Categories
Burudani

Mercy Johnson apendeza kwenye hafla ya kuwekwa wakfu kwa mtoto wake

Muigizaji wa nchi ya Nigeria Mercy Johnson anajulikana kwa umbo lake zuri la kiafrika ambalo yeye huambatanisha na mavazi ya kupendeza.

Mercy alijifungua mtoto huyo kwa jina ‘Divine-Mercy’ mwezi wa tano mwaka huu wa 2020, huko Marekani na wakati uliwadia wa kumweka wakfu kwa Mwenyezi Mungu jambo ambalo ni la kawaida kwa wakristo.

Mwanadada huyo alitikisa mitandao ya kijamii na picha za familia yake kuhusu tukio hilo ambapo alivaa vazi la kupendeza la rangi nyekundu rangi ambayo wote walikuwa wamevalia. Aliandika, “Tuliweka wakfu zawadi ya Mungu kwetu.”

Kulingana na maelezo kwenye akaunti yake ya Instagram, nguo aliyovalia Mercy Johnson ilishonwa na mwanamitindo maarufu Abiodun Shade Sandra ambaye anamiliki kampuni kwa jina “luminee couture” ambayo huvisha watu wengi maarufu nchini Nigeria.

Alimsifia sana mwanamitindo huyo akisema kwamba akiamua kushona nguo hana mchezo. Haijulikani kama mavazi ya watoto na baba yao pia yalishonwa na mwanamitindo huyo.

Mercy Johnson na mume wake Prince Odianosen Okojie walifunga ndoa mwaka 2011 na sasa wana watoto wanne.

Mwezi Novemba Mwaka 2013 Mercy Johnson alipigwa marufuku kuigiza nchini Nigeria baada ya watayarishaji filamu kulalamika kwamba alikuwa amekuwa ghali mno.

Hata hivyo marufuku hiyo iliondolewa mwezi Machi mwaka 2014 kufuatia hatua yake ya kuomba msamaha. Kwa sasa mwanadada huyo ni kati ya waigizaji wanaolipwa hela nyingi mno kwenye filamu za Nollywood.

Categories
Burudani

Rotimi asherehekea mapenzi, siku yake ya kuzaliwa

Rotimi kwa jina halisi Olurotimi Akinisho ni mwanamuziki, muigizaji na mwanamitindo wa Marekani mwenye asili ya Nigeria na ana kibao kipya kwa jina “love somebody”.

Yeye ni mpenzi wa mwanamuziki wa nchi ya Tanzania Vanessa Mdee ambaye wanaishi naye kwa sasa huko Marekani.

Alikuwa ametayarisha wafuasi wake kwa jambo kubwa ambalo angelitimiza tarehe 30 mwezi Novemba mwaka huu wa 2020 ambayo ni siku yake ya kuzaliwa na wengi walidhania kwamba yeye na Vanessa wangefunga ndoa.

Kupitia akaunti yake ya Instagram, Rotimi alizindua kibao hicho akisema, “Hakuna njia bora zaii ya kusherehekea siku yangu ya kuzaliwa kuliko kupitia kueneza mapenzi kupitia kwa wimbo huu wangu na mpenzi wangu.”

Siku ilipowadia mwanamuziki huyo alizindua kibao hicho cha mapenzi na yeye na mpenzi wake Vanessa ndio wanaigiza kwenye video ya wimbo huo.

Mwanzo wa mwezi wa nne mwaka huu, Vanessa ambaye hajakuwa akiendeleza fani yake kama mwanamuziki kama awali, alisema kwamba alikuwa ameamua kuchukua mapumziko na kufurahia mapenzi.

Wawili hao wamekuwa wakionyesha wafuasi wao kwenye mitandao ya kijamii jinsi wanapendana, kuanzia kwa Vanessa kumfundisha Rotimi Kiswahili hadi kwenye kupata michoro sawia kwenye miili yao au ukipenda “tatoo”.

Wawili hao waliamua kuandika majina yao kwenye ngozi ya mwili, Vanessa ana jina la Rotimi kwenye kifua karibu na shingo naye Rotimi ana jina la Vanessa kwenye mkono sehemu ambapo saa huvaliwa.

Mwisho wa mwaka jana wawili hao walizuru Tanzania jambo ambalo wengi walionelea kuwa hatua ya Mdee kujulikanisha mpenzi wake kwa familia yake.

Categories
Burudani

Williams Uchemba afunga ndoa

Muigizaji wa Nollywood ambaye pia ni mchekeshaji kwenye mitandao ya kijamii Williams Uchemba alifunga ndoa kanisani tarehe 21 mwezi Novemba mwaka huu wa 2020 katika kanisa kwa jina “Dominion City Church” lililoko Lekki, katika jimbo la Lagos.

Mhubiri David Ogbueli ndiye aliunganisha ndoa hiyo ya Williams na binti kwa jina Brunella Oscar ambayo ilihudhuriwa na ndugu jamaa na marafiki hasa waigizaji wenza kwenye Nollywood.

Arusi ya kitamaduni ya wawili hao ilifanyika tarehe 14 mwezi huu wa Novemba mwaka 2020 alikozaliwa Brunella, katika eneo la Alor jimboni Anambra nchini Nigeria.

Wote waliohudhuria arusi hiyo ya kanisani kama vile, Rita Dominic, Ini Edo, Chika Ike, Kate Henshaw na Ufuoma McDermott kati ya wengine wengi walivalia nadhifu ishara kwamba hawakuja kucheza.

Aliyezua kioja arusini ni bwana mmoja kwa jina “Pretty Mike” ambaye alifika akiwa ameandamana na wanadada sita wote wajawazito na inaaminika kwamba watoto wote wanaotarajiwa ni wake.


Hata hivyo wajuaji wanaonelea kwamba ilikuwa tu hatua ya kujitafutia umaarufu na kuzua minong’ono mitandaoni jambo ambalo kweli lilitimia.

Akihojiwa na jarida moja la arusi nchini Nigeria, Bi. Brunella alisimulia walivyokutana na Bwana Williams. Alisema kwamba alikuwa akidurusu mtandao wa Facebook tarehe 22 mwezi Novemba mwaka 2016 akapatana na video ya mwanaume akihubiria vijana kuhusu njia mwafaka ya kufuata maishani.

Akamtumia ujumbe kwenye ‘Messenger’ na baadaye akasikia sauti ambayo anaamini ni ya roho mtakatifu ikimweleza kwamba huyo ndiye mume wake.
Brunella na Williams waliwasiliana kwenye Facebook kwa muda kabla ya kukutana ana na kwa ana.

Categories
Burudani

Bado nina matumaini ya kuwa kwenye ndoa, Freddie Leonard

Frederick Leonard au ukipenda Freddie Leonard, amekuwa akiigiza kwenye filamu za Nollywood nchini Nigeria tangu mwana 2008, ni mtu maarufu lakini sio mengi yanafahamika kumhusu.

Maajuzi alihojiwa na jarida la ‘Allure Vanguard’ ambapo alifichua kwamba bado hajaoa na hilo likawa jambo la kuzungumziwa sana kwenye mitandao ya kijamii.

Muigizaji huyo alisema kwamba hajapoteza imani kwenye ndoa, anaamini katika ndoa kwani yeye ni mkiristo na Biblia inahimiza kwamba mtu asiwe peke yake.

“Nataka kuchukua muda wangu kuchagua mke ambaye tutakuwa tunaelewana kwa mambo mengi, sitaki kuharakisha kama wengine ambao ndoa zao huishia kusambaratika.” alisema muigizaji huyo.

Hata hivyo Freddie hajafurahishwa na jinsi waandishi wa habari katika mitandao ya kijamii wameangazia swala la ndoa pekee kati ya mambo yote ambayo alizungumzia kwenye mahojiano yake na jarida la Allure Vanguard.

Alifanya video mubashara kwenye akaunti yake ya Instagram ambapo alitaja mwanablogu mmoja kwa jina “Instablog9ja” akimsuta kwa kuzingatia tu swala la ndoa na kukosea kwenye swala la umri wake ingawaje hakusema umri wake halisi.

Muigizaji huyo mwenye sura ya kuvutia alishangaa ni kwa nini wanablogu wanafumbia macho mambo ya maana aliyogusia kama vile uongozi wa vijana kutokana na maandamano ya kulalamikia ukatili wa polisi, maendeleo ya sekta ya filamu nchini Nigeria almaarufu Nollywood na mengine mengi.

Frederick Leonard alizaliwa katika jimbo la Anambra nchini Nigeria tarehe mosi mwezi Mei lakini mwaka haujulikani.

Babake mzazi aliaga dunia Freddie akiwa na umri wa miaka 20 na mamake akaaga dunia akiwa na umri wa miaka 36.

Alisomea biokemia au ukipenda “Biochemistry” lakini akaingilia uigizaji kama kazi. Amewahi kushinda tuzo kadhaa kutokana na weledi wake katika kuigiza na anashikilia imani kwamba filamu za Afrika zina uwezo wa kukua na kufikia upeo wa ulimwengu mzima.

Ameendelea sana kiasi cha kuwa mtayarishaji filamu kwa sasa na ameahidi kuhakikisha uwepo wa shule za kutoa mafunzo kuhusu uigizaji na uundaji filamu.

Categories
Kimataifa

Jeshi la Nigeria lakana kuwaua waandamanaji

Jeshi la Nigeria limekanusha madai kuwa liliwaua waandamanaji wasio na silaha kwenye mkutano jijini Lagos mnamo mwezi uliopita.

Wanajeshi hao wamedai kuwa walikuwa wakitumia bunduki ambazo hazikuwa na risasi kwenye makabiliano na raia.

Afisa mmoja mkuu, Brigedia Jenerali Ahmed Taiwo aliwasilisha ushahidi wa kanda ya video kuthibitisha madai yake yaliyotolewa kwa jopo la wachunguzi.

Shirika la Kimataifa la kutetea haki, Amnesty International linasema watu 12 waliuawa wanajeshi walipofyatua risasi wakati wa maandamano ya kupinga ukatili wa polisi katika mtaa wa mabwenyenye wa Lekki, jijini Lagos.

Walioshuhudia waliliambia Shirika la Utangazaji la BBC kuwa wanajeshi waliwafatulia waandamanaji risasi.

Waandamanaji wengine 1,000 walikuwa wamekusanyika kwenye lango la kukusanya ushuru katika barabara ya kueleke mtaa wa Lekki mnamo tarehe 20 Oktoba kuzuia magari kutumia barabara hiyo kuu.

Askari waliripotiwa kuonekana kuweka vizuizi katika barabara ya kuelekea eneo la maandamano muda mfupi kabla ya risasi kuanza kufyatuliwa.

Shambulizi hilo lilitokea baada ya siku kadhaa za maandamano dhidi ya kitengo cha polisi cha Kupambana na Ujambazi, SARS, ambacho mienendo ya maafisa imekashifiwa vikalina na raia wa nchi hiyo.

Categories
Burudani

Emmanuella ajengea mamake nyumba

Mchekeshaji na muigizaji wa umri mdogo nchini Nigeria mtoto wa kike kwa jina Emmanuella alijengea mamake nyumba ya kuishi ambayo amemkabidhi hivi maajuzi.

Mtoto huyo wa miaka kumi alitangaza haya kupitia akaunti yake ya Instagram ambapo aliweka picha nyingi zinazoonyesha mambo yalivyokuwa wakati akimkabidhi mamake zawadi hiyo ikiwemo moja yake akiwa mbele ya nyumba hiyo na kuandika,

“Nilikujengea hii nyumba mamangu. Kwa maombi yote, ulivyonitia moyo na ulivyonisaidia. Mama najua ulisema unataka nyumba ndogo tu na ndio hii. Lakini utanisamehe kwa sababu lazima nikamilishe jumba lako kubwa mwaka ujao. Usijali hili halitatufanya twende ahera. Krismasi njema mamangu.”

Emannuella alianza kuigiza na kuchekesha akiwa na umri wa miaka mitano tu chini ya kampuni ya “Mark Angel Comedy” na mamake mzazi amekuwa nguzo muhimu katika sanaa yake.

Kulingana na picha alizochapisha Emannuella, nyumba hiyo imejengwa na kumalizwa vizuri na imewekwa samani za uzuri wa hali ya juu.

Wote ambao walikuwepo kushuhudia hafla ya kumkabidhi mamake zawadi hiyo walionekana wenye furaha akiwemo bwana mdogo anayeaminika kuwa ndugu yake mdogo na bwana mkubwa anayeaminika kuwa babake.

Mark Angel ambaye aligundua talanta ya mtoto huyo na kumpa jukwaa la kuigiza ambapo wanaigiza pamoja pia alikuwepo kwenye hafla hiyo.

Categories
Burudani

Mwanamuziki wa Nigeria Falz awakumbuka walioaga dunia kwenye maandamano

Mwanamuziki wa Nigeria Falz alizindua video ya wimbo wake kwa jina “Johnny” na picha zilizoko zinaangazia madhara ya maandamano yaliyojulikana kama EndSARS.

Falz ambaye huimba kwa mtindo wa ‘rap’ anasema kwamba inakera kuona kwamba maneno ya wimbo huo aliouandika na kuurekodi miaka miwili iliyopita bado yanahusiana na matukio ya sasa nchini Nigeria.

Kwenye akaunti yake ya Instagram, mwanamuziki huyo aliandika kwamba hawatakubalia viongozi na wanajeshi wafiche uzito wa matendo yao maovu na kwamba lazima haki itendeke.

Falz anatumia wimbo wa ‘Johnny’ kuwakumbuka na kuwaenzi wote ambao walipoteza maisha wakati wanajeshi walifyatua risasi kwa umati uliokuwa umekusanyika kwa maandamano katika eneo la Lekki katika jimbo la Lagos tarehe ishirini mwezi Oktoba mwaka huu wa 2020.

Video ya wimbo huo inaanza ikimwonyesha Falz akiwa amelala nchini kama ambaye amekufa huku akiwa amevalia mavazi meupe. Baadaye anaunganisha video ya watu ambao waliumia na wengine kufariki siku hiyo ya mauaji.

Kuna nyingine pia ambayo inaonyesha jinsi wanajeshi hao walikuwa wanafyatua risasi ikiwa na sauti ya mtu ambaye anajaribu kutoa maelezo na kutaja jina la Yesu.

“Hatutasahau mashujaa ambao wameuawa kinyume cha sheria. Kazi hii ni kwa ajili yao. Kwa kila uhai uliochukuliwa kinyume cha sheria, lazima tuhakikishe kwamba tunapata haki.” Aliandika Falz kwenye Instagram.

 

 

Categories
Burudani

“Wayo” Kibao kipya cha mwanamuziki wa Nigeria Kendickson

Kendickson ni mmoja wa wanamuziki tajika nchini Nigeria ambaye nyota yake inazidi kung’aa na sasa ana kibao kipya kwa jina “Wayo”.

Kibao hicho kimetayarishwa na Insane Chips ambaye ni muunda muziki wa Nigeria na sio cha mwendo pole pole sana au kasi ya juu. Wimbo huo ni wa mwendo wa wastani na mtu wa umri wowote anaweza kuucheza.

Katika maneno ya wimbo, mwimbaji anakiri mapenzi yake kwa mpenzi wake. Video ya wimbo “Wayo’ ilielekezwa na Clarende Peters na ina picha za wanaocheza wimbo huo kwa mtindo wa kipekee.

Kendickson alisema kwamba nia yake ni kuwapa mashabiki wake katika eneo la Afrika mashariki muziki mzuri akiongeza kwamba muziki huo umechochewa na mazingira yake ya sasa na pia anataka kuwa mwanamuziki bora zaidi.

“Natumai mashabiki wangu watafurahia wimbo huu” alisema Kendickson. Kwa sasa mwanamuziki huyo anaandaa alabamu yake ambayo ataizindua mwaka ujao wa 2021 pamoja na wakfu wake.

Kendickson ana uwezo wa kuimba aina tofauti za muziki kama vile Afrobeat, Hip Life, muziki wa kisasa na hata wa kiasili.

Ana vibao vingine vya awali kama vile, “jojo” na “Blessings” vyote ambavyo vimetayarishwa na Insane Chips.

Kuhusu maandamano yanayoendelea nchini Nigeria, mwanamuziki huyo anasema kwamba watu wamechoka na uongozi mbaya, wanataka mamlaka yarudishwe kwa raia, nchi iwe ya kidemokrasia ambapo mtu maskini anaweza kusikizwa kama vile tajiri.
Anasema pia kwamba hauwezi kumkanya mtu ambaye anapigania kilicho chake na hilo ndilo jambo ambalo linaendelea nchini Nigeria.

Categories
Burudani

Judikay afunga ndoa

Judikay au ukipenda Judith kanayo mwimbaji wa nyimbo za injili mzaliwa wa nchi ya Nigeria alifunga pingu za maisha jumamosi tarehe 7 mwezi Novemba mwaka huu wa 2020.

Mwimbaji mwenzake katika ulingo wa nyimbo za injili nchini Nigeria kwa jina Mercy Chinwo ndiye alitangaza hayo kupitia akaunti yake ya Instagram. Anaonekana akicheza kwa furaha kwa wakati mmoja kwenye harusi hiyo akiwa amevaa nguo nzuri ya rangi nyekundu na kilemba cha rangi ya dhahabu.

Judikay na mpenzi wake Anselm Okpara walionekana wenye furaha tele wakati wa sherehe hiyo ya kanisani huku akiwa amevalia vazi jeupe la kuvutia na mume wake akiwa amevaa nadhifu.

Wawili hao walifunga ndoa ya kitamaduni mnamo mwezi Agosti tarehe 15 mwaka huu wa 2020.

Judikay amekuwa kwenye fani ya uimbaji wa nyimbo za injili kwa muda ambapo alikuwa anasaidia waimbaji wengine kama “back up singer” lakini wimbo wake kwa jina “More than Gold” ambao alizindua mwaka jana ndio umemjulikanisha na kumpa nafasi ya kipekee katika fani ya nyimbo za injili ndani na nje ya Nigeria.

Kufikia sasa amezindua nyimbo nyingi kana vile, “More than Gold”, “Nothing Else”, “Song of Angels, “Fountain” na “Idinma”.

Mwezi Novemba mwaka jana, Judikay alizindua albamu ya nyimbo 14 kwa jina “Man of Galilee”.

Categories
Burudani

Boungei, Kibao kipya cha Emmy Kosgei

Mwimbaji wa nyimbo za injili Emmy Kosgei ana kazi mpya kwa jina “Boungei” ambayo alizindua rasmi Alhamisi tarehe 5 mwezi Novemba mwaka 2020.

Ameuimba katika lugha yake ya asili ambayo ni “Kalenjin” na ni wa mwendo wa pole kidogo ikilinganishwa na na nyimbo zake za awali kama “Taunet Nelel”.

Neno “Boungei” linamaanisha “Tawala” kulingana na tafsiri ambayo imefanywa kwenye video rasmi ya wimbo huo.

Emmy amemhusisha mume wake Anselm Madubuko, ambaye ni mhubiri nchini Nigeria katika wimbo huo na ulirekodiwa katika kanisa lao kwa jina “Revival Assembly Church” mjini Lagos nchini Nigeria.

Anselm anaonekana mwisho mwisho akiomba kwa lugha ya kiingereza kutumia maneo ya wimbo huo ambayo ni ya kumwita Mwenyezi Mungu atawale.

Watayarishaji wa wimbo huo wa ibada ni kampuni kwa jina “Jubal Entertainment” ambao pia walitayarisha wimbo wake kwa jina “Maloo”.

Baadhi ya maneno ya wimbo huo ni kama yafuatayo;

BOUNGEI Boungei eh eh boungei (Tawala eh eh tawala)

Boungei , boungei baba boungei x2 (Tawala Baba Tawala)

VERSE; 1 Rirei bororiet, rirsot chepyosok ak lagok ( Mataifa, Wanawake, Watoto wanalia …)

Oh oh baba, boungei oh ( oh baba, tawala)

Iluu eh kamuktaindet, nebo yaktaetap mugetut ( Inuka oh Mungu, wewe mwenye kisasi, Zaburi 94;1 )

Boungei boungei ( Tawala … )

 

Tazama wimbo huo hapa;