Categories
Michezo

Limbukeni Afrika ya kati na Namibia watoshana nguvu

Namibia na Jamhuri ya  Afrika ya kati zilitoka sare ya bao 1 katika mchuano wa mwisho wa kundi B  wa mashindano ya kombe la AFCON kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 , uliopigwa katika uwanja wa Cheikha Boudiya Noukchot  nchini Mauritania.

Flory Jean Michael Yangao aliiweka Afrika ya kati  dakika 8 baada ya mapumziko kabla ya  Penuua Kandjii  kusawazisha kwa Namibia  mwishoni mwa mechi na kusajili sare ya pili katika kundi hilo ,baada ya Tunisia na Burkina Faso kucheza sare tasa.

Mashindano hayo kuingia siku ya tatu Jumanne  kwa mikwangurano ya kundi C  ,mabingwa mara tatu Ghana watafungua dimba saa moja usiku dhidi Tanzania wanaoshiriki kwa mara ya kwanza nao Gambia wakumbane na Moroko saa nne usiku.

Mataifa 12 yanashiriki mashindano hayo .

 

Categories
Michezo

Tanzania yasajili ushindi wa kwanza CHAN na kuitimua Namibia

Taifa Stars ya Tanzania ilisajili ushindi wa kwanza katika michuano ya CHAN inayoendelea baada ya kuwaangusha Namibia goli 1-0 katika mechi ya kundi D iliyochezwa Jumamosi usiku katika uwanja wa Limbe.

Farid Mussa ambaye pia alitawazwa mchezaji bora alifunga bao hilo katika dakika ya 65 alitumia makosa ya mabeki wa Namibia walioshindwa kuondosha mpira katika lango lao na kufyatua mkwaju ulimwacha hoi kipa wa Namibia Kamaijanda Ndisiro.

Namibia maarufu kama Brave warriors walijaribu kwa udi na uvumba kurejesha bao hilo bila mafanikio huku kipa wa Taifa Stars Aishi Manula akipangua mikwaju mingi ya Wanamibia.

Matokeo hayo yanafufua matumaini ya Tanzania kufuzu kwa robo fainali wakihitaji ushindi dhidi ya Guinea Jumatano ijayo ili kufuzu kwa robo fainali.

Katika mechi ya awalia ya kundi hilo Jumamosi jioni Zambia walihitaji bao la dakika ya 87 ili kujinusuru na kulazimisha sare ya 1-1 dhidi ya Guinea na kuacha kundi hilo wazi kwa nafasi ya kutinga robo fainali.

Victor Kantabadouno aliwaweka Guinea kifua  mbele kwa bao la dakika ya 58  kabla ya Spencer Sautu kusawazishia Zambia dakika ya 87.

Mechi za Kundi A zinakamilika Jumapili usiku Mali wakichuana Zimbabwe nao  Burkinafasso wapimane nguvu na  wenyeji Cameroon .

Mechi hizo zitabaini timu mbili zitakazofuzu kwa robo fainali ya Jumamosi na Jumapili ijayo.

Categories
Michezo

Guinea na Zambia watema cheche za moto kombe la CHAN

Syli Nationale ya Guinea na Chipolopolo ya Zambia walisajili ushindi mkubwa katika mechi za kundi D kuwania kombe la CHAN Jumanne usiku katika uwanja wa Reunification nchini Cameroon.

Guinea waliisasambua Brave Warriors ya Namibia magoli 3-0 Yakhouba Gnagna Barry mshambulizi wa klabu ya AC Horoya  akipachika bao la kwanza kunako dakika ya 13  kufuatia makosa ya kutoelewana kati ya kipa wa Namibia Edward Maova na difenda  Immanuel Heita aliyetoa  pasi hafifu ya nyuma.

Morlaye Sylla aliongeza bao la pili kwa Guinea katika dakika ya mwisho ya mazidadi kipindi cha kwanza ,huku Guinea wakienda mapumziko kwa uongozi wa 2-0.

Kipindi cha pili Guinea waliongeza mashambulizi wakati wenzao Namibia wakionekana kupotea katika mechi na kulazimika kujihami katika mlango wao .

Hata hivyo katika dakika ya 86  Yakhouba Gnagna Barry alipiga tobwe lililomzidia kasi kipa na kupiga bao lake na pili linalomfanya kuwa mfungaji bora kufikia sasa .

Guinea watarejea uwanjani Jumamosi dhidi Zambia nao Tanzania wapimane nguvu na Tanzania.

Awali katika kundi hilo Tanzania waliangushwa mabao 2-0 na Zambia  Collins Sikombe na Emmanuel Chabula wakipachika bao moja kila mmoja katika kipindi cha pili.

Tanzania walicheza vizuri kipindi cah kwanza lakini wakalemewa kunako kipindi cha pili ingawa kipa Aishi Manula aliwaepushia fedheha zaidi kwa kupangua mikwaju kadhaa.

Categories
Kimataifa

Zaidi ya wanafunzi 300 waambukizwa Covid-19 nchini Namibia

Zaidi ya wanafunzi mia tatu nchini Namibia wameambukizwa virusi vya Corona tangu kurejelewa kwa shughuli za masomo.

Wizara ya afya imesema visa vingi vimetokea katika shule za bweni.

Waziri wa afya, Kalumbi Shangula alisema kanuni za usalama zinapaswa kuzingatiwa ili kudhibiti maambukizi hasa katika maeneo kama vile shule.

Vyombo vya habari nchini humo viliripoti mchipuko wa virusi vya Corona katika shule moja huko Oshikoto ambako kumeripotiwa visa vingi vya virusi hivyo.

Namibia ilifunga shule mwezi Machi kufuatia kuzuka kwa janga hilo na kisha kuzifungua tena mwezi Juni.

Wadau walidai hakukuwa na maambukizi ya ndani nchini humo.

Walimu na wanafunzi wote walihitajika kuvalia barakoa kila wakati ili kuzuia maambukizi ya virusi hivyo.

Wasimamizi wa shule pia walitakiwa kudumisha viwango vya juu vya usafi.

Namibia kufikia sasa imethibitisha kuwa imenakili visa 11,373 vya virusi vya Corona na vifo 123.