Categories
Habari

Msichana wa miaka 4 afariki kutokana na mkasa wa moto Mwingi

Msichana mwenye umri wa miaka mine ameaga dunia alipokuwa akitibiwa katika hospitali moja ya kibinafsi huko Mwingi baada ya nyumba ya familia yake kuteketezwa moto na watu wasiojulikana.

Akithibitisha kisa hicho, Kamanda wa Polisi wa Mwingi ya Kati Peter Mutuma amesema wakati nyumba hiyo ilipovamiwa na genge hilo, watu wane walikuwa ndani.

Mtu mmoja alifariki na watatu wakapelekwa katika hospitali za kibinafsi katika miji ya Mwingi na Kitui.

Kisa hicho kilitokea katika Kijiji cha Kivou, Kaunti Ndogo ya Mwingi ya Kati.

Ripoti zinasema kuwa eneo hilo limeshuhudia visa viwili vya utovu wa usalama katika muda wa wiki moja iliyopita.

Wakazi wa eneo hilo wamewanyoshea kidole cha lawama maafisa wa polisi kwa kuzembea katika kukabiliana na hali hiyo ambayo imewasabishia kuishi kwa hofu.

Wakazi hao wametoa wito kwa polisi kuwasaka na kuwakamata washukiwa wa uhalifu huo.

Categories
Habari

Shule moja yafungwa kaunti ya Kitui kutokana na maambukizi ya Covid-19

Shule nyingine imefungwa katika kaunti ya Kitui baada ya mwalimu mmoja kuthibitishwa kuambukizwa ugonjwa wa Covid-19.

Shule ya msingi ya  Waasya iliyoko Mwingi ya kati ilifungwa baada ya mwalimu huyo kugunduliwa kuwa na virusi vya Corona mapema wiki hii.

Haya yamejiri majuma machache baada ya shule ya msingi ya Kithumula Kitui magharibi kufungwa baada ya walimu wawili na mwanafunzi kuthibitishwa kuwa na ugonjwa huo.

Hatua ya kufungwa kwa shule hiyo ilithibitishwa na mkurugenzi wa elimu katika kaunti ya Kitui Salesa Adano.

Adano aliwahakikishia wazazi kwamba wanafunzi wote walipimwa na maafisa wa afya ya umma.

Kwa kujibu wa mkurugenzi huyo, shughuli za masomo zitarejelewa kufikia siku ya Jumatatu baada ya matokeo ya waliopimwa kuthibitishwa.

Mkurugenzi huyo wa elimu alisema mwalimu huyo alikuwa miongoni mwa walimu wengine kumi ambao pia baada ya kupimwa waligunduliwa kuambukizwa virusi hivyo vya Covid-19.

Categories
Habari

Vijana wahimizwa kuunga mkono BBI kwa manufaa yao ya kiuchumi

Vijana kote nchini wamehimizwa kusoma na kuelewa ripoti ya Mpango wa Maridhiano, BBI, kabla ya kufanya maamuzi yoyote kuhusu.

Chama cha wabunge vijana nchini kinasema ripoti hiyo ina uwezo mkubwa wa kunufaisha vijana nchini lakini lazima wajizindue na kushinikiza ajenda zao.

Kundi hilo lilizungumza wakati ambapo kuna maoni tofauti kuhusu ripoti hiyo huku baadhi ya vijana katika Kaunti ya Kitui wakitaka eneo la Mwingi liwe kaunti kiviake.

Wakati uo huo, Mbunge wa Butere, Tindi Mwale ameanza kuwaongoza baadhi ya vijana wa eneo la Magharibi mwa nchi kuunga mkono ripoti ya BBI.

Mbunge huyo anasema ripoti hiyo ni njia bora ya kujumuisha vijana kikamilifu katika maswala ya  utawala.

Katika Kaunti ya Kakamega, baadhi ya vijana wa eneo hilo wameapa kuunga mkono ripoti ya BBI wakisema inashughulikia uwezeshaji wa kijamii na kiuchumi wa kizazi kipya nchini.

Hata hivyo, kundi hilo linawalaumu wale wanaopinga ripoti hiyo, likiwarai Wakenya kujitenga na watu wachache wanaotumia mchakato huo kuigawanya nchi hii.

Categories
Habari

Mwanaume auawa Kitui baada ya kufumaniwa kwenye ‘tendo’ na ng’ombe

Wakazi waliojawa na hasira mjini Mwingi, Kaunti ya Kitui wamemshambulia hadi kumuua mwanaume mmoja mwenye umri wa makamo kufuatia madai ya kumfumaniwa akifanya tendo la ngono na ng’ombe.

Inadaiwa kuwa mwanaume huyo amepatikana katika hali hiyo tata na wapita njia alfajiri ya Jumanne katika eneo la Mavoko.

Walipojaribu kumhoji, mwanaume huyo amekosa kuwa mtulivu na akaanza kukabiliana na watu waliokuwa wamefika katika eneo hilo, hali iliyosababisha makabiliano yaliyopelekea kifo chake.

Maafisa wa polisi wamepashwa habari kuhusu tukio hilo lakini wakawasili wakati mwanaume huyo tayari ameaga dunia na wakaupeleka mwili katika hifadhi ya maiti ya Hospitali ya Mwingi huku uchunguzi ukianzishwa.

Akizungumza katika eneo la tukio, Chifu wa Kata ya Kavuvwani Nicholas Muvengei amewaonya wakazi dhidi ya kuchukua sheria mikononi mwao, akiwahimiza watoe habari kwa polisi wanaposhuhudia tukio lolote la kihalifu.

“Kuuwa si kitu cha kusaidia kwa sababu mtu huyo anaweza kusaidia polisi katika uchunguzi,” amesema Muvengei.

Muvengei ameongeza kuwa eneo la Mavoko limeshuhudia ongezeko la visa vya utovu wa usalama hivi karibuni na kwamba huenda wakazi wamepandwa na jazba ndipo wakatekeleza kitendo hicho.

Naye Loyce Issa ambaye ni mkazi wa eneo hilo ameeleza kuwa amepata habari kuhusu kitendo cha mwanaume huyo kulala na n’gombe na akakimbilia hapo ili kujionea lakini akapata mwanaume huyo tayari ameuawa.

Hata hivyo Issa amewahimiza wanaume watafute starehe kutoka kwa binadamu wenzao badala ya kugeukia mifugo.