Categories
Burudani

Beyonce ajiunga na miito ya mabadiliko ya polisi nchini Nigeria

Mwimbaji na Muigizaji wa nchi ya America Beyonce amejiunga na kampeni inayoendelea nchini Nigeria ya kutafuta mabadiliko kufanyika katika idara ya usalama hasa polisi almaarufu #EndSARS.

Jumanne tarehe 20 mwezi oktoba Beyonce aliandika ujumbe kwenye Instagram akisisitiza haja ya kufutiliwa mbali kwa kikosi cha polisi kinachojulikana kama SARS nchini Nigeria.

Siku hiyo hiyo kulitokea ripoti kwamba polisi walifyatua risasi kwa umati wa watu ambao walikuwa wanaandamana katika eneo la lekki.

Beyonce alifichua kwamba anashirikiana na makundi kadhaa nchini Nigeria kuwapa usaidizi wanaoandamana kwa ajili ya kutafuta mabadiliko nchini humo.

Alisema nia yao kuu ni kutoa matibabu ya dharura, chakula na makazi kwa wanaohitaji.

Kikosi hicho cha “Special Anti-Robbery Squad (SARS)” kimekuwa kikimulikwa sana nchini Nigeria na hata nje kwa sababu ya kile kinachosemekana kuwa ni kutumia nguvu kupita kiasi.

Video ilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha polisi wa kikosi hicho wakiwapiga risasi na kuwaua raia jambo ambalo lilisababisha maandamano katika sehemu kadhaa nchini Nigeria.

Awali Tiwa Savage ambaye ni mwanamuziki nchini Nigeria ambaye aliwahi kufanya kazi na Beyonce alikuwa amemwomba ajiunge na kampeni dhidi ya kikosi cha polisi cha SARS.

Tarehe 11 mwezi huu wa Oktoba mwaka 2020, Inspeka jenerali wa polisi nchini Nigeria Bwana Mohamed adamu alitangaza kuvunjwa kwa kikosi cha SARS na kuundwa kwa kikosi kingine kwa jina “Special Weapons and Tactics SWAT” lakini raia hawakuridhika.

Wengi walitaka wote waliokwenda kinyume na haki za binadamu katika kikosi hicho wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria jambo ambalo Rais wa taifa hilo Muhamadu Buhari aliahidi.

Categories
Kimataifa

Nigeria kuchunguza madai ya dhuluma za polisi

Serikali ya Nigeria imeagiza kubuniwa kwa majopo ya majaji katika majimbo yote 36 kuchunguza madai ya dhuluma za polisi.

Majopo hayo yatapokea na kuchunguza malalamishi kuhusu dhuluma za polisi, zikiwemo zile zinazohusishwa na kikosi maalum cha kukabiliana na wizi wa kimabavu, al maarufu, Sars kilichovunjwa.

Majopo hayo pia yatachunguza visa vya maafisa wa polisi kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandaanaji tangu maandaano yalipoanza juma lililopita.

Hii ni pamoja na jopo huru la uchunguzi lililobuniwa na tume ya kitaifa ya kutetea haki za binadamu nchini humo.

Maelfu ya raia wa nchi hiyo wamekuwa wakiandamana kwenye miji mikuu kulalamikia dhuluma za polisi.

Wametoa wito marekebisho ya idara ya polisi na kushtakiwa kwa wale wanaotekeleza  dhuluma hizo.

Categories
Kimataifa

Huenda jumuiya ya ECOWAS ikaiondolea Mali vikwazo

Jumuiya ya kiuchumi ya eneo la Afrika magharibi, ECOWAS imeashiria kwamba huenda vikwazo dhidi ya Mali vikaondolewa hivi karibuni.

Hayo ni kulingana na arafa iliyokuwa kwenye ukurasa wa twitter wa rais wa muda wa Mali.

Jumuiya ya  Ecowas iliiwekea nchi hiyo vikwazo hivyo vya kuiadhibu baada ya jeshi kumng’atua rais  Ibrahim Boubacar Keïta mwezi Agosti mwaka huu.

Ilishinikiza kurejeshwa kwa utawala wa kiraia lakini licha ya rais wa kiraia,  Bah Ndaw, na waziri mkuu, Moctar Ouane, kuteuliwa, vikwazo hivyo bado havijaondolewa.

Mapema juma hili, rais Muhammadu Buhari wa Nigeria alisema kuwa kungali na maswala yanayohitaji kusuluhishwa kabla ya mahusiano kurejea katika hali ya kawaida.