Categories
Kimataifa

Mtandao warejeshwa Uganda baada ya kufungwa wakati wa uchaguzi mkuu

Huduma ya mtandao imerejeshwa nchini Uganda baada ya kuzimwa kwa siku tano wakati wa uchaguzi mkuu.

kufuatia agizo la serikali, huduma hiyo ilifungwa Jumatano usiku, saa chache kabla ya kufunguliwa kwa vituo vya kupigia kura kwenye uchaguzi mkuu wa siku ya Alhamisi iliyopita.

Hata hivyo, mitandao ya kijamii bado imesalia kufungwa.

Wakati uo huo, msemaji wa chama cha upinzani cha National Unity Platform (NUP), Joel Ssenyonyi, amesema afisi ambapo mawakala wake walikuwa wakiandaa stakabadhi za kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi huo zimevamiwa na wanajeshi.

Ssenyonyi amesema mawakala hao walikuwa wakikusanya fomu za matokeo ya uchaguzi zilizo na ushahidi wa udanganyifu.

Hii ni baada ya makaazi  ya kiongozi wa chama hicho Bobi Wine kuzingirwa na wanajeshi wa serikali.

Bobi alikataa matokeo ya uchaguzi wa urais kama yalivyotangazwa na tume ya uchaguzi nchini humo.

Kulingana na matokeo hayo, Rais Yoweri Museveni ndiye aliyeshinda kinyang’anyiro hicho dhidi ya Bobi Wine aliyeibuka wa pili.

Bobi alishtumu vikali jinsi uchaguzi huo ulivyofanywa, huku akidai kwamba ana ushahidi wa kutosha kuhusu visa vya udanganyifu.