiti kusambaa kwa ugonjwa wa COVID-19 humu nchini kumehusishwa na ongezeko la hivi punde la idadi ya visa vya maambukizi hali ambayo huenda ikafanya kanuni kali zaidi kurejeshwa.

Hapo jana, Wizara ya Afya humu nchini ilithibitisha visa vipya 616 vya maambukizi ya ugonjwa huo katika muda wa masaa 24.