Usambazaji wa maji katika baadhi ya sehemu za Kaunti ya Nairobi utakatizwa Jumatano na Alhamisi kutokana na shughuli za ukarabati wa mitambo.
Kampuni ya maji ya Nairobi imesema wahandisi wananuia kufunga moja ya vituo vya usambazaji wa maji ili kufanikisha uboreshaji wa mitambo hiyo ya maji katika maeneo ya Uthiru na Dagoretti.
Kwenye taarifa, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya maji ya Nairobi Nahason Muguna amesema kituo cha maji cha Kabete kinaboreshwa ili kusambaza lita elfu 25 zaidi za maji hadi mitaa ya Karen, Riruta, Satellite, Kawangware na Uthiru.
Maeneo yaliyo karibu na barabara za Naivasha, Ngong, Langata na Waiyaki zitaathirika kutokana na ukarabati huo.
Kituo hicho cha maji kitafungwa kuanzia saa 12 alfajiri Jumatano hadi saa 12 alfajiri Alhamisi.
Kampuni hiyo imewahimiza wakazi watakaoathirika kutumia maji kwa makini huku juhudi zikifanywa za kurejesha usambazaji wa kawaida wa maji.