Categories
Habari

Mbunge mteule wa Msambweni feisal Abdalla Bader ameapishwa

Mbunge mteule wa Msambweni  Feisal Abdallah Bader ameapishwa wiki moja baada ya kuchaguliwa kwake.

Bader aliapishwa katika bunge la taifa Jumanne alasiri katika hafla fupi iliyoongozwa na spika wa bunge la taifa Justin Muturi huku akishangiliwa na wabunge wenzake.

Mbunge huyo aliazimia kutekeleza majukumu yake ipasavyo kama inavyohitajika kisheria na wakazi wa eneo bunge lake.

“Nitakuwa mwaminifu na mtifiu kwa katiba ya Kenya. Nitatekeleza majukumu yangu kwa uaminifu,”aliapa feisal.

Katika uchaguzi mdogo ulioandaliwa tarehe 15 mwezi Disemba,  Bader ambaye aliwania akiwa mwaniaji huru, alishinda kiti hicho kwa kura 15,251 dhidi ya kura 10,444 za mwaniaji wa chama cha  ODM Omar Boga.

Kiti hicho kiliwachwa wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa eneo hilo  Suleiman Dori ambaye alifariki alipokuwa akipokea matibabu katika hospitali ya Aga Khan kaunti ya Mombasa.

Categories
Habari

Raila akosoa kauli kwamba ODM imepoteza umaarufu Pwani

Kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga amepuzilia mbali madai kuwa umaarufu wa chama chake unadidimia katika eneo la Pwani.

Akizungumza kwenye kituo kimoja cha runinga humu nchini, Raila amesema chama cha ODM kilishinda uchaguzi huko Kilifi na kudai kuwa madai kwamba chama hicho hakina nguvu katika sehemu hiyo hayana msingi.

Raila amesema kuwa wafuasi wengi wa ODM walimpigia kura kwa wingi Feisal kwa kuwa alikuwa msaidizi wa marehemu aliyekuwa mbunge wa eneo hilo Suleiman Dori.

Feisal Bader, ambaye alishiriki kwenye uchaguzi huo kama mgombea huru aliwashangaza wengi alipojizolea kura 15,251, huku mgombea wa chama cha ODM Omar Boga akipata kura 10,444 kati ya kura 27,313 zilizopigwa kwenye uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Msambweni.

Boga alishindwa kwa kura 4,807 kwenye uchaguzi huo ambao matokeo yake yalitangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC, siku ya Jumanne usiku.

Ushindi wa Feisal na ule wa wagombea wa Wadi za Gaturi, Lake View na Dabaso umeelezewa na wachanganuzi wa maswala ya kisiassa kuwa kigezo kikubwa kuhusu maridhiano baina ya Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga.

Wakati wa kampeini za uchaguzi huo huko Msambweni, Raila alisema kuwa utakuwa kipimo cha umaarufu wa mpango wa maridhiano ya kitaifa, BBI, ambao ni nguzo ya kampeini za viongozi hao wawili za kutaka  kuifanyia marekebisho katiba.

Categories
Habari

Aisha Jumwa na Sifuna wakabiliwa na kesi ya matamshi ya chuki

Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa na Katibu Mkuu wa chama cha ODM Edwin Sifuna wameagizwa kufika mbele ya Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) kuhusiana na matamshi yasiyofaa waliyotoa hivi majuzi.

Katibu wa tume hiyo ya NCIC Skitter Mbugua amesema kuwa wawili hao watafika mbele ya tume hiyo tarehe 21 mwezi huu.

Sifuna anadaiwa kutoa matamshi ya chuki tarehe 11 mwezi huu wakati wa kampeini za uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Msambweni katika Kaunti ya Kwale.

Tume hiyo inasema kuwa matamshi kama hayo yanaweza kuathiri jamii mbali mbali zinazoishi kwa amani katika Kaunti ya Kwale.

Jumwa anasemekana kutoa matamshi sawa na hayo alipokuwa akimjibu Sifuna.

Wawili hao wametakiwa kufika mbele ya tume hiyo, la sivyo wakabiliwe na mashtaka ya kukiuka maagizo ya tume hiyo.

Siku ya Jumanne, mwenyekiti wa tume hiyo Samuel Kobia alishtumu vikali matamshi ya viongozi hao wawili akisema kuwa matamshi kama hayo yanaweza kuzua chuki, kuvuruga amani hasa miongoni mwa Wakenya na wafuasi wa viongozi hao.

Categories
Habari

Ruto ampongeza Feisal kwa kushinda kiti cha ubunge cha Msambweni

Naibu rais, William Ruto amempongeza Feisal Bader kwa kuibuka mshindi kwenye uchaguzi mdogo wa eneobunge la Msambweni.

Feisal alizoa kura 15,251 na kumshinda mpinzani wake wa chama cha ODM, Omar Boga aliyepata kura 10,444 kati ya kura 27,313 zilizopigwa kwenye uchaguzi huo.

Bader ambaye alionekana kuwa mwanasiasa mdhaifu alizima ndoto ya mgombeaji wa chama cha ODM ambaye kura za maoni zilikuwa zimempa ushindi mkubwa.

Kwenye ujumbe wake katika kitandazi cha Twitter, naibu Rais Dkt William Ruto alisema ushindi wa Bader ni ushindi kwa demokrasia.

Wakati huo huu, aliyekuwa seneta wa Machakos, Johnstone Muthama na mbunge wa Belgut, Nelson Koech wameachiliwa huru.

Viongozi hao wawili waliachiliwa huru baada ya kukamatwa kwa madai ya kuchochea visa vya udanganyifu kwenye uchaguzi mdogo katika eneobunge la Msambweni hapo jana.

Muthama na Koech waliachiliwa kwa dhamana ya shilingi shilingi elf-30 kila mmoja.

Muthama alizuiliwa kufuatia vurugu za jana katika kituo cha kupigia kura cha shule ya msingi ya Jomo Kenyatta huko Msambweni. Kituo hicho kilifungwa baadaye.

Mbunge wa Lungalunga, Khatib Mwashetani alinusurika kukamatwa na maafisa wa kitengo cha GSU waliokuwa wamezingira makazi yake.

Categories
Habari

Shughuli za upigaji kura zaendelea kwenye chaguzi ndogo tano nchini

Maelfu ya wapiga kura wanaendelea kujitokeza ili kushiriki kwenye shughuli za chaguzi ndogo katika maeneo matano mbali mbali humu nchini.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inasimamia uchaguzi mdogo wa Eneo Bunge la Msambweni katika Kaunti ya Kilifi.

Aidha, kuna chaguzi ndogo nne za Wadi za Dabaso katika Kaunti ya Kilifi, Kisumu Kaskazini katika Kaunti ya Kisumu, Kahawa Wendani iliyoko Kaunti ya Kiambu na Wundanyi/Mbale huko Taita Taveta.

Chaguzi hizo zinafanyika kwa kuzingatia kikamilifu maagizo ya Wizara ya Afya ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa COVID-19, ikiwa ni pamoja na kupimwa joto na kunawa mikono ama kutumia vieyuzi.

Vituo vya kupigia kura vimefunguliwa saa kumi na mbili alfajiri na shughuli ya upigaji kura inaendelea hadi saa kumi na mbili jioni.

Wapiga kura wanatambuliwa kwa kutumia vifaa vya kielektroniki kabla kuruhusiwa kupiga kura.

Tume ya IEBC imeweka makarani maalum wa kuhakikisha kwamba watu wanavaa barakoa, wanadumisha umbali ufaao na wananawa mikono kabla kuruhusiwa kuingia katika sehemu za kupiga kura.

Hata hivyo, macho yote yameelekezwa kwenye uchaguzi wa Msambweni ambako wakazi wanamchagua mbunge mpya kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa eneo hilo Suleiman Dori.

Ushindani mkali katika uchaguzi huo ni kati ya Omari Boga wa chama cha ODM na mwaniaji huru Feisal Bader anayeungwa mkono na Naibu Rais William Ruto.

Usalama umeimarishwa katika eneo hilo ili kuhakikisha kwamba zoezi hilo linafanyika katika utaratibu ufaao na bila fujo.

Categories
Habari

IEBC yakamilisha maandalizi ya chaguzi ndogo mbali mbali nchini

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC, imethibitisha kwamba karatasi za kupigia kura zimewasili kwenye vituo husika kabla ya chaguzi ndogo za tarehe 15 mwezi huu katika sehemu mbalimbali nchini.

Tume hiyo hiyo imesema kuwa masanduku yenye karatasi hizo yatafunguliwa mbele ya wawaniaji au waakilishi wao kabla ya kupelekwa kwenye vituo vya kupigia kura.

Aidha, IEBC iliandaa kikao na wachunguzi wa chaguzi Jumapili, ikisema tayari imewapatia mafunzo na kuwapa kiapo cha siri maafisa wa chaguzi hizo ndogo.

Tume ya IEBC pia ilishauriana na walemavu ikisema inaazimia kuhakikisha ujumuishaji wa kila mtu katika mchakato wa uchaguzi.

Chaguzi hizo ndogo zitaandaliwa katika Eneo Bunge la Msambweni kwenye Kaunti ya Kwale, Wadi ya Dabaso iliyoko Kaunti ya Kilifi na Wadi ya Kahawa Wendani, Naiorbi miongoni mwa nyingine.

Shughuli za kampeni kwa ajili ya chaguzi hizo zilitamatika usiku wa Jumamosi, masaa 48 kabla ya kura hizo kupigwa.

Uchaguzi mdogo wa Msambweni umeibua ushindani mkali kati ya mgombea wa chama cha ODM Omari Boga na mgombea huru Feisal Bader anayeungwa mkono na Naibu Rais William Ruto.

Categories
Habari

Jamvi la kampeni lakunjwa Msambweni huku uchaguzi mdogo ukinukia

Muda wa kampeni za uchaguzi mdogo katika Eneo Bunge la Msambweni umefika tamati usiku wa manane kabla kuandaliwa kwa uchaguzi huo Jumanne.

Viongozi kutoka sehemu mbali mbali za nchi hii walijumuika na wawaniaji wa kiti hicho wanaowaunga mkono ili kuwapigia debe katika masaa ya lala salama Jumapili.

Gavana wa Kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho aliongoza mkutano wa kumpigia debe mwaniaji wa chama cha ODM Omari Boga katika eneo la Ukunda.

Akihutubia wakazi, Joho alisema, “Mwaniaji wa chama cha ODM atapata ushindi mkubwa sana. Watu wengi wa Msambweni watapigia kura ODM kwa sababu chama hiki bado kina uungwaji mkono mkubwa miongoni mwa wakazi na pia mbunge aliyefariki alikuwa mwanachama.”

Joho alikuwa ameandamana na viongozi mbali mbali akiwemo Katibu Mkuu wa chama cha ODM Edwin Sifuna, Mkurugenzi Mkuu wa chama hicho Oduor Ongwen, wabunge Badi Twalib (Jomvu), Mishi Mboko (Likoni), Abdulswamad Nassir (Mvita), Junet Mohamed (Suna Mashariki), maseneta Issa Boy (Kwale), Mohamed Faki (Mombasa) na wawakilishi wa wanawake Zuleikha Hassan (Kwale) na Gertrude Mbeyu (Kilifi).

Naye Gavana wa Kwale Salim Mvurya alimpigia debe mgombea huru Feisal Bader ambaye pia anaungwa mkono na Naibu Rais William Ruto.

Mvurya aliwasihi wapiga kura wa Msambweni wamchague Bader kwa kuwa ni kiongozi kijana na mkakamavu ambaye ana nafasi nzuri ya kuwahudumia vyema wakazi wa eneo hilo.

Gavana Mvurya aliongeza kuwa ushindi wa Bader utakuwa ni ishara njema kwa nchi nzima kwamba wananchi hawachagui tena chama bali wanachagua kiongozi mwenye rekodi nzuri ya maendeleo na anayeweza kuwaleta pamoja wananchi wa tabaka mbali mbali.

Viongozi wengine walioandamana na Mvurya ni wabunge Khatib Mwashetani (Lunga Lunga), Benjamin Tayari (Kinango), Mohamed Ali (Nyali), Aisha Jumwa (Malindi), Kimani Ichungwa (Kikuyu) na Nixon Korir (Langata) na vile vile maseneta wa zamani Hassan Omar (Mombasa), Johnston Muthama (Machakos) na Bonny Khalwale (Kakamega).

Mbali na Boga na Bader, wawaniaji wengine katika uchaguzi huo ni Charles Bilali na Mansury Kumaka (wawaniaji huru), Marere Wamwachai (chama cha National Vision), Hassan Mwakulonda (chama cha Economic Democracy), Mahmoud Sheikh (Wiper) na Khamis Mwakaonje (United Green Movement).

Wapiga kura Msambweni wanatarajiwa kumchagua mbunge wao mpya Jumanne tarehe 15 Desemba, ili kuchukua nafasi ya aliyekuwa mbunge wa eneo hilo Suleiman Dori ambaye aliaga dunia mwezi Machi.

Categories
Habari

Gavana Mvurya ampigia debe mgombea huru Abdalla Feisal kwenye uchaguzi mdogo wa Msambweni

Gavana wa Kwale Salim Mvurya amekariri kwamba anamuunga mkono mwaniaji huru Abdhala Feisal kwenye uchaguzi mdogo ujao wa ubunge wa Msambweni.

Mvurya amewahimiza wakazi wawachague viongozi kwa misingi ya uadilifu wao na ajenda ya maendeleo.

Gavana huyo amekariri haja ya kuishi pamoja kwa amani ili kuleta maendeleo.

Ameyasema hayo alipokutana na baadhi ya viongozi na wafuasi wa kanisa katoliki huko Msambweni.

“Nataka kuwahakikishia kwamba mimi pamoja na Naibu Gavana tunamuunga mkono [Abdalla Feisal] na tunawauliza mumuunge mkono,” akasema Mvurya.

Kwa upande wake Abdhala amewahimiza wakazi wajiepushe na viongozi wanaonuia kuwagawanya katika misingi ya kidini na kikabila.

Amesema ataendeleza ajenda ya maendeleo ya marehemu aliyekuwa mbunge wa eneo hilo Suleiman Dori kwa vile alikuwa msaidizi wake wa kibinafsi.

“Kila mmoja wetu yuko na jukumu la kuhakikisha kuwa uongozi utakaochaguliwa hapa utakuwa wa kisawasawa, utaleta haki kwa watu wote, utaunganisha jamii na dini zote ili tupate utulivu na amani,” amehimiza Abdalla

Uchaguzi mdogo wa eneo hilo utafanyika tarehe 15 mwezi huu na unafuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa eneo hilo Suleiman Dori.

Abdalla hata hivyo anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa mwaniaji wa ODM Omar Boga.

Categories
Habari

Joho ahimiza Wapwani kuunga mkono BBI

Gavana wa Kaunti ya Mombasa, Hassan Joho, amewahimiza wakazi wa Pwani kuunga mkono mchakato wa jopo la BBI kwa manufaa ya taifa hili.

Joho amesema mchakato wa BBI unaoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga ni wa kuleta umoja na unafaa kuungwa mkono na Wakenya wote.

Amesema mchakato huo wa kisiasa unanuia kukomesha uhasama miongoni mwa jamii za humu nchini kila baada ya uchaguzi mkuu.

Aidha Joho amesema mchakato wa BBI unanuia kuwajumuisha wote na kugawanya ufanisi na amewahimiza Wakenya kuunga mkono mpango huo.

“Mchakato wa BBI utaboresha nchi hii kwa kuhakikisha maendeleo yanafikia jamii zote nchini,” akasema Joho.

Gavana huyo amesema haya alipokutana na wawakilishi wa jamii ya Wakikuyu wanaoishi katika Eneo Bunge la Msambweni katika kaunti ya Kwale.

Joho ambaye pia ni naibu kiongozi wa chama cha ODM alikuwa katika eneo bunge hilo kumpigia debe mwaniaji wa chama cha ODM, Omar Boga, kwenye uchauzi mdogo wa Msambweni utakaoandaliwa tarehe 15 mwezi Disemba.

Kiti hicho kilibakia wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa Bbunge wa eneo hilo, Suleiman Dori, mwezi Machi.

Categories
Habari

Sharlet Mariam ajitoa kwenye uchaguzi mdogo wa Msambweni

Mgombea huru Sharlet Mariam amejiondoa kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi mdogo katika Eneo Bunge la Msambweni utakaofanyika tarehe 15 mwezi Disemba, mwaka huu.

Akiwahutubia wanahabari, Mariam, ambaye alikuwa msaidizi wa Gavana wa Nairobi Mike Sonko amesema sasa atamuunga mkono mwaniaji wa kiti hicho kwa tiketi ya chama cha ODM Omari Boga.

Aliwaambia wanahabari kwamba alifanya uamuzi huo baada ya kukutana na wafuasi wake ambapo walikubaliana kwamba hakuna haja  ya kuufanya uchaguzi huo mdogo kusababisha mgawanyiko.

“Tunataka wanawake wetu hapa Msambweni wasiangamie. Vijana wetu wasiangamie na chama (cha ODM) kiko imara na hapa Msambweni wataona kivumbi,” akasema Mariam.

Baada ya kukihama chama cha ODM, Mariam alitaka kugombea kiti hicho kwa tiketi ya chama cha Jubilee kabla chama hicho kutangaza kwamba hakitajihusisha kwenye kinyang’anyiro hicho.

Kufuatia tangazo hilo, Mariam alilazimika kuwa mgombea huru ambaye aliidhinishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC mwezi uliopita.

Kiti hicho kiliachwa wazi kufuatia kifo cha Mbunge wa eneo hilo Suleiman Dori mwezi Machi mwaka huu.